Pinda aetembea na kiziba mdomo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda wiki mbili zilizopita alilazimika kuzozana na vyombo vya habari hasa gazeti moja lililochora katuni inayomhusu.

Katika katuni hiyo, M7 kama anavyoandikwa badala ya Museveni, alichorwa akikata keki kusherehekea miaka 25 ya utawala wake.

Keki aliyokuwa anakata ni ramani ya Uganda na yeye alionekana kukata katikati. Kwa tafsiri yake alidai kuwa gazeti lilikusudia kuonyesha anaikatakata vipande nchi hiyo hivyo akaamuru watiwe ndani.

Hata hivyo, mwanasheria mkuu alipuuza tafsiri hiyo akisema ni katuni ya kawaida na hasa ikichukuliwa maanani kwamba yeye amekaa madarakani kwa miaka 25 sasa.

Angalau mwanasheria mkuu amekuwa na busara kuona ukweli, hapa Tanzania watawala wote hawataki kuona ukweli ndiyo maana kazi kubwa inayofanyika siyo wao kuheshimu ukweli kwa vile uko wazi ila kuziba midomo wale wanaoeneza ukweli.

Mathalani, katika siku ya kwanza ya kile kilichoitwa semina elekezi kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri mkuu, Mizengo Pinda inadaiwa aliwapiga marufuku wabunge kulumbana na serikali.

Kwa maneno mengine, Pinda alitumwa kuwataka wabunge wa CCM waheshimu maamuzi yanayofanywa na serikali yao bila kuhoji uhalali. Waziri mkuu anaona mambo yote yanayoamuliwa na serikali ni halali na yamejaa tija na maslahi kwa wananchi.

Kauli ya Pinda ni kielelezo kwamba serikali ya CCM bado haijajitambua inavyowaudhi wananchi wake na kwamba wabunge hao anaowazuia ni wawakilishi wa wananchi wanaopinga ufisadi.

Badala ya kumtuma Pinda awaulize wabunge hao kwa nini wameinunia serikali na kuikosoa kwa nguvu hadharani, yeye amekwenda na gundi aina ya supagluu kuziba midomo wasikosoe.

Wabunge wa CCM hawatakiwi kuisema serikali kwa vile kwa kufanya hivyo watakuwa wanaimong’nyoa serikali.

Bila shaka Pinda anaihami serikali isikosolewe kuhusu ushiriki wake katika ufisadi kupitia EPA, Kiwira, Meremata, Tangold na kandarasi za barabara.

Tazama wakati John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, mwaka 2005, kujenga kilomita moja ya barabara ya lami ilikuwa kati ya Sh 500milioni na Sh.800milioni.

Magufuli alionekana anatia kiwingu akapelekwa haraka kuhesabu samaki, aliporudishwa safari hii gharama ya ujenzi wa kilomita moja ya barabara ya lami imeshafika kati ya Sh 1.4bilioni na Sh. 1.8bilioni.

Magufuli anadai viwango hivyo ni vikubwa kuliko nchi za Afrika Mashariki na ni vikubwa kuliko hata baadhi ya nchi zilizoendelea.

Nani ametufikisha hapo? Serikali ilidai imeshindwa kuendesha Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikawaleta wahindi wa Rites, lakini serikali ndiyo inalipa Sh. 1.1bilioni za mishahara kati ya Sh. 1.7bilioni zinzohitajika. Nani ametufikisha hapa?
Haya ndiyo madudu ambayo Pinda hataki wabunge wa CCM waseme maana kuisema serikali itakuwa sawa na kulumbana nayo.

Mabadiliko

Moja ya vigezo vya ziada alivyoongeza Rais Benjamin Mkapa wakati wa kuteua jina la Jakaya Kikwete kuwania urais mwaka 2005 ni kwamba ilikuwa ujana wake.

Mkapa alisema wapigakura wengi mwaka ule walikuwa vijana, hivyo kwa kutozingatia kigezo hicho, CCM ilikuwa hatarini dhidi ya Chadema iliyokuwa inakuja juu huku mgombea wake alikuwa kijana Freeman Mbowe.

Ni ukweli usiopingika kwamba vijana ndio wamebadili upepo wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2010. Upepo huo wa mabadiliko unaendelea.

Mtu yeyote aliyetazama kongamano la uzinduzi wa mjadala kuhusu katiba mpya lililofanyika kwenye ukumbi wa Nkuruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), atakuwa alipata jibu moja kuu kwamba vijana wanataka mabadiliko.

Vilevile mtu aliyewasikia au kusoma kauli ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), atakuwa alipata jibu moja kuu vijana wanataka mabadiliko. Pinda atafanikiwa kuwasiliba supagluu wote hao wasione ufisadi wa serikali yake?

0789 383 979
0
Your rating: None Average: 3.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: