Padri Karugendo amekata minyororo


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 04 February 2009

Printer-friendly version
Padri Privatus Karugendo

KAVULIWA upadri kwa Padri Privatus Karugendo kumejadiliwa na watu wengi bali kuna kitu kimoja wengi wanakubaliana nacho: Ameonewa.

Nilimpelekea Karugendo ujumbe wa kumpongeza na kumwasa asijione kama kashindwa bali kashinda kifungo cha ukimya na unafiki.

Padri Karugendo ametumikia kifungo cha zaidi ya miaka tisa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa. Ni kwa msingi huu wengi wanaona ameonewa na kumwaibisha Papa Bendikto XVI ambaye ni gwiji la mabadiliko katika kanisa.

 Je, papa anayedaiwa kushiriki uamuzi, alipitiwa au ametumiwa kama mhuri kuhalalisha visa vya bosi wa Karugendo, askofu wa jimbo la Rulenge Severin NiweMugizi?

Je, hatua hii inalijenga kanisa au inalibomoa? Mbona Yesu alipopelekewa yule mwanamke aliyetuhumiwa kwa uzinzi, alimtaka maelezo na ndipo akaamua, “Asiye na dhambi awe wa kwanza kutupa jiwe?”

Leo hii, kanisa la Vatikana chini ya rais wake, Papa Benedicto XVI linafanya mashauriano na baadhi ya wanamapinduzi ya kiroho juu ya “Sakramenti Takatifu ya Ndoa.”

Harakati hizi, kwa upande mwingine, zinaongozwa na askofu mwenye mke, Emmanuel Milingo toka Zambia ambaye ameunda jumuia yake iitwayo “Married Priest Now (MPN)” –  “Mapadri ingia katika ndoa sasa.”  

Dunia inakumbuka jinsi gwiji huyu wa theolojia na uponyaji alivyolitia kanisa msukosuko pale alipoamua kuachana na ukapela na kumuoa Dk. Maria Sung (48) toka Korea ya Kusini.

Ndoa hii iliyofana ilibarikiwa na Mchungaji Sung Myung Moon wa kanisa la Unification mwaka 2001.

Kanisa Katoliki, kwa nguvu zake zote, lilifanikiwa kumnasa na kumrejesha Milingo kwenye kundi; akakana mkewe, kurejea Vatikana alikofanya maombi na kufunga kabla ya kupelekwa uhamishoni nchini Argentina.

Kwa kitambo kidogo kanisa liliona kama limeshinda kumbe wapi. Milingo alimrudia mkewe na kuendelea na kazi yake ya uponyaji na kuishi maisha ya ndoa.

Milingo, mwanamapinduzi na mwanatheolojia asiyeshindwa na anayejua anachofanya, ameibuka upya jijini New York, Marekani akiwa na mkewe. Amekwenda maili moja mbele kwa kuanzisha jumuia inayoitwa Mapadri ingia katika ndoa sasa.

Kanisa limemtimua tena baada ya kuwapa daraja la uaskofu mapadre wanne waliooa nchini Marekani. Hao ni Padri George Augustus Stallings Jr., wa Washington, Peter Paul Brennan wa New York, Patrick Trujillo wa New Wark New Jersey na Joseph Gouthro wa Las Vegas, Nevada.

Katika kutaka upatanisho Milingo alikaririwa akisema, “Hakuna upatanisho mzuri wa kulinusuru kanisa… kama kuangalia familia na ndoa.” Hadi sasa kuna mapadri waliooa wapatao 150,000.

Milingo ameishaitangaza jumuia yake na ameishakutana na mapadri waliiooa wapatao 1,000.

Tukirudi kwa Karugendo, kuna haja ya kanisa kuanza mchakato wa kujali upya useja kwa kuzingatia maneno ya Mtume Timetheo ambayo tutayakariri huko mbele.

Wale wanaopinga useja kwa makasisi wanadai kuwa hata Petro, Papa wa Kwanza (kama kanisa linavyotuaminisha), alikuwa ameoa. Vilevile ukisoma Biblia hakuna sehemu hata moja Mungu anapozuia mapadri kuoa wala kuzuia masista kuolewa.

Kitu kingine kinachofanya wanaopinga useja wa kulazimishwa kwenye kanisa la Roma ambao umekuwapo kwa takribani miaka 1,000, ni kuongezeka kwa kashfa za uzinzi na ulawiti miongoni mwa mapadri na uzinzi kwa masista.

Karugendo amekuwa muwazi na kuepuka dhambi ya unafiki. Je, ni mapadri na maaskofu wangapi wana vimada wao hata watoto? Kuna padri mmoja mwenye majina ya SNM ana mtoto Arusha.

Tukariri maneno ya Timotheo kwenye Timotheo ya Kwanza, Sura ya 3 mistari 1-12, anasema ukiitaka kazi ya uaskofu umetaka kazi njema.

Askofu awe mume wa mke mmoja, mtu wa makamo, asiwe mpenda mvinyo na pesa na mtu anayeweza kuitiisha familia yake. Je, maaskofu wa Kikatoliki wanazo sifa hizo?

Vilevile Timotheo ya Kwanza, Sura ya 4 mistari 1-4, anasema wazi kuwa kutakuja wakati wengi wataanguka wakizitii roho chafu na itikadi za kishetani; kwa kutumia unafiki wa waongo tena kwa ugumu wa chuma. Wanaozuia ndoa na kutetea kuacha kula baadhi ya vyakula...

Ni katika mafunzo haya ya Timotheo inaonyeshwa kuwa watawa au masista wawe na umri si chini ya miaka 60 kwani chini ya hapo bado wanahitaji kuolewa na kuzaa watoto. Je, masista wetu wapo?

Kwa vile wengi wameishatia mikono kwenye kesi ya Karugendo, tutatumia historia kama shahidi ili umma na kanisa viamue upya na viamue vizuri.

Papa Paulo V (1605-1621) alipotaka madanguro yote ya Roma iliyokuwa na watu 100,000 na madanguro 6,000 yavunjwe, waumini walikuja juu wakisema kuwa kufanya hivyo kutafanya mapadri wawatongoze wake zao.

Papa Grigori XV (1621-1623) alipoamuru kisima karibu na nyumba ya watawa kikaushwe, alishtuka kukuta mafuvu ya vichanga zaidi ya 6,000.

Albert The Magnificient wa Humburg, Ujerumani, mnamo mwaka 1477 alipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa wanawake wapatao 11,000 kwenye jimbo lake walikuwa wamewekwa kinyumba na watawa.

Msemo kuwa Padre ni “kuwa mume wa wanawake wote,” ulianzia hapa na ukawa na maana zaidi ya inayoeleweka.

Akiwaonya Mapadri wake, Albert alisema "Si non caste, tamen caute;" yaani kama huwezi kuoa basi kuwa mwangalifu. Yaani ufanye mambo yako kwa usiri.  Je, huu ni usiri au unafiki? Karugendo kalishinda hili. Amekata minyororo.

Hivyo basi ni wakati muafaka wa kulirudisha kanisa kwenye ukweli kwa kuruhusu mapadri waoe na masista waolewe. Tena itakuwa rahisi maana wawili hawa wanajuana vilivyo; ni suala la kutangaza kuachana na usiri na unafiki, vinginevyo tendo lipo na halina ubishi.

Kufanya hivyo kutarejesha hata imani ya waumini kwa watumishi wa Mungu ambao kusema ukweli kwa sasa ni hatari na ni uzembe kuwaamini hasa katika masuala ya ndoa au kuwa karibu na wapendwa wetu.

Kwa haya machache, kuna haja ya kumpongeza ndugu yetu na padri wetu Privatus Karugendo kwa kukata mikatale/minyororo na kuushinda unafiki.

Isitoshe, huu siyo mwisho wa maisha na ajuaye nini kitatutokea siku ya mwisho, si mwana wala nani, isipokuwa Baba Mwenyewe.

Karugendo amwachie Baba baada ya kanisa lake kumuangusha. Asirudi nyuma. Aandike na kuelezea aliyoona ni dhambi kuyaeleza. Atasaidia.

Mwanzo wa kushinda mawazo mgando ni kuasi na haya ndiyo matokeo ya kuelimika vilivyo. Akina Yesu, Plato, Sophocles, Martin Luther na wengine walikuwa waasi walioishia kuwa wateule.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)