Osama kupata mjukuu mwingereza


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Omar bin Laden, mtoto wa Osama

MTOTO wa mtuhumiwa namba moja wa ugaidi duniani, Osama bin Laden aitwaye Omar, amepanga kuzaa mtoto na mwanamke raia wa Uingereza katika tukio linalodaiwa kuzusha balaa nchini hapa.

Mwanamke huyo, Louise Pollard, mwenye umri wa miaka 24 ni mzungu na tayari amewahi kuzaa watoto wawili wengine kwa njia ya kupandikizwa mbegu.

Pollard alitangaza Jumamosi iliyopita kupitia kituo cha televisheni cha ITV cha Uingereza kwamba amepata mtu wa kumlipa ili azae naye mtoto lakini hakutaka kumtaja kwa jina.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti la The Sun la nchi hiyo ulibaini baadaye kwamba Pollard alikuwa tayari amefanya mazungumzo na kukubaliana na Omar bin Laden juu ya kumzalia mtoto.

Mtoto huyo wa nne wa Bin Laden mwenye umri wa miaka 29, amemuoa mwanamke wa mwingereza, Jane Felix Browne, mwenye umri wa miaka 54 ambaye hawezi kuzaa kwa vile umri wake wa kuzaa umepita.

Tangu wapenzi hao wafunge ndoa mwaka 2007, serikali ya Uingereza imekuwa ikimkatalia mtoto wa Laden kuingia nchini humo kwa madai kwamba hilo linawaweza kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Sheria za Uingereza, hata hivyo, zitampa haki Omar kuingia na kutoka ndani ya nchi hiyo atakavyo kama atafanikiwa kupata mtoto na mwanamke yeyote raia wa nchi hiyo.

Wakati Omar alipoona na mwanamke huyo ambaye sasa amesilimu dini na kuwa mwislamu akitumia jina la Zaina Mohamed Al Sabah Bin Laden, wananchi wa Uingereza walilalamika kwamba “mtoto huyo wa gaidi” alikuwa anataka kupata uraia wa nchi hiyo ndiyo maana alifunga ndoa.

Umri wa mwanamke huyo unalingana na umri wa mama yake Omar aliyefahamika kwa jina la Najwa, na ndiyo maana ndoa hiyo ilizua maswali mengi.

Kutokana na ukweli kwamba mtoto huyo wa Osama amekataliwa kuingia nchini Uingereza, ndoa hiyo ilifungwa mara mbili; kwanza nchini Misri na baadaye, Jeddah , Saudi Arabia ambako ndiko iliko asili ya Bin Laden.

Mwanamke huyo ana asili ya eneo la Cheshire na kabla hajaolewa na mtoto wa Bin Laden tayari alikuwa ameolewa na wanaume tofauti mara tano.

Katika ndoa zake hizo, mwanamama huyo wa kizungu alifanikiwa kupata watoto watatu ambao wote ni watu wazima hivi sasa, lakini juhudi zake za kutaka kuzaa na Omar zimekwama kwa sababu za kiumri.

Katika hali ya kawaida, mwanamke anakuwa na uwezo wa kuzaa hadi katikati ya miaka ya 40 na ni mara chache sana kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 50 kupata watoto.

Mtoto huyo wa Osama amedaiwa kuhuzunishwa sana na kushindwa kupata mtoto kwa mkewe huyo na inadaiwa mara ya mwisho walifanya jaribio la kutaka kupata mtoto kwa njia ya kupandikiza mbegu Aprili mwaka huu.

Baada ya mpango huo kushindikana, ndipo sasa Omar na mkewe wameamua kuchanganya mbegu zao na kuzipandikiza kwenye tumbo la Pollard ili wapate mtoto.

Wanandoa hao walifahamiana na Loiuse Pollard kupitia mtandao wa watu wanaotafuta watu wa kuwazalia watoto kwa kutumia mbegu zao za uzazi.

Mpango wa sasa wa Omar na mkewe ni kumpa Louise yai lenye mbegu zao lakini kama itaonekana mbegu za Jane zina matatizo na haziwezi kutoa mtoto, itabidi mwana wa Bin Laden achanganye mbegu zake na za binti huyo ili wapate mtoto.

Vyovyote vile itakavyokuwa katika njia hizo mbili, Uingereza inajiandaa kupata mjukuu wa Bin Laden katika kipindi cha ndani ya mwaka mmoja kutoka sasa.

0
No votes yet