Pinda ameamua "kufa" ili waovu wapone


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version

MIZENGO Pinda aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, bila shaka, ili asaidie kuondoa wingu la tuhuma za ufisadi linaloifunika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Bali Ijumaa iliyopita, nadhani kwa bahati mbaya, alijikuta akijawa na kigugumizi juu ya kampuni ya Meremeta na Tangold ambazo zimechotewa kiasi kikubwa cha fedha kutoka serikali, huku zikishindwa kuonyesha faida zozote kwa umma.

Baada ya kubanwa na wabunge, hasa Dk. Willibrod Slaa (Chadema) na John Cheyo (UDP) kutaja wamiliki wa Meremeta, Pinda aliharakisha kusema kuwa kampuni hiyo ilianzishwa na serikali kwa ajili ya kusaidia shughuli za ulinzi na usalama wa nchi.

Pinda alisema wazi kuwa yuko radhi kusulubiwa na wabunge kuliko kusema kwa undani shughuli za Meremeta, mbali ya kusema tu kuwa ilikuwa ikichimba dhahabu na kwamba ni kwa ajili ya kusaidia shughuli za kiusalama za nchi.

Kwa hitimisho la Ijumaa juu ya Meremeta, hakuna ubishi kwamba serikali ya awamu ya nne imejiruhusu kuwa tena kikaangoni kwa mwaka mwingine mzima.

Ni mwaka mwingine kwa sababu kwa kauli za baadhi ya wabunge na kwa taarifa zilizoko mitaani, Merermeta ni kashafa nzito na chafu pengine kuliko hata EPA, Richmond na Buzwagi kwa pamoja.

Hadi sasa, ingawa Pinda anataka wabunge wasadiki kuwa Meremeta ni kampuni ya kuchimba dhahabu iliyokuwa inamilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kuna taarifa za ndani kwamba kampuni hii imejihusisha na mambo ya kujichotea fedha za umma kwa mambo ambayo hayawekwi wazi.

Mathalani, kuna taarifa kwamba kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza sheria na mikataba ya madini nchini, iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani, imegundua kwamba mkataba mzima wa Meremeta uligubikwa na utata mkubwa.

Miongoni mwa mambo ambayo Pinda atakuja kujutia na kusaga meno kutokana na kauli yake, ni habari kwamba ndani ya Meremeta shughuli za kiutendaji na uwajibikaji zilikuwa chini ya wageni. Wageni baki, wasio raia wa Tanzania, hawa ndio walikuwa wakiendesha Meremeta.

Katika hali kama hii, iweje mambo ya usalama wa nchi, tena ya kijeshi, yaachwe mikononi mwa watu ambao kwanza, si raia na pili, si wanajeshi ambao wamekula kiapo cha kulinda siri na usalama wa nchi.

Meremeta na "nduguye" Tangold hadi, mradi huo unasitishwa walikwisha kuchotewa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sh. 158 bilioni. Hizi ni fedha zaidi ya zilizofujwa na mafisadi wa EPA ambazo ni Sh.133 bilioni.

Kuna fedha nyingine zaidi ya Sh.10 bilioni ambazo zimechukuliwa kutoka BoT kwa ajili ya kuendesha shughuli za Meremeta. Kwa kifupi, fedha ambazo zimechotwa BoT chini ya kivuli cha Meremeta ni kiwango kikubwa na cha kutisha.

Hapa Pinda amejenga ajenda mpya ya kuandamwa na umma kuhusu fedha za Meremeta. Watu wanashindwa kujua sababu za serikali kupitia kwa Pinda inajaribu kufunika kashfa ya Meremeta kwa kisingizio cha usalama wa taifa wakati zipo taarifa za wazi kabisa za watu nje ya mfumo wa serikali waliolipwa fedha hizo tena kwa mabilioni.

Kuna taarifa kwamba kuna chama cha siasa kimenufaika na fedha hizo; kuna taarifa na mkanganyo wa hadhi za wakurugenzi wa Tangold; kuna mkanganyo wa manufaa ya umma yalivyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa Meremeta ikilinganishwa na kiasi cha fedha zilizochotwa ambazo ni jasho la walipa kodi wa nchi hii.

Sasa ni wazi kwamba ufisadi unaitafuna nchi lakini wabunge wa CCM waliokuwa wamefyata mkia siku nyingi, wakiogopa ubabe wa utawala wa Mkapa, wameamua kuunga mkono juhudi za kuibana serikali kusema ukweli.

Mkutano wa Bunge unaoendelea umezidi kuthibitisha kuchoka kwa wabunge wa CCM kuvumilia uchafu wa serikali yao. Jaribu kutafakari kauli za watu kama akina Aloyce Kimaro; Anne Kilango Malecela na wengineo. Zina maana kwamba kuna mpasuko mkubwa kati ya serikali na wabunge wa chama chake.

Wapo wenye ujasiri wa kuzungumza hadharani. Hawa ni wachache. Wapo wanaolalamikia chini kwa chini. Hawa ni wengi. Kundi hili la wengi wanajisikia kuburudika moyoni pale akina Dk. Slaa na Cheyo wanapoelekeza mishale yao kwa serikali na kutaka uwajibika juu ya mbinu chafu za kuifilisi nchi chini ya kivuli cha 'usalama wa taifa.'

Kwa jinsi ileile ya mwaka wa fedha wa 2007/08 ambao serikali na wabunge wake walijikuta wamelazimishwa kujielekeza kwenye ajenda ya kupambana kujibu tuhuma za ufisadi, mwaka wa fedha wa 2008/09 hauonyeshi kwamba serikali itajitoa kwenye kitanzi hicho.

Serikali haijiokoi kwa sababu uwongo daima hausimami. Kwa mwaka mzima wa fedha wa 2007/08 serikali ilishindwa kujitoa kwenye kashfa ya Buzwagi, Richmond na EPA. Sasa inaaza mwaka mpya wa fedha na kiporo cha kashfa hiyo, lakini safari hii ikiwa imebebeshwa bango jingine la Meremeta na Tangold.

Ni katika kutafakari hali hii naanza kupata hisia kwamba kiti cha uwaziri mkuu kwa Pinda kinaweza kuwa cha moto kuliko alivyotarajia mwenyewe au hata umma ulivyokuwa umedhania.

Pinda anaingia kuficha mambo ambayo kwa kweli hayalengi kuijenga serikali; hayaonyeshi kujenga uwajibikaji na kwa ujumla, ameamua afe yeye ili waovu wapone.

Tunajua kwamba Pinda ni mkristo wa madhehebu ya Katoliki. Tunafahamu anajua kwamba Yesu Kristo alikufa ili wengine wapone; kwa hali hii ameamua kufuata nyayo za Bwana wake ili kuwasaidia waovu serikalini wapone.

Pinda amemua kuwa kondoo wa kafara akidhani kukataa kutaja wahusika wa Meremeta kunaua hoja ya kashfa hiyo. Ukweli ni kwamba Pinda ametoa silaha kwa wapinzani wake, na hakika watazitumia vilivyo kumshughulikia.

Majibu ya Pinda kwamba yuko radhi kusulubiwa na wabunge kuliko kusema yaliyomo ndani ya Meremeta, yanavuta hisia kwamba hata utekelezaji wa azimio la Bunge juu ya Richmond, na hatua dhidi ya mafisadi wa EPA itakuwa ni porojo tupu.

Pinda kaanza na mguu mbaya, safari ya uwaziri mkuu wake itakuwa chungu pengine kuliko ya mtangulizi wake, Edward Lowassa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: