Paulsen tutakupa ushirikiano, wewe tupe ushindi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version

KOCHA mkuu mpya wa Taifa Stars, Jan Borge Paulsen amelonga; “Watanzania nipeni ushirikiano kwa manufaa ya soka ya Tanzania.”

Paulsen ameomba ushirikiano huo akijua kwamba hiyo ni moja ya silaha muhimu za kupata ushindi uwanjani katika kampeni za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

“Watanzania, wapenzi wa michezo, viongozi wa klabu, wadhamini, shirikisho la soka na waandishi wa habari zote tuwe na mwelekeo mmoja wa kusukuma mbele mafanikio,” alisema.

Tayari mbele yake kuna mechi ya kirafiki dhidi ya Misri Jumatano ya Agosti 11, 2010 jijini Cairo, Misri.

Paulsen, aliyewasili nchini Jumamosi usiku tayari ametangaza kikosi cha kuivaa Misri akiwarejesha kundini kipa Juma Kaseja wa Simba na kiungo wa Yanga Athumani Idd Chuji.

Wachezaji hao vipenzi walitemwa katika mazingira ya kutatanisha na mtangulizi wake Marcio Maximo wa Brazil.

Kila aipoulizwa kuhusu wachezaji hao alioa majibu kuwa ni watovu wa nidhamu. Hakufafanua aina ya utovu wa nidhamu hadi siku moja kabla ya kuondoka.

Alidai kwamba Kaseja alifurahia Stars kufungwa mabao 4-0 na Senegal na pia alimchongea kocha huyo kwa wadhamini wa Taifa Stars, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) baada ya kumkata posho.

Paulsen amerejesha imani kwa wapenzi wa soka kwa kuwaita wachezaji wanaofikiriwa kuwa nyota na muhimu kwa Taifa Stars.

Kaseja huenda akaonyesha tofauti kuanzia mechi hiyo ya kirafiki hasa ikizingatiwa, Stars ilichapwa mabao 5-1 zilipokutana mara ya mwisho chini ya Maximo.

Baada ya Stars kufundishwa na makocha wengi wa kigeni, wakiwemo Bukhard Pape wa Ujerumani na Maximo, bila mafanikio, kiu ya wadau wa soka na hasa Watanzania ni kuona Stars inashinda mechi muhimu na kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.

Kumbukumbu zilizopo ni Taifa Stars kutwaa Kombe la Challenge kwa mara ya kwanza mwaka 1974 chini ya wazalenzo hayati Paul West Gwivaha na Joel Bendera ambao waliipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1980.

Tanzania ilisubiri hadi mwaka 1994 Syllersaid Mziray alipoiwezesha Taifa Stars kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili. Mwaka 2001 ni Mziray na Boniface Mkwassa waliotwaa Kombe la Castle.

Ni kutokana na matokeo hayo Watanzania wana kiu ya mafanikio chini ya makocha wa kigeni na jahazi hili sasa liko chini ya Paulsen.

Ili kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 zitakazofanyika Gabon na Guinea ya Ikwete, Stars itakumbana na Algeria, Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Algeria na Morocco zimekuwa na mafanikio makubwa katika soka ya Afrika na zina vikosi vizuri. Algeria iliyoitoa Misri katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa, ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini na iliitoa kamasi England.

Japokuwa Afrika Kati haina historia ya kutisha, Stars inapaswa kujiandaa vilivyo kuhimili vishindo vyovyote kutoka timu hiyo.

Kwamba wachezaji wamebadilika, wana uzalendo na nidhamu, wanawahi mazoezi ni wimbo uliochosha masikioni. Kinachohitajika ni ushindi.

Paulsen ajue watu atakaofanya kazi nao uwanjani kila siku ni binadamu wenye viwango tofauti vya nidhamu, hivyo lazima awe na saikolojia ya kuishi nao.

Wachezaji hao ni vijana wenye hulka tofauti; baadhi yao bado wana tabia za kitoto, wanahitaji kuvumiliwa na wajue fursa zilizopo mbele yao ili watimize wajibu wao kwa taifa.

Paulsen ajue pia kwamba hakuna taifa lolote duniani lenye wachezaji wenye nidhamu kwa asilimia 100. Lakini pia hakuna taifa lililojaa wachezaji wasio na nidhamu kwa asilimia 100.

Tutahitaji kuona akidhibiti nidhamu ya wachezaji lakini kwa watovu wa nidhamu atoe maelezo yanayoeleweka badala ya kusubiri simu ya mwisho kama alivyofanya Maximo.

Kwa hiyo atapata ushirikiano wa dhati alioomba kutoka kwa Watanzania, ambao huhudhuria mechi uwanjani na kushangilia kwa nguvu, lakini naye atupe ushindi.

0
No votes yet