Omba Mungu ‘watu hao wawili wapatane’


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WAKATI Prince Bagenda akipanda jukwaa la kongamano la Katiba Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam, ili kuzungumza, mtu mmoja aliyekuwa nyuma yangu alisema kwa sauti ndogo maneno ya kiingereza yaliyokuwa na tafsiri kuwa, “Anakwenda kwenye eneo hasa lililotegwa mabomu.”

Akiwa amevalia shati jeupe na makobadhi miguuni, Bagenda aliyetambulishwa kama mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kongamano hilo kwenye ukumbi wa Nkrumah, alihutubia hadhara lakini maji yakazidi unga, akalazimika kutomaliza muda wake.

Ingawa baadhi ya wahudhuriaji idadi kubwa wakiwa ni wanavyuo, walimlazimisha kuacha kumalizia alichojiandaa kueleza akiwa amebakiza dakika moja kati ya kumi walizotengewa wawakilishi wa vyama vya siasa, sikuona tatizo lolote kwa kile alichoeleza. Naona alifanya vizuri nikizingatia mazingira ya hadhara.

Dakika kumi kwa chama kilichothibitisha sasa kuachwa nyuma na sehemu kubwa ya wasomi, ni nyingi. Ukitaka kujua kwa kiasi gani muda huo ulikuwa mrefu, muulize Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Momose Cheyo, ambaye alipotimiza dakika sita tu, alilazimika kuachia jukwaa kutokana na kelele za upinzani kutoka kwa umma uliokuwepo ukumbini.

Kuna siri moja kubwa katika alichokizungumza na hicho ndicho kilichomfanya adumu jukwaani – alitenganisha CCM na Serikali. Kwanza alikiri kuwa ajenda ya katiba si ya CCM isipokuwa imeichukua kwa sababu ndiyo matakwa ya wengi. Na akawataka wananchi, wakiwamo wana-CCM, kuhakikisha wanadai haki kwa vile si kila kitu wananchi hupewa na serikali yao kabla ya kukidai.

Matatizo ambayo wachambuzi wanayaona kwenye muswada wa sheria ya marejeo ya Katiba ulioandaliwa na serikali, kwa Bagenda ameona ni mzigo wa serikali waliouandaa, wala si CCM.

Ndipo akili yangu ikarejea kwenye mjadala uliopo miongoni mwa wana-CCM sasa kuhusu ama waendelee na utaratibu wa kofia mbili; yaani kuwa na kiongozi mkuu serikali ambaye pia ni kiongozi mkuu wa chama, au kiongozi kuwa na kofia moja tu kati ya hizo.

Kwa kuzingatia nilichokiona katika ukumbi wa Nkrumah jijini Dar es Salaam, ni rahisi sasa kwa CCM kufikiri kuwa njia rahisi kwake kuliko zote ni kutenganisha kofia hizo mbili.

Itakuwa rahisi CCM kujitenga kutoka na serikali isiyopendwa ili kujinusuru. Na inaonekana CCM huenda ikafanya vizuri iwapo itaamua kufuata mfumo huo.

Hata hivyo, kama itafikia hatua hiyo, ni lazima ijiridhishe kuwa inafanya maamuzi yenye faida katika kipindi kirefu kuliko kifupi. Ni lazima wale wanaotaka mabadiliko wakumbuke kauli ya Mwalimu Nyerere aliyesema chama na serikali vinaweza tu kuwa katika hali nzuri iwapo kofia hizo mbili zinashikwa na watu wawili wanaopatana.

Kwa maneno yake mwenyewe, Nyerere alisema; “Omba Mungu wapatane.” Kabla CCM haijafanya mabadiliko inayotaka kufanya, inapaswa kwanza ifikirie mazingira yatakayokuwapo wakati chama au serikali kitakapoongozwa, kwa mfano, na watu wa makundi mawili makubwa yaliyopo ndani ya chama hicho kwa sasa.

Katika utafiti niliofanya, nimebaini kuwa nyingi ya nchi ambazo viongozi wa serikali huwa pia viongozi wa chama ni zile zenye mfumo wa utawala unaoongozwa na Bunge si serikali.

Nchi kama Uingereza walio vinara wa mfumo wa madaraka wa kibunge unaozuia kuwepo rais au makamu wa rais, kiongozi wa chama cha Labour au Conservative kitakachokuwa madarakani, ndiye anayekuwa Waziri Mkuu, ambaye ni mkuu wa Serikali.

Kiongozi wa chama anayeongoza chama chake kushindwa uchaguzi, mara nyingi huachia ngazi kupisha mtu mwingine aongoze. Huyo ndiye atakuwa sura ya chama hadi uchaguzi mwingine utakapofika. Na atakaposhinda anaendelea kuwa kiongozi wa chama chake.

Hapa nchini kwetu hali ni tofauti. Katika mfumo wetu wa utawala, rais ndiye mkuu wa serikali na nchi. Ni mfumo unaotumika pia nchini Marekani. Mara nyingi rais anakuwa si kiongozi wa chama chake.

Katika nchi kama Tanzania, rais ana nguvu kubwa kiasi cha kuwa ni vigumu kuendesha utawala utakaomfanya awe chini ya mtu mwingine. Katika nchi zinazoongozwa na waziri mkuu, anakuwepo mfalme au rais ambaye hufanya majukumu mengine, ambayo kwetu yangeweza kufanywa na rais.

Kwetu, rais ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Katika nafasi yake hiyo, rais ndiye hupandisha vyeo wanajeshi kuanzia ngazi ya kanali.

Rais anateua mawaziri na manaibu wao. Anateua makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao. Anateua wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Anateua wakurugenzi wa mashirika ya umma na mabalozi wanaoiwakilisha nchi katika nchi za nje.

Tusisahau pia kwamba rais wa Tanzania anateua baadhi ya wabunge na ana mamlaka ya kuvunja bunge anapoona halimsaidii. Rais huyohuyo pia ndiye anayepaswa kuwa mgeni rasmi katika matukio yote ya kitaifa. Ni majukumu mengi na makubwa kwelikweli.

Katika mazingira haya, ni vigumu kwa rais mwenye nguvu hivyo kufanya kazi chini ya mtu mwingine anapokuwa ndani ya chama chake. Ni mtazamo wangu kuwa ili mfumo wa kutenganisha kofia mbili ufanye kazi vizuri, ni muhimu kwanza kuwekwa utaratibu wa kupunguza madaraka ya rais.

Tanzania ina tofauti kubwa na Marekani ingawa sote tunatumia mfumo wa urais. Rais Barack Obama, hawezi kuteua Mwanasheria Mkuu (AG) bila ya kwanza uteuzi huo kupitishwa na bunge. Bunge likikataa, hawezi kulazimisha.

Hapa nchini, rais anaweza kuteua AG na majaji 20 wa mahakama kwa mpigo, na hakuna yeyote anayeweza kuhoji na akazuia hilo. Rais yeyote wa Marekani anajua madaraka yake yana mipaka lakini rais nchini petu anajua yuko juu ya sheria.

Ndiyo, Obama hana tatizo wakati anapokwenda kwenye chama chake na kukuta ana bosi kule. Hajazoea ubosi wa katika kila eneo. Katiba yetu inampa rais mamlaka yanayomfanya awe juu ya sheria. Hili ni jambo la kulitazama kwa makini.

Kama CCM itaamua kutenganisha kofia hizi mbili bila ya kwanza kuangalia nguvu na mamlaka makubwa ambayo rais wa nchi anayo; hatutakuwa na la kufanya zaidi ya kufanya kile Mwalimu Nyerere alichokisema miaka mingi iliyopita – Tuombe Mungu wapatane.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: