Piga nikupige kinyang’anyiro cha ubunge CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Gumzo

KINYANG’ANYIRO cha ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimebeba wengi – washindani na wasindikizaji.

Mkoani Dar es Salaam, wanachama wa CCM 96 wamejitosa kuwania nafasi nane za uteuzi. Bali wanaoonekana kuwa washindani katika mkoa huu, hawazidi 20.

Katika jimbo la Kigamboni pekee, wana-CCM 18 wamechukua fomu kupambana na mbunge wa sasa, Abraham Mwinchumu.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema ushindani mkubwa upo kwa wagombea wanne – Mwinchumu, Philis Magese, Mariam Kambi na Brigedia Jeneral Aroon Othman.

Jimboni Temeke, mbunge wa sasa, Abas Mtevu anakabiliwa na kibarua kigumu. Ananyukana na wanachama wenzake 13. Hata hivyo, bado anayo nafasi ya kushinda.

Katika jimbo jipya la Segerea, Makongoro Mahanga ambaye amekimbilia huko baada ya mgawanyo mpya wa majimbo uliotokana na kuligawa jimbo la Ukonga na kutoa majimbo mawili – Ukonga na Segerea – anakabiliwa na wanachama 11.

Hata hivyo, ni Glorious Luoga, mwanasheria wa chama hicho, anayetajwa kunyima usingizi Mahanga.

Katika baadhi ya maeneo, ambako mikutano ya kunadi wagombea imefanyika, Mahanga amekumbana na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wenzake.

Baadhi yao wamemtuhumu hadharani, kwamba ameshiriki “kuangamiza maendeleo” ya Ukonga.

Wengine wanasema, “Mahanga ameshindwa kusimamia miundombinu hasa ya maji na barabaara katika maeneo ya Tabata, Vingunguti, Kiwalani na Segerea. Hata hivyo, lolote linaweza kutokea.

Mbunge wa Ilala, Azan Zungu anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wanachama watatu. Bado anaweza kushinda.

Bali, Zungu hapaswi kupuuza kampeni za Jafari ole Koinele, aliyejitosa kuangamiza Zungu kisiasa, hasa katika kipindi hiki cha lala salama.

Katika jimbo la Ubungo, mchuano mkali upo kwa wagombea watatu, kati ya 13 waliojitokeza.

Lakini washindani wakubwa wanatajwa kuwa ni Waziri wa Maliasili la Utalii, Shamsa Mwangunga, mwanasiasa machachari, Nape Nnauye na mkuu wa wilaya ya Bukombe, Hawa Ngh’umbi.

Tayari Nape amenukuliwa akilalamikia kile alichoita, “hujuma” kutoka kwa viongozi wake. Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na viongozi wake.

Mkoani Iringa, kinyang’anyiro kipo katika majimbo tisa kati ya 11 mkoani humo. Katika baadhi ya majimbo, kinyang’anyiro kimebeba hata wasiochagulika.

Kwa mfano, katika jimbo la Iringa Mjini, kati ya wagombea 12 waliojitosa, ni wagombea wanne tu, ndiyo wanaoweza kuchagulika.

Wanaoweza kuchagulika ni mbunge wa sasa, Monica Mbega, Fredric Mwakalebela, Jesca Msambatavango na Thomas Kimata.

Katika jimbo la Kalenga, kati ya wagombea 14 waliojitosa, wagombea wanne ndiyo wanaochuana. Mbunge wa sasa, Steven Galinoma hakugombea nafasi hiyo.

Wagombea wanaopewa nafasi ya kushinda, ni Mhandisi Gabriel Karinga, mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abas Kandoro, William Mgimwa na Hafsa Mtasio.

Huko Njombe Magharibi, zaidi ya wanachama tisa wamechukua fomu. Hata hivyo, wanaoonekana kuwa washindani ni mbunge wa sasa, Yono Kevella, Thomas Nyimbo, Daniford Mpumilwa na Isaya Mengela.

Katika jimbo la Mufindi Kusini, kuna wagombea 11. Kati ya hao, ni Spian Tweve, Mika Mlonganile, Medrand Kigola na mbunge wa sasa, Benito Malangalila, wanaotajwa kuwa washindani.

Kwa upande wa jimbo la Njombe Kaskazini, ni Mwenyekiti wa viwanda vidogovidogo, Enock Ndondole na mbunge wa sasa, Jackson Makweta, ambao wanaonekana kukabana koo.

Mchuano mkubwa upo katika jimbo la Kilolo ambako Profesa Peter Msolla anakabiliana na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Venance Mwamoto. Ni miujuza tu, inayoweza kumuibua tena Profesa Msolla.

Hali kama hiyo, inatajwa kuwapo pia katika jimbo la Ludewa. Mbunge wa sasa, Profesa Raphel Mwaliosi anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Deo Haule.

Hata hivyo, Profesa Mwaliosi anaweza kuibuka mshindi.

Kinyang’anyiro katika majimbo ya Makete, Ismani na Njombe Kusini, kinaonekana kukosa mvuto kutokana na udhaifu wa baadhi ya wagombea.

Taarifa zinasema, William Lukuvi (Ismani), Dk. Binlith Mahenge (Makete) na Anne Makinda (Njombe Kusini), wanaweza kupenya.

Mkoani Mbeya, kinyang’anyiro kikali kipo katika majimbo ya Mbeya Mjini, Chunya, Kyela, Rugwe Magharibi, Rugwe Mashariki na Mbozi.

Katika jimbo la Rugwe Mashariki, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya anakabiliana na Stephen Mwakajumilo.

Hata hivyo, Profesa Mwandosya anapewa nafasi kubwa ya kushinda. Mwandosya anajivunia utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni mwake.

Katika kipindi chake cha miaka 10 ya ubunge, wananchi wanasema Rungwe Mashariki imebadilika. Umeme umefika sehemu nyingi, maji yanatiririka katika vijiji vingi na vituo vipya vya afya vimejengwa na vya zamani kukarabatiwa.

Naye, mbunge wa Rungwe, Profesa David Mwakyusa anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Fank Magoba ambaye tayari amemaliza vyama kwa kuhamahama na mwanachama kijana, Richard Kasesela.

Katika jimbo la Chunya, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Njelu Kasaka anahaha kutaka kurejea tena bungeni.

Kasaka aliyevuliwa ubunge na mbunge wa sasa, Victor Mwambalaswa, baada ya kushindwa katika kura za maoni, alikikimbia chama chake na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF). Alirejea CCM miaka miwili baadaye.

Hatua yake ya kuondoka katika chama chake na kujiunga na upinzani, ndiko kunakompa mtaji wa kisiasa Mwambalaswa, kwa hoja kwamba Kasaka ni “mwanaCCM maslahi.”

Katika jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Elius Mwakalinga, Elias Mwanjala, Rhoda Mwamunyange na George Mwakalinga.

Hata hivyo, anayeonekana kutaka kumtoa macho Dk. Mwakyembe ni Mwanjala. Kimsingi katika jimbo hilo, lolote laweza kutokea.

Kwa upande wa Mbeya Mjini, ushindani mkubwa upo kati ya mbunge wa sasa, Benson Mpesya na mbunge wa kuteuliwa, Thomas Mwang’onda.

Mtaji mkubwa anaojivunia Mwang’onda ni kule kuungwa mkono na vijana na baadhi ya wazee wanaodaiwa kuheshimu mchango wa baba yake, Apson Mwangonda ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa usalama wa taifa.

Hata hivyo, kati ya wagombea hao wawili, kila mmoja aweza kushinda.

Mkoani Tabora, mvutano mkubwa upo katika majimbo ya Igunga, Urambo Mashariki, Nzega na Tabora Mjini.

Jimboni Urambo Mashariki, mbunge wa jimbo hilo, Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa meneja wa kampuni ya simu mkoa wa Mwanza, Ali Masanywa.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, “lolote linaweza kutokea.” Tayari Spika Sitta amelalamikia hujuma anayosema inafanywa na wapinzani wake wa kisiasa.

Mbunge Rostam Aziz ambaye katika chaguzi mbili zilizopita alipita bila kupingwa, sasa anakabiliwa na wagombea wanane jimboni Igunga, ingawa anayepewa nafasi ya kutoa ushindani ni Dk. Peter Kafumu.

Mkaoni Arusha, kampeni kubwa ipo katika majimbo ya Arusha Mjini, Monduli na Arumeru Magharibi.

Katika jimbo la Monduli, Edward Lowassa, amekabwa koo na mganga mkuu wa Hospitali wa mkoa wa Arusha, Dk. Salash Toure.

Tayari Toure amelalamika kuhujumiwa. Katika malalamiko yake anasema, “…napata kila aina ya vikwazo kutokana na hatua yangu ya kutumia haki yangu ya kikatiba ya kugombea.”

Huko Arusha Mjini, mbunge Felex Mrema anakabiliwa na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Batilda Buriani.

Batilda anategemea kura kutoka kwa makundi ya wanawake, huku Mrema akitegemea kuvuna kutoka kwa wanachama wenye msimamo wa wastani.

Hata hivyo, yeyote kati ya wagombea hawa anaweza kushinda, ingawa bado Mrema anaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi.

Mkoani Dodoma, kinyang’anyiro kimechukua sura mpya. Wanachama watano ambao awali walikuwa wanatuhumiwa kutumika kumchafua Alhaji Adam Kimbisa, wamekamatwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).

Wanachama hao wanatuhumiwa kugawa fedha kwa wapigakura za maoni kwa lengo la kushawishi kumchagua Elia Ndejembi, mtoto wa mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoa wa Dodoma, Pascal Ndejembi.

Mkoani Kilimanjaro, mshikemshike upo katika jimbo la Mwanga, kati ya Profesa Jumanne Maghembe na Joseph Thadayo. Yeyote kati ya hao aweza kuibuka na ushindi.

Mshikemshike upo pia katika jimbo la Moshi Vijijini. Mbunge wa sasa, Dk. Cyril Chami anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Ansi Mmasi.

Miongoni mwa wagombea hawa wawili yeyote anaweza kushinda, ingawa Dk. Chami anapewa nafasi kubwa.

Katika hatua hii ya kinyang’anyiro cha ubunge, ni wanachama wanne tu waliopita bila kupigwa mpaka sasa.

Hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri na mbunge wa Msalala Ezekiel Maige.

Vyovyote itakavyokuwa, mchakato huu, kwa jinsi unavyokwenda, utaishia kukiacha chama hiki katika makovu makubwa ya lawama na kununiana na huenda hata kukihama wakikimbilia upinzani.

Hii ni kwa sababu, katika maeneo mengi, mchakato unadaiwa kuendeshwa kwa rushwa, fitina na upendeleo.

Hata pale ambapo wagombea wamewasilisha malalamiko yao, mathalani katika jimbo la Bunda, mkoani Mara ambako wagombea wamemlalamikia Steven Wasira kuanzisha makundi ya vijana kutishia maisha wagombea wenzake, hakuna dalili za madai hayo kufanyiwa kazi.

Aidha, hata hicho kinachoitwa mkakati wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), katika maeneo mengi, ukiacha Dodoma, inadaiwa kinalenga baadhi ya watu ambao hawako karibu na viongozi wakuu.

Kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge na udiwani kupitia CCM zimepangwa kufanyika nchini kote, tarehe 1 Agosti mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: