Pinda ameanza kunogewa na madaraka


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

SIKU moja nilikuwa najadiliana na rafiki yangu juu ya mustakabali wa taifa hili hasa tunapowatazama viongozi wa kisiasa. Pamoja na mengi aliyonieleza, kitu kimoja hadi leo ninakikumbuka.

Alisema hivi: “Si rahisi kumjua binadamu hadi umpe vitu viwili; mosi, madaraka au mamlaka na pili, fedha!”

Alifafanua kwa mifano. Alisisitiza kwa kutoa mfano wa Mwalimu Nyerere kwamba katika kizazi cha viongozi wake na kwa aina ya nchi za Afrika zilizokuwa zinapata uhuru, alijipambanua kwa njia ya ajabu sana kuonyesha kwamba kwake madaraka na fedha si vitu vya kumtoa katika misingi ya uongozi; aliongoza, akaishi na kufa kama kiongozi.

Rafiki yangu aliniambia ndiyo maana katika kutafuta viongozi mataifa yaliyopiga hatua yana kazi ya kwenda nyuma zaidi kuchunguza historia ya mtu; je, anabadilika kulingana na mazingira, na je, ana misimamo ya kweli au ni mfuata mkumbo na kujinufaisha kwa mazingira yanavyobadilika?

Katika mambo ambayo katika siku za hivi karibuni yameanza kusumbua fikra zangu ni juu ya uongozi wetu kama taifa; kwamba baada ya kufika hapa tulipo, tutapigaje hatua moja mbele zaidi?

Ukisoma vitabu vya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu utapata mafunzo mengi ya kina juu ya nafasi ya kiongozi hata katika ngazi ya mtaa. Mwalimu alipata kuwaeleza walimu na hata baadaye wanafunzi wa chuo kikuu kwamba wao ni watu waliobahatika katika jamii masikini sana.

Wao ni sawa na mtu mmoja aliyetumwa na wanakijiji ambao walikuwa wanakabiliwa na njaa, lakini wakachanga chakula kilichobaki ili mtu huyo afuate chakuka kingi katika kijiji kingine. Mtu huyo ana wajibu wa kurejea kuwapelekea wenzake chakula; asiporudi atakuwa amewasaliti.

Atakuwa amshindwa kutambua wenzake walivyojitoa mhanga ili yeye si tu aishi, bali akifikie chakula ili aje kuwaokoa na wengine. Asiporudi huyo ni msaliti; ni mlafi, mbinafsi, hafai na wala si mtu wa kutiliwa maanani na jamii yake tena. Huyo ameamua kuwaacha wenzake waangamie.

Mfano huu wa Mwalimu hauna tofauti sana na hadithi ya kwenye Biblia ya safina ya Nuhu na ndege kunguru. Alitumwa toka safinani hakurejea, aliishia kula mizoga hadi leo.

Kwa takribani wiki tatu sasa nchini kumekuwa na mjadala wa moto juu ya posho za wabunge, lakini hizi si za wabunge tu bali hata kwa watumishi wa serikali. Kelele zimepigwa kwamba kinachohujumu taifa hili si kitu kingine isipokuwa matumizi mabaya ya fedha za umma kama hizi posho. Katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/12 kiasi cha Sh. 0.987 trilioni kimetengwa kama posho.

Baadhi ya wabunge wamesema na kulalamika kwamba matumizi ya namna hiyo si mazuri kwa taifa na kwa uhakika ni hatari kwa maendeleo na ustawi wa taifa hili, hasa wananchi walalahoi wanaoishi kwa kipato cha chini ya Sh. 1,500 kwa siku.

Miongoni mwa changamoto za taifa hili ni jinsi ya kufuta kundi la watu wanaoishi kwa pato hilo. Hii ni kazi nzito na ngumu. Mipango na mikakati mbalimbali ambayo imeanzishwa na serikali kusaidia hali hii bado haijazaa matunda tarajiwa.

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limekuwa katika malumbano na serikali juu ya kima cha chini cha mshahara. Tucta wanasema kuwa wakati sasa umefika kwa serikali kulipa walau Sh. 315,000 kwa mwezi kama kima cha chini. Serikali imekalia msimamo wake kwamba haina fedha na haiwezi kulipa fedha hizo, eti ni nyingi mno na ikilipa itafilisika!

Haya yakiendelea kwa muonekano huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiongozi ambaye amejipambanua kuwa ni mtoto wa mkulima akiwa amekataa hata kupewa gari jipya la kazi yake kwa kuwa aliamini hilo alilokuwa nalo bado lilikuwa linafaa; akiwa ndiye mwasisi wa kuacha ununuzi wa mashangingi serikalini, amesema kuwa posho zinazopigiwa kelele kwa ajili ya wabunge ni fedha ndogo tu.

Pinda! Mtoto wa mkulima anaamini kwamba wabunge eti wanalipwa fedha kidogo za posho na kwamba wala haziwatoshi kwa sababu wanagawana na wapiga kura! Nani aliwatuma wabunge kugawa fedha? Huu si ni ule utaratibu wa rushwa? Kwa nini tunaamini kwamba tunaweza kuwasaidia watu wetu kwa kuwagawia Sh. 2,000 au fulana au kofia au ubwabwa? Je, huku ndiko kujenga njia ya kujitegemea na kuendeleza nchi? Pinda atatusaidia huko tuendako.

Kama serikali inagawa posho kwa wabunge ili nao wazigawe kwa wananchi, ni kwa nini basi wasiboreshe mishahara ya watumishi wa serikali ambao ni wengi ili fedha hizo zisambae kwa wananchi wengi zaidi na kwa uhakika badala ya kusubiri fadhila za mbunge mmoja mmoja?

Mwalimu Nyerere alikaa na Benjamin Mkapa kwa miaka na miaka, kama mwandishi wake, kama waziri wake, kama mtu aliyemwamini hadi kumpigia kampeni ili awe rais akiamini Mkapa hakuwa mpenda mali, alikuwa kiongozi mwadilifu.

Lakini baada ya kupata madaraka halisi ya urais, alionyesha rangi yake. Leo hii ukisema uongozi na mali ni ndugu hapo utakuwa unamtaja Mkapa.

Ninachelea kumtazama Pinda katika sura hii, kwamba huenda hatujamjua vizuri, kwamba labda sura ya mtoto wa mkulima anayodai kuwa nayo si yake kweli.

Kukataa kwake shangingi la serikali si sura yake kamili, kwa sababu tunakumbuka Mkapa alipata kukataa kukanyaga zulia jekundu (red carpet) kule Kigoma mara tu alipoanza kipindi chake cha urais. Lakini baadaye ile hali yake ya unyenyekevu ilipotea kadri alivyozoea madaraka na ilifika mahali pa kuwatusi wananchi wake, wapiga kura hadharani!

Ni kwa jinsi hii tunaweza kudhani suala la posho ni dogo sana kama alivyotaka Pinda watu waamini, lakini ni dogo kwa uchumi upi? Kwa wakulima wapi ambao hawawezi hata kununua jembe jipya achilia mbali hizo power tillers zinazopigiwa debe?

Baada ya kauli ya kubeza kelele za kupunguza posho za wabunge na ndani ya serikali kwa ujumla, Pinda bado anajisikia kuwa yeye ni sauti ya mtoto wa mkulima? Mwalimu Nyerere alitufundisha kwa mifano mingi, lakini bado hatujaweza kujua kwa jinsi gani tunatambua yupi atatufaa huko tuendako ili kweli tuwe na kiongozi anayejali na kutambua kodi za wananchi si kitu cha mchezo.

Kwa msimamo wake kuhusu posho za wabunge na serikalini Pinda anaweza kusema kwa dhati kabisa kuwa anarejea kwa wale waliojifunga kibwebwe ili afike hapo alipo? Amewakilisha vipi wakulima anaowalilia?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: