Palestina: Timu inayotokea uhamishoni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version

MASHABIKI wa soka nchini, wanatarajia kushuhudia kwa mara ya kwanza, pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Taifa Stars na Palestina kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kiingilio cha chini katika pambano hilo kitakuwa Sh. 1,000 wakati cha juu kitakuwa Sh. 10,000.

Pambano hilo, mbali ya kuziandaa timu zote mbili kwa ajili ya mashindano ya kimataifa, litasaidia kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Timu ya soka ya Palestina inaandaliwa na Shirikisho la Soka la Mamlaka ya Palestina (PFA). Shirikisho hilo lilizaliwa mwaka 1952, na halikuwa linatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hadi mwaka 1998, baada ya kuanzishwa rasmi utawala wa Mamlaka ya Palestina.

Wakati pekee ambao Palestine ilipanda nafasi ya juu katika chati ya ubora wa FIFA ilikuwa Aprili 2006 iliposhika nafasi ya 115. Palestina ilifurahia nafasi hiyo kwani ilipanda kutoka nafasi ya 191 mwaka 1999.

Hivi sasa Palestina inashika nafasi ya 178 wakati Stars iko nafasi ya 123.

Tofauti na Taifa Stars, Palestina imekuwa na wakati mgumu katika maandalizi na ushiriki wa mashindano ya kimataifa kutokana na kukabiliwa na vikwazo kutoka Israel.

Katika miaka yote hiyo, tangu ilipotambuliwa na FIFA haikuwahi kucheza mechi ya mashindano katika uwanja wake wa nyumbani hadi Oktoba 26, 2008 ilipoumana na Joradan.

Pambano hilo lilifanyika kwenye uwanja wao mpya wa Faisal Al-Husseini mjini Al-Ram kaskazini mwa Jerusalem na iliisha kwa sare ya 1-1.

Historia

Kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizokuwa zikitawaliwa na wakoloni, soka ilikuwa ikichezwa Palestina ilipokuwa ikitawaliwa na Uingereza. Kilikuwepo chama cha soka kilichoitwa Palestina/Eretz Israel kilichoanzishwa mwaka 1928 na kutambuliwa na FIFA mwaka 1929.

Klabu za soka zilizokuwa zinashiki ni za Kiarabu, Kiyahudi na za polisi na askari wa Kiingereza katika eneo hilo kipindi kati ya Vita I ya Dunia na uhuru wa Israel mwaka 1948.

Mechi za kufuzu kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 1934 na 1938 zilichezwa chini ya chama cha Palestina/Eretz Israel zikihusisha zaidi wachezaji wa Kiyahudi na Waingereza.

Lakini Mamlaka ya Palestina iliomba rasmi uanachama FIFA na ikakubaliwa mwaka 1998.

Palestina ‘huru’ ilicheza mechi za kwanza za kirafiki dhidi ya Lebanon, Jordan, na Syria Julai 1998. Mwaka uliofuata, timu hiyo ikiwa chini ya kocha mwenye asili ya Israel na Kiarabu, Azmi Nasser ilishiriki mashindano ya nchi za Kiarabu mwaka 1999 ambako ilishika nafasi ya pili baada ya kuzishinda Syria, Qatar, na Falme za Kiarabu.

Katika mashindano hayo, Palestina ilifungwa na wenyeji Jordan tu. Juhudi za Palestina kutaka kufuzu kucheza fainali za Kombe la Asia mwaka 2000 na Kombe la Dunia mwaka 2002 hazikuzaa matunda lakini ilipata ushindi dhidi ya Hong Kong na Malaysia.

Mwaka 2002, PFA ilimwajiri Nicola Shahwan kuwa kocha mkuu. Shahwan, ambaye alizaliwa Beit Jala, alikulia uhamishoni Chile na alikuwa na uhusiano na Wapalestina waliokuwa wanaishi Santiago.

Kocha huyo aliwaingiza kwenye kikosi wachezaji wanaoishi uhamishoni kama kina Roberto Bishara, Roberto Kettlun, Edgardo Abdala, Francisco Atura na Pablo Abdala mzaliwa wa Argentina.

Wachezaji wengine kutoka Amerika Kusini waliingizwa katika kila mashindano ya mwaka 2002, 2004, 2006 na pamoja na mazingira hayo magumu Palestina imekuwa ikitoa upinzani mkali.

Matatizo

Shirikisho la Soka la Palestina hukabiliwa na matatizo katika kuandaa timu hiyo iweze kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Hata mazoezi tu huwa kazi nzito. Hii hutokana na kunyimwa viza za kusafiria zinazotolewa na Israel kwa wakazi wa Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Kwa hiyo wachezaji wengi wa Palestina hukusanywa kutoka nje—Chile na Marekani. Kitendo cha serikali ya Israel kuzuia viza kilisababisha Palestina kushindwa kushiriki mashindano mengi.

Novemba 2006, wachezaji wote kutoka Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza walinyimwa viza.

Oktoba 2007, mechi muhimu ya marudiano ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia kati ya Palestina na Singapore haikuchezwa kutokana na timu kunyimwa viza. Mei 2008, timu ilizuiwa kwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Asia.

Mgogoro wa kisiasa kati ya Palestina na Israel ndio hasa umekuwa ukiathiri maendeleo ya wachezaji. Tariq al Quto aliuawa na majeshi ya Israel na mshambuliaji Ziyad Al-Kord alizuiwa kusafiri na nyumba yake iliharibiwa.

Mgogoro kati ya Israel na Ukanda wa Gaza mwaka 2008/ 2009 wachezaji wa Palestina, Ayman Alkurd, Shadi Sbakhe na Wajeh Moshtahe walikuwa miongoni mwa majeruhi wa vita.

Katika kikosi kilichokuja Tanzania, wachezaji kadhaa waliokuwa Palestina walilazimika kuomba viza kwenda Jordan ambako waliungana na wenzao kutoka Jordan, Ujerumani, Misri, Poland na Algeria ambako kocha mkuu wa sasa, Mousa Bezaz amesema wanacheza soka ya kulipwa.

Kwa hiyo Palestina si dhaifu ila kutokana na kushindwa kucheza mechi za kirafiki na mashindano imejikuta ikkosa alama muhimu za kuipandisha katika chati ya ubora. Hivyo, Stars itakumbana na Palestina imara na bora.

0
No votes yet