Ole wao wasioona alama za nyakati


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

RAIS Jakaya Kikwete na mgeni wake Yoweri Museveni wa Uganda walipata aibu kubwa walipotembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Wakuu wa nchi hao walikumbwa na zomeazomea.

Marais hao, waliohudhuria kwa furaha sherehe za chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kianzishwe, walipokewa kwa mabango ambayo mengine yalimtaka Museveni kumtendea haki kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kiza Besigye.

Kiza Bisigye amekuwa mtu wa kusulubiwa na askari wa Museveni kiasi kwamba dunia sasa inamhurumia na kumwona Museveni kama kiongozi katili asiyeheshimu demokrasia.

Polisi wa Uganda walimzingira Besigye mita chache kutoka nyumbani kwake alipoanza kutembea kuelekea kazini. Walimtaka achague kati ya kurudi nyumbani kwake, kwenda kazini kwa gari au akamatwe kwa kusababisha maandamano.

Akawajibu, “Mnaweza kunikamata iwapo mtataka’’. Wakamkamata. Sura ya Uganda duniani imechafuliwa na vitendo vya polisi dhidi ya Besigye. Kinachofanyika Uganda ndicho kinafanyika Tanzania.

Serikali ya Uganda inapambana dhidi ya Besigye wakati serikali ya Tanzania inanyamazisha sauti ya Mbunge wa Arusha, Godbless Lema!

Wanachogombea, kutembea kwa miguu. Hapa mmoja wao lazima atakuwa mpumbavu. Kutembea ni haki ya kila mtu duniani kote. Kumzuia mtu kutembea ni kuvunja haki za mtu huyo. Anayezuia haki hiyo na kuwaita watu panya, huyo ni mpumbavu.

Lema alidakwa na polisi wakati anatembea kwa miguu kutoka mahakamani alikoshtakiwa anarudi kazini kwake kama alivyokutwa Besigye. Yeye hakuambiwa achague. Alikamatwa na kushtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyo halali.

Ni kweli kuwa kila kuandamana ni kutembea lakini siyo kila kutembea ni kuandamana. Askari wanapofanya gwaride huku wakitembea uwanja nzima utasema wanaandamana? Waumini wanapokwenda au kutoka kwenye nyumba za Ibada hutembea katika vikundi, utasema wanaandamana? Watnanchi wakiupokea au kusindikiza mwenge, utasema wanaandamana?

Katika kamusi ya Kiswahili sanifu iliyochapishwa na Oxford toleo la pili maandamano yametafsiriwa kuwa ni, “Mfuatano au msululu wa watu wengi wanaotembea kuelekea mahali ili kutimiza lengo fulani”. Watu wengi wanaotoka mahakamani watembeeje ili yasionekane kuwa ni maandamano kwa macho ya Kamanda wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji?

Viongozi wetu mpaka leo mikono yao bado inatiririsha damu ya ‘wanawema’ waliouawa na polisi tarehe 5 Januari 2011 katika maandamano ya CHADEMA kutokana na amri ya mpumbavu mmoja tu! Dhambi hii ingali inaning’inia juu ya vichwa vyao mpaka siku yao ya mwisho!

Lema aligoma kuwekewa dhamana katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha hata baada ya kujitokeza  kwa wadhamini waliotimiza masharti yaliyotolewa na mahakama. Hivyo alilazimika kwenda rumande katika gereza la Kisongo kwa siku 14 wakati wenzake wakiachiwa kwa dhamana. Lema alisindikizwa na watu 12 ambao licha ya kutokuwa watuhumiwa au wafungwa waliomba watiwe rumande pamoja naye, wakakataliwa!

Mpumbavu anapopitisha chuma kwenye tanuri la moto hudhani anakidhoofisha kumbe anakiimarisha. Hawa wanampatia usugu!

Wanachotegemea madikteta wa dunia hii ni polisi wenye silaha na vyumba vya magereza. Wananchi wakiondoa hofu au wakishakuwa na usugu navyo hakuna serikali inayobaki imesimama. Mwisho wao huwa mchungu kupita shubiri! Tumeyaona Tunnisa, Misri na kwa Gaddafi.

Godbless alichukuliwa na polisi chini ya ulinzi mkali. Ulinzi mkali ni shilingi ngapi? Mtuhumiwa mwingine alisafirishwa kwa ndege ya jeshi wakitumia mamilioni ya shilingi kutoka Dar es Salaam ha Arusha mahakamani ili akapewe dhamana tu! Waliopaswa kuwa walinzi wa mali na raia wamegeuka na kuwa wafujaji wa mali na watesi wa raia! Mwisho wao umekaribia!

Godbless alisema, “Nakwenda gerezani kupinga ukandamizaji wa haki za binadamu. Sioni ugumu kuchukua maamuzi haya, upendo nilionao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya kufikia maamuzi haya. Jamii ya watu duni imeendelea kuishi katika hali duni ya mashaka na vitisho kwa muda mrefu. Wasifikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha. Wanafikiri tutaendelea kuabudu woga.  Wanafikiri wataendelea kutunyanyasa bila sababu za msingi. Lakini sisi tunajua tutashinda kwa sababu haki tunayoipigania ni makusudi ya Mwenyezi Mungu.” Akaongeza, “Ni afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Hofu na mashaka vimekosa thamani kwangu. Sitomwogopa mtu yoyote awe na silaha au awe na cheo chochote!”

Wapumbavu wamemjenga Lema kwa upumbavu wao. Na sasa inakula kwao!  Nikamkumbuka mpigania uhuru wa Afrika kusini, Solomon Kalushi Mahlangu, ambaye wakati wake wa kunyongwa na makaburu ulipofika alisema, “…damu yangu itakayomwagika, itazirutubisha mbegu zitakazochipua na kuwa mti utakaoleta uhuru wa kweli”.

Lema haililii Arusha na wana Arusha peke yao, bali anaililia na nchi yake, anatulilia na sisi! Kwa kuwa Lema anasimamia haki ya wengi atashinda, Mungu atakuwa upande wake, nao watesi wake wataanguka kwa aibu!

Alikataa kudhaminiwa, lakini alikubali wafuasi wake wadhaminiwe ili yatimie yaliyoandikwa kuwa. “Ni mimi hapa nikamateni. Waacheni hawa waende zao ili lile neno lipate kutimia, kuwa katika wote ulionipa, baba sikumpoteza hata mmoja”.

Namwonea wivu kijana huyu, kuingiza jina lake katika orodha ya mashujaa wema wa Bara la Afrika akiwa na umri mdogo. Kama ilivyo kwa jehanamu, kuipata raha ya milele hutokana na uliyoyafanya  hapa duniani!

Lema amesema yuko tayari kwa kifo wakati Katibu wa CHADEMA mkoa wa Arusha Amani Golugwa amesema, “Hatuogopi silaha wala magereza kwani tuko wengi majasiri ambao tuko tayari kupoteza chochote hata ikibidi uhai wetu ili haki, ukweli na usawa vipatikane!”

Kwa msimamo huu Lema hatakufa peke yake! OCD Mwombeji ataua wangapi!  IGP Said Mwema ataua wangapi! Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsa Vuai Nahodha ataua wangapi! Kwa nini viongozi wetu mnataka kulazimisha kisasi? Ole wao walioshindwa kuona alama za nyakati!

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet