Omar Mzee ondoa uchafu ujenge uchumi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KAMA kuna mawaziri wachache walioteuliwa kuongoza wizara inayosimamia moja ya nyanja ambayo waziri ameisomea hasa, basi Omar Yussuf Mzee hawezi kupitwa na wengine.

Anaongoza Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, inayoendelea kuwa chini ya rais mwenyewe, kama ilivyokuwa kwa wakati wote wa uongozi wa Amani Abeid Karume uliofikia kikomo Oktoba mwaka huu.

Moja ya masomo muhimu katika taaluma ya uongozi wa fedha ni takwimu; na hili ni eneo hasa waziri Omar amebobea baada ya kupita vyuo mbalimbali.

Kumbukumbu za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar zinaonyesha Omar ana shahada ya pili katika fani ya takwimu aliyoipata baada ya kumaliza mafunzo Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia (Australia National University) 1983-1985.

Kabla ya hapo, alisomea shahada ya kwanza ya masuala ya takwimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1979-1982. Kwa mwaka mmoja, 1987-1988, alipata mafunzo zaidi ya takwimu na maendeleo, alipokuwa Chuo Kikuu cha Nehru, India.

Hapana shaka, hicho ni kiwango cha juu kielimu kinachomfanya awe mstahili hasa wa kushika uwaziri katika wizara hiyo.

Omar pia ni kada mzuri wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye safari hii alimua kutogombea ubunge katika hali ambayo haikueleweka kwa wengi. Alikuwa na siri aliyoiweka moyoni mwake na imekuja tu kudhihirika baada ya uchaguzi.

Dk. Ali Mohamed Shein, rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM) anayeongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa, naona anamfahamu Omar.

Anamfahamu kwa kuwa naye karibu kama msomi mwingine. Anamfahamu zaidi kwa miaka mitano akiwa mmoja wa manaibu waziri katika serikali ambayo Dk. Shein alikuwa Makamu wa Rais.

Kama Omar aliamua asitetee kiti cha ubunge cha Kiembesamaki huku watu wengi wakishangaa na kutojua hasa sababu, na ghafla jina lake kusikika katika walioteuliwa kuwa wawakilishi wa kuteuliwa na rais, na wiki chache baadaye kutangazwa ndiye waziri wa wizara hii nyeti, ni dhahiri “wanafahamiana vema.”

Omar anao uzoefu wa uongozi serikalini. Ameongoza idara na wizara. Katika miaka ya mwanzo ya 1990, alikuwa Afisa Mdhamini wa wizara ya nchi mipango akifanyia kazi kisiwani Pemba.

Baadaye aliteuliwa Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Mipango na Vitega Uchumi wakati ikiongozwa na Ali Juma Shamhuna 1995-2000. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2000 uliomuweka madarakani kwa mara ya kwanza Rais Karume, Omar aliteuliwa nafasi hiyohiyo, katika Ofisi ya Waziri Kiongozi.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, akiwa ameshinda kiti cha ubunge jimbo jipya la Kiembesamaki, Unguja, aliteuliwa Naibu Waziri wa Ulinzi. Lakini, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza jipya Februari 2008, baada ya kuvunja la kwanza kutokana na mvumo wa kashfa ya Richmond, alimteua naibu waziri katika Wizara ya Fedha na Uchumi.

Ukweli amepewa dhamana kubwa. Anaongoza wizara muhimu mno kwa uchumi wa nchi na ustawi wa watu wa Unguja na Pemba. Lakini uchumi haukui na watu hawapati ustawi iwapo taratibu za kifedha haziendi vizuri katika nchi.

Katika serikali yoyote ile, kwa nchi tajiri au masikini, hii ndiyo wizara husika katika mipango na utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa kodi.

Ndiyo wizara inayosimamia malipo ya serikali kwa watumishi wa serikali na mengine yoyote yaendayo nje ya serikali. Watumishi wote wa serikali hulipwa kutokana na mapato yanayokusanywa na wizara hii.

Bajeti ya serikali ya kila mwaka inayoelezea matokeo ya mipango ya maendeleo mwaka uliopita wa fedha na matarajio kwa mwaka unaokuja, huandaliwa kwa kutegemea hesabu na rekodi za mipango ya maendeleo zilizothibitishwa na wizara hii.

Wizara ya Fedha ndiyo kiungo na nguzo kati ya bajeti na utekelezaji wa bajeti. Kila wizara na idara zinazojitegemea hupata fedha za matumizi kutoka wizara hii.

Kwa maneno machache, niseme “kuzorota kwa ufanisi wa utendaji kwa wizara hii, ni kuanguka kwa ufanisi kwa serikali yenyewe.”

Uzoefu unaonyesha lawama nyingi huangushiwa wizara ya fedha pale wizara nyingine na taasisi za serikali zinapokosa mgao kamili wa kibajeti.

Kwa Zanzibar, hii ni wizara inayolaumiwa sana kwa jambo hilo. Inalaumiwa kwamba haisimamii vema mapato na mali za serikali. Inaendekeza mianya ya kisheria na kulea tatizo la wizi wa mapato ya serikali na uharibifu wa mali za serikali.

Kuna suala la misamaha ya kodi ambayo wajuzi husema inachangia sana kuiibia serikali. Misamaha ya kodi inasababisha rushwa inayonufaisha viongozi wakuu wa wizara na wakubwa zao.

Isitoshe, kupitia misamaha ya kodi, wananchi wanaumizwa kimatumizi kwa kulipia mafungu ambayo washirika wa rushwa wameyaficha mifukoni. Mfanyabiashara aliyedaiwa rushwa, anaongeza bei ya bidhaa alizoingiza.

Kadhalika, zipo kumbukumbu za wale wanaosamehewa kodi, pengine kwa visingizio vya kilaghai, huziingiza bidhaa sokoni na kuziuza kwa bei ya juu kama vile zililipiwa kodi. Haya yanatokea kwa bidhaa kama sukari, mashuka na saruji. Hivi karibuni, wizara hii ilisamehe kodi kwa mfanyabiashara aliyeingiza nchini saruji lakini ilipotolewa tu bandarini, ikamwagwa sokoni na kuuzwa.

Ni udanganyifu wa kifisadi uliohalalishwa kifisadi na wakuu wa wizara kwa sababu za kifisadi si vinginevyo.

Zipo taarifa kuwa wakuu wa wizara waliwahi kuandika barua kwa viongozi wa taasisi chache za serikali na kuagiza mapato yasipelekwe benki. Ni agizo la kifisadi lililofanywa kwa malengo ya kifisadi. Fedha za serikali zisipelekwe benki ziende wapi?

Itakuwa ni mifukoni mwa wezi kama inavyotokea kwa wale wanaoiba kwa kutumia utaratibu wa wafanyakazi hewa. Na eneo hili bado linaendelea kunufaisha maofisa waandamizi wizara ya fedha wakishirikiana na mawakala wao idara za utumishi za wizara na taasisi zikiwemo ofisia za wakuu wa mikoa.

Hivi itabidi Waziri Omar atoke aeleze ni vipi wizi kupitia wafanyakazi hewa umekoma. Mpango wa wafanyakazi hewa umekuwa ukiinyima serikali mamilioni ya shilingi kila mwezi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: