Pinda, amesahau ‘wazazi’ wake


Ephraim Mujungu's picture

Na Ephraim Mujungu - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

NIMEJITOSA mjadala wa posho za wabunge baada ya kuona upotoshaji mkubwa uliofanywa na waziri mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda.

Kwanza, posho zinazojadiliwa sasa, ni zile wanazolipwa wabunge tu. Lakini kuna aina nyingi za ambazo serikali inalipa kama motisha kwa watumishi wake. Kwa mfano, katika ngazi ya mkoa kuna aina tatu za vikao vinavyofanyika. Viwili vina posho na kimoja hakina. Vikao vyenye posho, ni kile cha Bodi ya barabara mkoa na kamati ya ushauri (RCC). Kikao kisichokuwa na posho ni kile cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa.

Mwenyekiti wa vikao vyote hivyo, ni mkuu wa mkoa. Wajumbe ni, wakuu  wa idara mkoani (Regional Scretariat), wakuu wa vyombo vya dola mkoa, wakuu wa wilaya mkoani humo, meya, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri, wabunge na mhandisi wa halmashauri zote zilizopo kwenye mkoa husika.

Kwa kawaida idadi ya wajumbe wa vikao hivi viwili huwa kati ya 200 na 250, kutegemea ukubwa wa mkoa na idadi ya wilaya ndani ya mkoa. Kila mjumbe analipwa kati ya Sh. 150,000 (laki moja na hamsini) na Sh. 175,000 (laki moja na sabini na tano elfu).

Wajumbe kutoka wilayani wanalipwa Sh. 80,000 kama posho ya kulala. Kwa hesabu hiyo, kila mjumbe anarudi kwake akiwa ameweka kibindonni Sh. 230,000 au 255,000 kwa kikao kimoja. Hii ni nje ya fidia ya usafiri kwa afisa anayetumia gari la serikali.

Ukipiga hesabu utaona kuwa kila mjumbe hulipwa sh 660,000 au sh 765,000 kwa mwaka kutoka kwenye bajeti ya barabara.

Kama mkoa una wajumbe 200; mkoa huo hulipa sh 132 milioni kwa mwaka na kama mkoa una 250 hulipa hadi Sh. 153 milioni. Kwa mikoa 21 ya Tanzania Bara, serikali hulipa karibu Sh. 12 bilioni kwa mwaka. Hizi ni fedha nyingi sana. Tayari serikali imeunda mikoa mipya na wilaya mpya, jambo litakaloongeza wanaolipwaji posho.

Lakini ukiacha posho hizo, serikali inalipa viongozi wake kuanzia waziri, mkuu wa mkoa, katibu tawala wilaya, mkuu wa wilaya, makatibu wakuu, wakurungenzi na wakuu kadhaa wa vitengo kwenye wizara na idara za serikali posho za vikao. Viwango vinatofautiana kutokana na ngazi ya kikao.

Kuna posho zingine za kujikimu. Hizi ni zile zinazotolewa kwa ofisa wa serikali mwenye stahiki ya kupewa nyumba, lakini wanakaa kwenye nyumba za kupanga ama ndani ya nyumba zao kwa vile serikali imeshindwa kuwapatia nyumba za kuishi.

Idadi ya maofisa wanaolipwa posho za aina hii imeongezeka baada ya serikali kuuza nyumba zake. Hapa kuna mawili. Kwanza, afisa kuhamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine na pili ni yule aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Hakuna tatizo kwa afisa anayestaafu. Tatizo ni kwa yule anayechukua nafasi ya mwenzake. Analipwa posho ya makazi. Kwa mujibu wa taratibu za serikali, afisa asiyepewa nyumba na muajiri wake huku anastahili, hulipwa posho ya asilimia 30 ya mshahara wake.

Kwa mfano, afisa ambaye mshahara wake ni Sh. 2 milioni kwa mwezi, serikali hulazimika kumlipa Sh. 750,000 (laki saba na elfu hamsini) hadi atakapopewa nyumba na serikali.

Mlolongo wa posho kimsingi ni mkubwa. Kuna posho za kukaimu cheo cha afisa ambaye kwa sababu moja au njingine hayupo ofisini. Afisa anapokaimu kwa zaidi ya siku ishirini lazima alipwe kiasi fulani cha posho. Tangu kumalizika uchaguzi mkuu uliyopita, nafasi nyingi serikalini ziko wazi. Kuna wakuu wengi wa mikoa na wilaya wanakaimu kwenye mikoa na wilaya nyingine baada ya wale waliokuwapo kujitumbukiza katika mbio za ubunge.

Sasa swali tujiulize: Tunawezaje kuondokana na mlolongo huu wa posho? Tuanze na kuangalia sheria ambazo anayejiita “mtoto wa mkulima” anaitumia kuhalalisha malipo hayo.

Suala la posho limefafanuliwa vizuri na sheria ya Kodi ya Mapato sehemu ya 3 (PART III).

Sheria Na. 6 kifungu 13 ya sheria Na 7 ya mwaka 1994 kifungu.8 kinasema, “Kutokana na maelezo ya vifungu (3), (4) na (5) unapokadiria mapato au faida ya mwajiriwa kwa  mwaka malipo yafuatayo lazima yaingizwe: Malipo hayo, ni mshahara, posho ya likizo, malipo mengineyo, posho ya kujikimu…”

Hebu tujiulize posho wanazolipwa wabunge hazimo katika orodha inayotajwa na sheria hii? Posho  anazolipwa waziri mkuu na viongozi wengine serikalini wakiwa kwenye ziara ndani na nje ya nchi hazimo? Hivi ni kweli Pinda hajui sheria hii mpaka afikirie itungwe sheria nyingine?

Waziri mkuu analipwa posho za safari au za malipo ya umeme na simu. Zote hizo hazitozwi kodi.

Je, katika mazingiara haya, nani anaweza kukubaliana na utetezi wa Pinda juu ya posho? Yuko wapi anayeweza kusema “posho si mradi wa wakubwa ndani ya serikali?”

Kama kweli waziri mkuu analipwa posho ya simu, umeme, mavazi akiwa nje ya nchi, kwa nini taifa hili lisieendelea kuwa ombaomba?

Aidha, kama katibu mkuu wa wizara analipwa kila mwezi mshahara mnono, lakini papo hapo serikali inamlipa posho kadhaa, tena bila kulipa kodi, uko wapi hicho kinachoitwa, “maisha bora kwa kila Mtanzania,” wakati wengi wao hawawezi kumudu hata mlo mmoja kwa siku?

Kuna usemi wa wahenga unaosema, “Mmulika nyoka huanzia miguuni pake.” Nasi tufuate. Tuondokane na ubinafsi wa kusema, “Tukikubali hoja hii, tutawapa mtaji CHADEMA.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: