Pinda ahalalisha uhalifu mkoani Mara


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, wiki iliyopita alifanya ziara mkoani Mara ambako pamoja na mambo mengine aliagiza na kuelekeza kwamba wakazi wa mkoa huo unaogubikwa na vurugu na mapigano ya mara kwa mara watumie mabaraza ya jadi maarufu kama iritongo kutatua migogoro yao.

Pinda ambaye ni miongoni mwa viongozi walisoma mkoani humo katika shule maarufu ya Musoma Sekondari enzi hizo ikiitwa Musoma Alliance Secondary School (MASS) alitoa pendekezo hilo ikiwa moja ya njia za serikali inayohangaika kutafuta dawa ya kutibu mapigano ya wakazi wa Mara.

Kwa vile alisoma Mara, Pinda anauelewa vema mkoa wa Mara na wakazi wake kuanzia Wangoreme, Waikoma, Wanata, Waisenye, Waikizu, Wakenye, Wanyamongo, Wairegi, Watimbaru, Wanyabasi, Wakira, Walenchoka, Wanchari, Wasweta, Wahunyaga, Wasimbiti, Wazanaki, Wakabwa, Wakwaya, Wakiroba, Wategi, Wakiseru, Wasuba, Warieri na hata Wakine.

Pamoja na nia nzuri ya kutaka kutatua migogoro katika mkoa huo, Pinda aliyewahi kuiongoza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, anapaswa kuwa ameyatafakari kwa kina maelekezo na maagizo yake. Baadhi ya mbinu au njia za utatuzi zilizokuwa zinatumiwa na mabaraza hayo enzi hiyo, zilikuwa zinasababisha matatizo makubwa katika jamii.

Maagizo yake yanaweza kuchochea uhalifu, kusababisha ongezeko kubwa kwa uhasama baina ya koo na koo na kuasababisha familia kusambaratika badala ya kuondoa kero ya migogoro kama anavyotaka Pinda. Nitatoa maelezo kwa kirefu.

Tunaikataa njia hii ya kutatua migogoro kwa sababu adhabu zinazotolewa huwa hazina mantiki na ni za kipuuzi. Adhabu hizo za kimila ni pamoja na kulaani mtu, kumroga na kumpiga faini ya kulipa ng’ombe.

Faini hiyo, wakati mwingine  huishia kwa wazee kugawana na nyingine huwapa polisi waliokwenda kukamata ng’ombe hao. Ndiyo maana polisi wengi hufurahi au hupendelea kuhamishiwa Mara wanakopata ng’ombe wa bure.

Kwa kumsaidia Waziri Mkuu Pinda, wakazi wa Mara wana njia nyingi za kutatua migogoro bila kuhusisha serikali. Njia hizo zilikuwa nzuri wakati hakuna mahakama, enzi hizo za kabla ya wakoloni na hata wakati wa kikoloni. Njia hizo zikitumika sasa sambamba na mahakama hazileti mantiki yoyote.

Mfano ni mabaraza ya wazee maarufu kama abagaka baekimila au abagaka baenchama au kwa lugha rahisi wazee wa mila. Wazee hawa hukutana na kufanya mashauri yanayopelekwa kwao na kuyatolea uamuzi lakini adhabu zao huwa zinazua utata mkubwa kwa vile siyo lazima mwenye makosa alipe faini bali hata ndugu wa karibu hulipa faini hiyo.

Inapotokea mhalifu ameadhibiwa kulipa faini ya ng’ombe watatu wakati mhalifu mwenyewe hana hata kuku, basi ng’ombe hao “huronwa” yaani huporwa kutoka kwa ndugu wa kuzaliwa na mhalifu huyo.

Kama mhalifu aliyepigwa faini hana ndugu wa baba mmoja na mama mmoja basi hukimbilia kwa ndugu yake kwa baba mkubwa na ikiwa naye hana ng’ombe watatu watakwenda kwa ndugu yake kwa baba mdogo. Ikitokea hao wote hawana mali basi huandamwa ndugu yeyote wa mhalifu katika ukoo wao kwa upande wa baba.

Kwa mtindo huu, mhalifu mwenye ndugu wenye mali huendelea kutekeleza vitendo vya kihalifu kwa kuwa si yeye anayeadhibiwa au kulipa faini bali adhabu huwa kwa ndugu wa karibu. Ikitokea kuwa hawapo basi ukoo mzima huwajibika kulipa deni lililosababishwa na mwanajamii mwenzao.

Matokeo ya aina hii ya kutatua migogoro ni kwamba wapo watu wanafilisika kwa sababu ya matendo ya kihalifu ya ndugu zao. Sasa swali, je Pinda ambaye kitaaluma ni mwanasheria, yuko tayari kuona akina Nyaronyo Kicheere wanaoishi Dar es Salaam wakiadhibiwa kwa makosa yanayofanywa na akina Maheri Kicheere wanaoishi Nyamongo? Yaani Pinda anataka Athumani kuadhibiwa kwa kosa la Abdalla?

Kwa mtindo huu, wezi wataendelea kuiba kwa sababu hawaadhibiwi binafsi na pia husababisha koo zilizoibiwa kugombana. Familia zinazoronwa ng’ombe kwa sababu ya ndugu yao mwizi zitasambaratika. Je, haya ndiyo anayoyataka Pinda?

Nija nyingine ya kutatua migogoro ni ya kutumia wanajamii wote, kwa maana ya iritongo. Njia hii nayo siyo sahihi kwa sasa kutokana na namna ushahidi unavyotolewa. Hii ndiyo njia potofu iliyotumika miaka ya 1980 kuhamisha watu kwenda Mtwara, Lindi na Ruvuma eti kwa makosa ya kuiba ng’ombe ambayo hayakuthibitishwa katika mahakama yoyote ile nchini.

Kinachofanyika kwenye iritongo ni kuita watu wote, yeyote atakayepata nafasi kuhudhuria na wote kuhojiwa kwa pamoja, je, Nyaronyo Mwita Kicheere ni mwizi? Waliohudhuria kwenye hadhara hiyo wakinyamaza labda kwa sababu hawamfahamu Nyaronyo basi inachukuliwa kuwa yeye ni mwizi.

Kwa hiyo, watu wakikunyamazia kwa sababu ya tuhuma nyingine kama vile ugoni, kugombea shamba au umeshinda kwenye mieleka na kucheza ngoma ya iritungu basi wewe unachukuliwa kuwa ni mwizi.

Je, Waziri Mkuu Pinda anataka mkoa mzima uache kufuata taratibu za leo za kutoa ushahidi mahakamani badala yake wakanyamaziane kwenye mikutano? Yaani leo hii, enzi hii ya sayansi na teknolojia, Wakurya  waendelee kutawaliwa kama ilivyokuwa enzi za ujima wakati wengine wanafuata mtindo wa kupelekana mahakamani? Pinda anatakiwa kuomba radhi. 
Iritongo na wazee wa kimila huweza kulaani mtu au kumroga kama hatatekeleza wanayotaka. Haya ndiyo mabaraza na taasisi pekee zinazoruhusiwa kwa mila ya Wakurya kuroga wao wanaita kuteema. Wanaweza kukuteemela ukoma, ndoli (ugonjwa wa kuanguka), kichaa au ugonjwa wowote mbaya.

Pia wazee hawa wanaweza kukuulia familia yako na hata ukoo mzima kama hukutekeleza wanavyotaka. Yaani watoto wako, mkeo na ndugu zako wa karibu wanauawa kwa kurogwa. Sasa Waziri Mkuu Pinda anataka mkoani Mara aendelee kurogana kama njia ya kutatua migogoro? Au waziri mkuu hakuelewa anaagiza nini?

Kuwaagiza au kuwaelekeza au kusema tumieni wazee wa jadi au tumieni iritongo hakuna tofauti na kuwaagiza au kuwaelekeza au kusema mkarogane na mpigeni faini watu wasiohusika na makosa alimradi tu wanahusiana na wahalifu! Haki ipo wapi mwanasheria wetu Pinda? Usawa upo wapi hapa mwenzetu Pinda?

Na kwa sababu ya urahisi wa kunyang’anyana mali njia hii hupendelewa sana na polisi, mgambo, sungusungu, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa wilaya. Pia wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata na vijiji hupendelea sana njia hii ya kutumia wazee na iritongo kwa sababu ya urahisi wa kupora mali ya watu eti kwa sababu ndugu yao ni mwizi au anadaiwa.

 Pinda hana haki kuwarejesha Wakurya enzi ya ujima ya kuadhibu ukoo kwa makosa ya mtu mmoja. Mtu anatoka baa akifika nyumbani anaambiwa ngombe kachukuliwa kwa kosa la kaka yako, kesho kosa la mdogo wako na kesho kutwa kosa la baba mdogo kutohudhuria mkutano! Huu ni uhuni na tunaukataa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: