Pengo amkemea Lowassa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo, amesema kanisa siyo mahali pa “kujisafisha na kujijenga kisiasa.”

Amesema kanisa halipaswi kufanyiwa majaribio ya kugeuzwa kuwa uwanja wa watu kujisafisha na kujijenga kisiasa, limeeleza gazeti la kanisa Katoliki, Kiongozi.

Pengo alikuwa akikemea kilichotokea Ifakara, mkoani Morogoro, 19 Machi 2012, ambako Edward Lowassa “alihutubia” sherehe za kuzinduliwa kwa jimbo jipya la Katoliki.

Mbali na kuzinduliwa kwa jimbo, sherehe zilihusu kusimikwa kwa Askofu Salutaris Libena kuwa askofu mwasisi wa jimbo hilo.

Gazeti la Kiongozi, toleo la 30 Machi 2012, lilikuwa likinukuu Radio Tumaini inayomilikiwa na jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kardinali Pengo ni askofu mkuu jimbo kuu la Dar es Salaam.

Amesema, “… jambo ambalo ni lazima kulikwepa, ni kwamba kwa namna yoyote, kanisa katoliki halipaswi na lisifanywe uwanja wa siasa; lisigeuzwe kuwa ni uwanja wa mapambano kwa wanasiasa; wanasiasa wana ya kwao, wafanye shughuli zao hukohuko.

“Sio mtu anashindwa kujieleza katika ulingo wa siasa, anakuja kukimbilia ulingo wa Kanisa na hapo anaanza kujinadi na kutoa maoni na vitu vingine kama hivi. Hii si sawa na hiyo ndiyo athari inayoweza kujitokeza iwapo hatutalinda mfumo wa kanisa,” amesema.

Katika hali isiyo ya kawaida, kwenye sherere za kanisa Ifakara, mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, aliyepewa heshima ya kukaribisha Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alikacha maelekezo hayo na kumwita Lowassa kwanza.

Hatua hii ndiyo Kardinali Pengo amelaani kuwa ilikuwa kinyume na ratiba iliyopangwa. “Lowassa hakualikwa kama mgeni rasmi na hakuwa miongoni mwa wageni walioandaliwa kuzungumza lolote wala kupanda jukwaani, bali alichomekwa.”

Amesema ni kweli Lowassa “…alialikwa afike, lakini sio kama mgeni rasmi kiasi kwamba asimame azungumze yale aliyoongea. Hiyo haikuwapo; haikuwapo kwa sababu wamekuja wageni wangapi ambao wangesimama na kuongea….”

Gazeti linamnukuu Bendera akisema, “Kabla sijamkaribisha Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, ningependa kwanza kutambua uwepo wa Mheshimiwa ndugu yetu, Edward Lowassa na ninamkaribisha kwanza aseme nanyi.”

Bendera alipohojiwa na mwandishi huyu juu ya tukio hilo, alisema alifanya kazi yake ya kutambulisha wageni wa kiserikali, kama alivyotakiwa na wenyeji.

“Kama walitaka nisimtambulishe Lowassa wangeniambia. Nilitakiwa kutambulisha wageni wa kiserikali, wawe wastaafu hata walioko madarakani. Mimi nilifuata ratiba niliyopewa na wenyeji wangu.

Aliongeza, “hata wageni wengine maalum kama Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambao hawakuwapo niliwatambulisha na kutoa salamu zao, kama wangekuwapo wangezungumza,” alisema.

Bendera hakusema kwa nini alitambulisha wageni ambao hawakuwepo kwenye sherehe hizo.

Kwa upande wake, Lowassa amesema alialikwa kuhudhuria sherehe hizo. Alipoulizwa iwapo alielezwa kuwa angetakiwa kuhutubia, alisema nafasi aliyopewa na Bendera ilikuwa ya “kusalimia tu.”

“Mimi nilialikwa na pale nilipewa nafasi kusalimia…Ebu ngoja kwanza niwapigie simu walionialika, nitakupa uzungumze nao baada ya dakika kama tano…” alisema kisha akakata simu.

Alipotafutwa baadaye, simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Kardinali Pengo amesisitiza kuwa mwanasiasa yeyote, kulingana na mazingira, anaweza kualikwa, hata kama katika siasa ana vita au mambo yanayofanya agombane na wenzake.

“Hili halifanyi kanisa liseme usije kwetu, hapana.  Huyu ni mwamini; mkewe ni mkatoliki na yeye mwenyewe si kwamba ana uhasama na kanisa katoliki; pia ukimwalika mkewe (Regina Lowassa), kwanini mume asije…” alisema Kardinali Pengo.

Hata hivyo amesema, “Sasa kwanini waliingiza mpango wa kumwita Lowassa, aje kuzungumza na hata kutoa matamko ya mambo ya ajira; mambo ambayo ni mazuri lakini hatukutegemea yatoke upande wake. Tungetegemea kama Rais Mstaafu (Mwinyi) angesema, yangeeleweka kwa niaba ya serikali.”

Kabla protokali kuvurugwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Yuda Thadeus Rwa’ichi aliongea na kumwalika Bendera ili amwalike mgeni rasmi, Mzee Mwinyi.

Siku za karibuni, Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu, Februari 2007 kufuatia  kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, amekuwa akiibukia katika makanisa.

Katika makanisa Lowassa amechanga  mamilioni ya shilingi na kupata fursa ya kutoa kauli kuhusu anachoita “ukosefu wa ajira kwa vijana nchini ni bomu linalosubiriwa kulipuka.”

Akiwa Ifakara, Lowassa alisema Kanisa Katoliki, katika mipango yake, likumbuke miradi inayoweza kuwawezesha vijana kujiajiri ili kupunguza tatizo la ajira kwa vile serikali imeshindwa.

Hata hivyo, Kardinali Pengo anasema,  “Matukio ya Kanisa wanasiasa wanaweza kuhusishwa; wakafika na kutekeleza majukumu yao, lakini ninachosisitiza ni kwamba, yasichukuliwe kama mwaliko wa Kanisa. Kanisa lina mtindo wake wa kuchukua msimamo kwamba tunamwalika huyu sisi kama Kanisa Katoliki.”

Akatoa mfano amesema, “Mimi naweza kumwalika mwanasiasa akaja tukashirikiana katika shughuli hiyo; mara ngapi ninamwalika Mzee Mwinyi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam; lakini kamwe nisingeweza kusema mwaliko wangu ni mwaliko wa kanisa katoliki.

Amesema mwaliko wa kanisa unatamkwa na wale wenye mamlaka rasmi na “kwa kibali cha Jumuiya ya Maaskofu. Wakitamka, hiyo inakuwa ni kauli au tamko la kanisa katoliki.”

Kardinali Pengo amesema imetokea parokia zikakurupuka kualika wanasiasa bila kibali wala askofu wa jimbo kujua.

“Huko ni kukiuka misingi; kabisa ni kukiuka misingi…. kama unaalika mtu iwe ni katika ngazi ya parokia, lazima askofu wa jimbo ajue na kama ni level (ngazi) ya Baraza la Maaskofu, Mwenyekiti lazima ajue; ni lazima,” amesisitiza.

Kwa mamlaka ya juu, Pengo amesema ni Baba Mtakatifu pekee, anayeweza kutamka kitu peke yake kikasemwa ni cha Kanisa katoliki.

Amesisitiza, “Ni papa peke yake anayeweza kutamka kitu ambacho ni cha kanisa. Daima yeye akitamka, ni sauti ya kanisa katoliki.”

Ametumia nafasi hiyo pia kufafanua kauli iliyowahi kutolewa na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini kuwa “Kikwete ni chaguo la Mungu.”

Kardinali Pengo amesema, kauli ya Kilaini haikuwa na haiwezi kuwa kauli ya kanisa kwa kuwa haikufuata hatua “ili lieleweke ni tamko la Kanisa Katoliki Tanzania.”

Amesema anashangaa baadhi ya watu, kwa makusudi, wanazidi kung’ang’ania kauli ya Kilaini kuwa ni tamko la kanisa katoliki.

“Nilishaeleza kuwa hilo sio tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kiasi kwamba hata mimi ningetamka kitu cha namna hiyo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lina haki ya kuniuliza nimepata wapi authority (mamlaka) ya kutamka kitu cha namna hiyo, amenukuliwa akifafanua.”

0
Your rating: None Average: 3.8 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: