Pinda akimbia MwanaHALISI


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda

SERIKALI imezuia mwandishi wa MwanaHALISI kuhudhuria mkutano wa vyombo vya habari ulioitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hiyo ilikuwa Ijumaa, saa 4:45 asubuhi katika Ofisi ya waziri mkuu iliyoko Magogoni, Dar es Salaam.

Irene Kakiziba, mwandishi wa habari msaidizi wa waziri mkuu, alimweleza Saed Kubenea, “Hatukukualika.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na mwandishi wa waziri mkuu, Said Nguba siku moja kabla Pinda kukutana na wahariri, “Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa waziri mkuu wa kukutana na wahariri.”

Akiwa ameandamana na mwandishi wa Tanzania Daima, Martin Malela na mhariri wa Nipashe, Deodatus Muchunguzi, Kubenea alielezwa na maofisa wa usalama wa taifa wa ikulu waliokuwa katika lango la kuingilia kuwa jina lake halimo katika orodha ya waandishi wanaotakiwa katika mkutano huo.

Hata hivyo, maofisa wa usalama wa ikulu walimueleza Kubenea, “Kwa kuwa “tunakufahamu, tunakuruhusu kuingia ndani ili usubiri maelekezo zaidi kutoka kwa Irene.”

Akiwa kwenye lango la mwisho la kuingia ndani, ambako kulikuwa na wageni mbalimbali na waandishi wa habari waliokwenda kuhudhuria mkutano huo, Irene alimweleza Kubenea, “Nimepokea maelekezo kuwa huruhusiwi kuhudhuria mkutano huu.”

Kubenea alipotaka kuelezwa sababu za kuzuiwa kuhudhuria mkutano huo, Irene alisema, “MwanaHALISI hamjaalikwa. Hivyo, siwezi kukuingiza…”

Alipotakiwa kueleza sababu za kubagua MwanaHALISI, huku magazeti mengine yakiruhusiwa kuhudhuria mkutano huo, Irene alisema, “Hayo ndiyo maelekezo niliyopewa. Mimi sina njia nyingine ya kukusaidia.”

Alimtaka mwandishi kuwasiliana na Nguba ambaye kwa mujibu wa Irene, yuko mkoani Arusha kikazi. “Hilo ndilo ninaloweza kukueleza. Vinginevyo, uwasiliane na Nguba ambaye yuko safarini Arusha ili kupata kibali cha kuingia.”

Kubenea alipong’ang’ania kuwa Nguba “hakuondoka na ofisi mabegani,” na kwamba hakukuwa na sababu ya kuwasiliana naye, Irene akionyesha kuudhika alisema, “Haya ndiyo maelekezo yaliyopo.”

Irene alisema tayari ameongea na mwandishi wa gazeti hili, Ezekiel Kamwaga dakika chache zilizopita na kumwambia kuwa “gazeti lenu halikualikwa.”

Mabishano kati ya Irene na Kubenea yalifanyika mbele ya wahariri wa vyombo vya habari, maofisa wa habari kutoka Idara ya Habari (MAELEZO), wageni mbalimbali na maofisa usalama wa taifa.

Hata pale mwandishi alipomweleza ofisa huyo wa habari wa ikulu, kwamba “hapo ni mahali pa kupita,” – akimaanisha ofisi ya waziri mkuu – bado Irene aliendelea kusisitiza, “Siwezi kubadilisha msimamo wangu.”

Kushindwa kwa MwanaHALISI kuingia katika mkutano wa waziri mkuu, kumelinyima gazeti fursa ya kupata majibu ya maswali kadhaa.

MwanaHALISI liliwahi kuhudhuria mikutano hii ya kawaida ya Pinda mara mbili huko nyuma. 

Yalikuwa maoni ya wahariri wengi, pale walipopata taarifa za mkutano wa Pinda, kwamba waziri mkuu atazungumzia suala la Katiba mpya ambalo limekuwa vinywani mwa wananchi wengi.

MwanaHALISI, kwa wiki kadhaa sasa, limekuwa likiandika kwa “uzito wa aina yake” makala na maoni ya wananchi wengi wanaotaka kuona nchi inapata Katiba mpya.

Mkutano na waziri mkuu ulikuwa fursa nyingine adhimu kwa gazeti hili kuuliza maswali juu ya katiba mpya na hata hatma ya waziri aliyeonyesha kutozingatia matakwa ya sasa ya katiba.

Mwandishi wa habari hii alifanikiwa kuona orodha ya maswali ya MwanaHALISI ambayo Kubenea alikuwa akiipeperusha huku akisema, “…tulikuwa na maswali yetu haya; basi angalau angekubali tuwasilishe maswali yetu.”

Kwa mujibu wa Kubenea, kutopatikana kwa fursa ya kukutana na waziri mkuu kumesababisha gazeti lake kutopata majibu kwa maswali yaliyokuwa yameandaliwa. Kwa mfano, gazeti lilitaka:

Kwanza, kupata maelezo ya waziri mkuu Pinda juu ya madai yaliyopo mitaani kwamba yeye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya usafirishaji abiria ya Sumri. Inadaiwa kuwa hisa za Pinda zinamilikiwa kupitia kampuni ya One Move Transport.

Pili, huko nyuma Pinda aliwahi kunukuliwa akisema, “Hakuna wa kuiogopa Kagoda.” Baadaye akanukuliwa akisema, “…Kagoda ngumu.” Gazeti likitaka kujua kwa nini serikali imeshindwa Kagoda.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna watu walichukua fedha Benki Kuu ya Taifa (BoT); kuna walioweka fedha hizo CRDB Benki; kuna waliosambaza fedha hizo  katika matawi ya CRDB jijini Dar es Salaam na kuna waliokuwa wakichukua fedha hizo.

MwanaHALISI lilitaka kupata maelezo kutoka kwa waziri mkuu: Kuna nini hapa? Je, kwa nini serikali imeshikwa na kigugumizi kwa Kagoda?

Tatu, gazeti lilikuwa linataka kupata msimamo wa serikali kuhusu katiba mpya. Kwamba kwa nini serikali, badala ya kutaka kufanya marekebisho kwa katiba iliyopo, isimalize kabisa tatizo hilo kwa kuandika katiba mpya?

Pamoja na maswali hayo yaliyokuwa yameandaliwa, kulikuwa na uwezekana wa kupatikana maswali ya nyongeza.

“Hii ni hujuma ya wazi kabisa,” anasema Kubenea. “Ni kuhujumu gazeti kwa njia ya kulikosesha habari. Lakini pia ni kuhujumu wananchi kwa njia ya kuwakosesha habari zinazohusu serikali na watawala.”

Kwa mujibu wa taarifa, vyombo vya habari ambayo Irene anadai vilialikwa ni pamoja na gazeti la serikali Daily News, Habari Leo, TBC, Radio Tanzania, Uhuru, Mtanzania, Rai, Hoja, Mwananchi, Raia Mwema, Tanzania Daima, ITV, Majira, Jambo Leo, Star Televisheni, Nipashe na Mlimani Televisheni.

Gazeti la MwanaHALISI liliwahi kufungiwa kwa siku 90  miaka miwili na nusu iliyopita na aliyekuwa waziri wa habari, George Mkuchika kwa madai ya uchochezi ambayo serikali, hata hivyo, haikuyathibitisha.

Gazeti hili limekuwa likinyimwa pia matangazo na baadhi ya ofisi za serikali na makampuni ambayo ni maswahiba wa ama serikali au Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua ya kuzuia MwanaHALISI kushiriki mkutano wa waziri mkuu na waandishi wa habari, ni hatua nyingine ya serikali ya kudhibiti vyombo vya habari ambavyo inaona siyo “rafiki wake.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: