Othman, Makinda: Kilio cha katiba mpya kiko kwenu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman

TAIFA limepata mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa mihimili miwili, Bunge na Mahakama. Viongozi waliochaguliwa wanakalia ofisi hizo wakati huu ambao taifa linakabiliwa na changamoto kubwa ya katiba.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kilio kikubwa kinachopazwa na umma ni madai ya katiba mpya.

Madai haya yemepamba moto kutokana na msukumo mpya kwa sababu moja tu, kwamba pamoja na ukweli kwamba taifa hili tangu mwaka 1992 liliingia katika mfumo wa vyama vingi baada ya kazi kubwa iliyofanywa na tume ya Jaji Mkuu mstaafu, Francis Nyalali, bado sheria zetu nyingi zinaakisi mfumo wa chama kimoja.

Katiba ambayo ni sheria mama pamoja na kufanyiwa marekebisho kadhaa ili kukidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi, bado inaakisi mfumo wa chama komoja.

Wapo wanaojenga hoja nyepesi kwamba katiba ya sasa haitaji kuandikwa upya, wanadai kwamba imeweka misingi yote muhimu ya kisheria yanayotoa uhuru wa wananchi kushiriki katika utawala wan chi yao.

Hoja hizi zinapewa nguvu zaidi na wale walioko madarakani wakiamini kwamba hali iliyoko sasa inawalinda na kuwapa fursa ya kuongoza kwa utashi wao.

Hawa wanang’ang’ania katiba iliyopo kwa sababu, kwao inawapa nguvu ambazo aghalabu hutumika kukanyaga haki za wengine.

Kwa kifupi katiba ya taifa letu, ni katiba ya kiserikali zaidi. Aliyekalia kiti au ofisi ya umma anakuwa na nguvu na uwezo wa kufanya lolote hata kama umma haukubaliani naye.

Hii ni katiba iliyoshonwa na kujisimika mfumo wa wateule wachache katika jamii kujiimarisha madarakani na hata pale umma unapochoshwa nao, inakuwa kazi kubwa na nzito kuwaondoa.

Kwa mfano, kumekuwa na kilio cha miaka mingi juu ya haki za binadamu. Mojawapo ni haki ya msingi ya kila raia kushiriki katika kuchagua na kuchaguliwa.

Suala la mgombea binafsi limekuwa tete kiasi kwamba serikali inaamini kuwa ndiyo yenye haki ya kuamua juu ya haki za kuzaliwa za watu wake.

Kumekuwa na hoja zinazojengwa juu ya madaraka ya kila muhimili wa dola na jinsi kila mmoja unavyopora madaraka ya mwingine.

Kwa mfano, kumekuwa na hoja kuwa madaraka ya rais ni makubwa mno kiasi kwamba katika kutekeleza wajibu wake, wapo watu wanaodandia kwenye madaraka yake kinyemela.

Ipo mifano mingi tu inayoeleza jinsi madaraka haya yanavyotumika ovyo, mara nyingi si na rais, ila na wale wanaomzunguka.

Kuna wakati fulani wasaidizi wa rais walitumia vibaya nafasi yao kwa kuchomeka jina la mhalifu mmoja katika orodha ya wafungwa waliokuwa wapate msamaha wa rais wakati wa kumbukumbu za uhuru wa taifa.

Kuna mifano mingi tu: Ukitazama kwa kina orodha ya watu wenye madaraka mbalimbali katika taifa wanaoteuliwa na rais, ni vigumu kwa hakika kusema kwamba hao wanaoteuliwa, wote rais anawafahamu.

Rais wa taifa hili huteua waziri mkuu, mawaziri na manaibu mawaziri, makatibu wakuu, manibu katibu wakuu, wakurugenzi wote wa wizara na taasisi za serikali zinazojitegemea.

Rais huteua mabalozi wote, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya; huteua majaji akiwamo Jaji Mkuu; makatibu tawala na makarani wengine. Orodha ni ndefu.

Ukiacha jina la waziri mkuu ambaye hulazimika kuidhinishwa na Bunge, wengine wote hakuna wa kuhoji au walau kutoa baraka za uteuzi huo.

Katika mazingira hayo, ni uongo wa mchana kuamini kwamba eti rais atakuwa anawafahamu wote anaowateua na katika mfumo wa utawala kama wa kwetu ambao rushwa imeota mizizi, ni rahisi sana rais kuchomekwa watu na kuwateuwa kuongoza ofisi za umma.

Hali hii imeshuhudiwa katika maeneo mengi; mara majina yanapowekwa wazi juu ya uteuzi fulani, umma hushindwa kujua ni kitu gani hasa kimesababisha hao walioteuliwa kupewa nafasi hizo. Wengi wamekabidhiwa nafasi walizonazo kwa sababu ya kujuana, kulindana, au kulipa fadhila.

Hata pale watu wanapoboronga inakuwa ni vigumu mno kwa umma kusema waondoke. Kwa sababu hawawajibiki kwa umma ingawa wamekalia ofisi za umma.

Mfumo wa kisheria wa namna hii hauleti sura inayoakisi mfumo wa siasa wa vyama vingi, ambao kila nafasi ya ofisi ya umma ni lazima ipatikane kwa ushindani.

Bunge letu pamoja na kujitutumua hapa na pale, bado ni bunge lililodhibitiwa vilivyo na serikali (utawala); rais ni sehemu ya Bunge, akitaka anaweza kulivunja kama ataoona linahatarisha madaraka yake.

Hata kile kinachoitwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais (impeachment) kwa mujibu wa sheria zetu, ni jambo ambalo ni ndoto kufanikiwa.

Katika mfumo kama huo ambao kwanza rais akishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni mshindi ukiungansha na uwezekano mdogo wa kushitakiwa na Bunge, na kuitazama madaraka yaliyorundikwa kwa kiongozi huyo, demokrsia ya maamuzi ya wengi inakuwa ngumu kutekelezeka.

Ni kwa kutazama hali hii inapotokea changamoto kubwa kama ya kilio cha katiba mpya wakati huo ukiwa na viongozi wakuu wapya wa mihimili miwili ya dola, yaani Bunge na Mahakama, inakuwa ni kama neema fulani kwa taifa.

Tanzania sasa ina Jaji Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman na spika mpya, Anne Makinda.

Ni matarajio ya wengi kuwa viongozi hawa watasaidia umma katika kiu yao ya kupata katiba mpya inayoakisi mfumo wa vyama vingi.

Kufanikisha hilo watakuwa wametoa mchango mkubwa kwa taifa na bila shaka taifa litawakumbuka kwa hilo. Ni muhimu wakasaidia kuendesha harakati hizi.

0
No votes yet