Ole wao wapelekao kondoo kwa wezi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

WACHUNGAJI wetu hawasikii. Ole wao wachungaji wapelekao kondoo kwa wezi, kwani saa ya anguko imekaribia. Watakimbiza kondoo wao na kondoo watatafuta malisho mapya hata kama yatawakwama kooni.

Nimesikitishwa na kukwaza na kitendo cha wajiitao wachungaji kutetea wizi wa wazi kwa kudai kuwa ni “maono ya Bwana.”

Wachungaji hawa ambao wametuthibitishia bila kuwa wanachochunga ni matumbo yao na wanachojaribu kukwepa ni mahabusi, saa yao imefika kwani kondoo hawatapelekwa machinjioni tena. 

Kuna kundi la wachungaji waliojitokeza kuitetea DECI (Development Entrepreneurship Community Initiative) na kuwatia shime au kuwaacha kondoo wao kuingia kwenye mchezo huu wa upatu. Hawa wanapaswa kutubu na kumrudia Mungu.

 Hakuna wakati wowote ambapo wachungaji wamewatendea vibaya kondoo halafu Mungu akawaachilia tu. Haijawahi kutokea.

Mchungaji yeyote yule ambaye anadai kuwa amepakwa mafuta na Bwana na kwamba ana “Upako” wa Roho Mtakatiku, siku anapoamua kutetea dhambi na kuitafutia maelezo ya Kitaalamu, siku hiyohiyo anajiandikia adhabu mbele ya Mungu

Hii ni kwa kuwa moja ya mambo ambayo Mungu hafanyii mzaha, ni wachungaji wapotoshao.
 
Tunasoma katika kitabu cha Nabii Ezekieli ambapo Mungu anasema, “Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu, nami nitawalaza.” Kauli hiyo au ahadi hiyo inakuja baada ya Mungu kusema maneno makali yasiyo na utata juu ya wachungaji.

Tatizo alilonalo Mungu, kwa mujibu wa Ezekieli, ni kuwa wachungaji wanatumia nafasi zao vibaya; nafasi ambazo zinatokana na kondoo kuwaamini.

Tukikumbuka maneno ya Yesu ambayo yanajulikana kama maneno ya “Mchungaji Mwema,” tunatambua kwanini wachungaji ni lazima wawe waangalifu linapokuja suala la kuchunga kondoo.

Yesu anasema, “Kondoo wangu waijua sauti yangu nao wanifuata.” Ni hii imani ya Kondoo ambayo naona wachungaji wetu wanaitumia vibaya.

Hili tatizo la kufuata sauti za wachungaji limeleta madhara mengi na imefika mahali baadhi ya nchi wachungaji wanaangaliwa kwa woga na shuku. Na hili ndilo ambalo watanzania wanahitaji kuanza kuliangalia.

Kutokana na kuongezeka kwa hali ngumu ya maisha, mwelekeo mbaya wa kiuchumi duniani na zaidi ya yote kutokana na kuongezeka kwa nafasi za kujinufaisha kiujanja, basi tutarajie kuwa muda si mrefu tutaona watu wenye kutumia vyeo vya “uchungaji na upadri” na wenyewe wakijitokeza kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

Lakini, siyo wachungaji wa DECI ambao wamenitibua kichwa wiki hii bali pia kundi la maaskofu ambao wanaamini kuwepo kwao kwenye hafla fulani, basi kunafanya hafla hiyo iwe “Takatifu” na kuwa maneno wanayoyatoa kwenye hafla hiyo basi yakubaliwe kama kwa imani.

Maaskofu hawa katika akili zao wanaamini kuwa wana ujumbe kwa wananchi; ujumbe ambao wameshindwa kuutoa mahali pengine isipokuwa katika meza zao na washirika wa ufisadi.

Viongozi hawa wa dini wamelala kitanda kimoja na wanasiasa na wakati wanasiasa hao wanapopata matatizo basi wachungaji ndio wanakuwa wa kwanza kujionesha kuwa wanawatetea na kuwasafisha.

Kama hao kondoo wanajua wamefanya makosa au wanajua wamefanya dhambi ya aina fulani, basi ni jukumu lao kutubu na kugeuka na kuonesha kuwa walichofanya hakikuwa sahihi.

Ni matumaini yangu hawa mafisadi mambo leo, watatambua makosa yao na badala ya kuwaalika viongozi wa dini ili wapate baraka au waonekane kuwa wameongoka, basi watatangaza kukubali makosa yao na kuonesha kuwa wanajirudi.

Binafsi nitakubali kuongoka kwa fisadi yoyote ambaye atakuja na kusema, “Mimi nilinufaika na kampuni ya Meremeta kwa wizi, na nilichukua Sh. 20 bilioni na sasa nimeona nuru, narudisha zote pamoja na riba yake ya muda wote huu ambayo ni bilioni nyingine saba.” Huyo hata mimi nitampigia kampeni.

Tatizo ni kuwa hakuna hata fisadi mmoja aliyekubali makosa na kusema alichofanya ni makosa na yuko tayari kujirudi na kurekebisha. Badala yake wote wanatafuta kisingizio cha kuelezea ufisadi wao.

Yupo mmoja katika kujitetea kwake amefika mahali ametafuta mtu mwingine wa kumtwisha mzigo wake. Mtu huyo ameona bora awashirikishe ikulu makosa yake lakini bila ya kuthubutu kusema ni nani hasa huko ikulu anayehusika naye.

Kwa kweli ninachotaka kusema leo ni ombi la wazi kwa viongozi hawa wa madhehebu ya Kikristu: Acheni kuwachanganya waumini wenu! Msiwapoteze wale “wa dogo kati ya hawa,” kwani yule Bwana mnaedai kuwa mnamtumikia alisema ole wao wanaopotosha watoto wadogo.

Katika kina cha upendo wake alisema wazi; mtu anayewapotosha watoto hao ni bora angefungwa jiwe shingoni akatupwe baharini. Fikiria msururu wa wachungaji ambao tungewafunga mawe shingoni na kuwaelekeza bahari ya Hindi, tena kupitia maeneo ya Kigamboni!

Nyinyi wachungaji ambao mnachunga matumbo yenu, mliojawa na tamaa ya mali za wizi imekuwaje muendelee kulala kitanda kimoja na ufisadi mkiupepea na kuuimbia mapambio?

Ni mpaka lini mtasimama na wananchi na kuongoza maandamano kupinga udhalimu na kuwa tayari kwenda kifungoni mkiitetea kweli?

Ni mpaka pale mtakapokuwa tayari kujitenga na uongozi wa kifisadi ndipo umuhimu wenu utakapojulikana.

Wale ambao wamewapotosha maelfu ya Watanzania na kuwaingiza katika mchezo wa wizi wa upatu na kwenda kinyume na maneno ya Biblia kuwa “kwa jasho lako utakula matunda ya nchi,” wageuke na watubu.

Wachungaji wasimame leo na kuukana upatu huu na kuwa wa kwanza kuhakikisha maskini wa Mungu walioacha kufanya kazi na kujishughulisha katika “jasho” lao wanarudishiwa fedha zao.

Lakini wito wangu wa mwisho ni kwa wale waumini ambao wanasikiliza maneno ya wachungaji kana kwamba kila walisemalo lina mafuta.

Kumbukeni Mungu hana ubia na mchungaji yoyote na wakati wowote Mungu anaweza kuondoa roho wake toka kwa mmoja na kwenda kumpa wasiyemtarajia. Kumbukeni kisa cha Sauli na Daudi.  

Wachungaji wenu wanapokuja na mipango hii ya maendelo na miradi ya kuwekeza wahojini, wapingeni, na ikibidi waumbueni. Muwe na akili na ubishi wa mbuzi na mioyo yenu ikiwa na utii wa kondoo.

Msikubali kuburuzwa na viongozi wa dini ambao wanatumia Biblia kufanya ufisadi kama walivyofanya wale wamisionari wa awali ambao mkono mmoja walibebe dini na mkono mwingine wakawa watetezi wa ukoloni.

Kama ambavyo sisi wengine tumewapinga viongozi wa kisiasa ambao wanaamini kuwa wao ni zawadi ya Mungu kwa Tanzania, wakati umefika kwa wananchi kuwapinga viongozi wa dini ambao wanaamini kuwa wamepakwa mafuta ili kutuburuza.

Wachungaji wa DECI na wale mliosimama kutetea wizi huu mkitumia Jina la Bwana, mnazo siku saba kugeuka na kutubu. Neno ndilo hilo. Vinginevyo, “Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana.” 

0
No votes yet