Pinda ametangaza 'umasikini'


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametangaza "umasikini" wake na hakuna aliyemwamini, ikiwa ni pamoja na yule aliyemuuliza swali.

Shilingi 25 milioni kwenye akaunti yake, chumba kimoja katika nyumba ya babu, nyumba mbili za “kawaida” na gari moja kwa njia ya mkopo kwa mbunge.

Wanaoamini hayo waseme NDIYO. Wasioamini hayo waseme HAPANA. Waliosema HAPANA wameshinda. Kuna haja ya kutaja utajiri wake na siyo umasikini.

Enzi za TANU na CCM ya awali, “kiongozi” ilikuwa na maana ya mume na mke. Jinsi mambo yalivyokwenda yakibadilika, mama alichuma vyake na baba alichuma vyake.

Katika hatua nyingine ya “maendeleo,” ukaingia uchambuzi mpya; kwamba kama mama lwake na baba lwake, basi na mtoto lwake.

Waweza kutunga shairi:

Baba lwake,
Mama lwake,
Mtoto lwake
Tusiulizane!

Miiko ikazeeka au ikakatikakatika vipande. Walioitengeneza wakazeeka au wakatoweka mmojammoja kwa kunyakuliwa na “kinyemelezi.” Lakini hata kabla ya kutoweka kwao, uhusiano mpya ukazaliwa.

Heshima ya mume kitu gani; sharti uwe na chako. Heshima ya mke kitu gani sharti usinitegemee. Heshima ya mtoto ni nini kama kila siku ombaomba. “Tujitegemee.”

Awali waliishaimba: Usiwe kupe jitegemee. Baba wa Taifa keshasema kila mmoja ajitegemee. Wimbo shuleni kukariri; watoto wakue wakijua. Wanasiasa wazunguka nchi nzima kuimbisha wimbo mwepesi ulimini.

Ni enzi hizo. Enzi za baadaye hakuna anayechangia mwenzake. Aliyesoma katoka; amepata “maendeleo.” Wimbo uleule waimbwa kwa mantiki mpya.

Tajiri mwenye biashara ajitegemee. Mwenye kiwanda ajitegemee. Mkurugenzi ajitegemee. Ofisa ajitegemee. Mfanyakazi ajitegemee. Mkulima ajitegemee. Ombaomba ajitegemee. Wanasiasa wakaimba.

Mwanasiasa kastuka. Vipaumbele anaweka yeye. Mipango ya maendeleo anapanga yeye. Bajeti ya nchi anayo yeye. Misamaha ya kodi asimamia yeye. Sheria anatunga yeye. Ukwapuaji kokote kule ni katika msafara wa mamba na kenge yumo.

Baba kakaa siasani, mbele kabisa kujiweka; mengimengi kupakia na mdomoni kujikweza: Safi! Safi!

Sikilizeni wimbo mpya na mahusiano ya familia:

Nifanyavyo hivi mama
Nawe fanya himahima
Nifanyavyo hivi dogo
Nawe fanya utukuke
Kila mmoja avune
Na mwache kulalama
Mtaji huu nawapa
Kila mtu lwakelwake.

Miaka imekuja na miaka imekwenda. Walobaki madarakani miaka nendarudi utamu wakolea kila kukicha. Wengi walokwenda shule chamacho watamani; usipojiunga nao huli nao asilani. Kata kadi.

Mwishowe mazoea yamekuwa kanuni. Kila mwonja asali haachi mzinga kuchonga. Pengine miti wamekata, mizinga wamechonga na asali wamerika. Lakini wengine wamerudi na kuchoma nyuki; wameangamiza malkia.

Hakuna anayejali. Kesho ni ya wengine wao hawatakuwepo. Mla ni mla leo mla kesho kala nini? Miti imekatwa, nje kuuza magogo ndani kubaki jangwa. Madini yameuzwa na kuacha mahandaki.

Mbuga zimeuzwa kwa “wawekezwaji” na wao kujitangazia mataifa; huku wakifagia raia kama majani yapukutikavo mtini – wakiwaondoa kwenye makazi yao, matambikio yao, makaburi yao – ardhi yao.

Sera walizotunga, mipango waliyoweka na sheria walizohalalisha ni uza, uza, uza. Kama una fedha nunua kama huna nyamaza. Usilete wivu wa kiwifi! Kama unapinga kafilie mbali.

Na wanaotaka kulima ardhi wauzie lakini fanya kijanja. Wape miliki ya miaka 99 na wajinga wa Danganyika hawataelewa maana yake.

Watakaoelewa ni wachache na wao hawana sauti. Hawatungi sera, hawaandai mipango. Hawapitishi sheria. Wataishia kulalama, kusonya, mwishowe watafyata kwa kuwa hawajui maana ya “maendeleo;” kwa kuwa “wamevaa miwani ya mbao.”

Huko ndiko atokako Kayanza Mizengo Peter Pinda. Panga majina yake utakavyo. Yote ni yake. Kwanza wamemwita “mtoto wa mkulima” – ushabiki wa waliobahatika kuwa na vyombo vya mawasiliano.

Humo ndimo anaongelea Pinda Kayanza Peter Mizengo. Asipokubaliana nami kwa mpangilio wa majina haya basi ayapunguze abakie na mawili tunayoweza kukumbuka mpangilio wake.

Mtoto wa mkulima hatajali kuitwa vyovyote, kwani ndivyo humwita kijijini. Leo ni waziri mkuu. Mtendaji mkuu miongoni mwa mawaziri. Msimamizi. Nyapara – ukitaka.

Waziri kiongozi katangaza ana nini. Vinaitwa mali. Kasahau nini? Katangaza kwa misingi wa TANU au kwa msingi wa “kisasa?”

Nani atamlaumu kama katangaza kisasa. Tunasonga mbele. Hakuna anayetaka kurudi nyuma. Kisasa ni kutaka wakusikie. Kutaka wakujadili. Kutaka kuwemo. Ni mwenendo tu. Ni fasheni.

Nani atajua kuwa yaliyosemwa ndiyo yote katika fomu za kamisheni ya maadili? Pale kuna ugo mkubwa, mnene na mzito. Sheria imekaa kama chatu mrefu.

Licha ya kukuziba na kukukatizakatiza, chatu huyo aweza kuziba kabisa lango la kuingilia ofisi ya kamisheni. Ni miongoni mwa sheria zinazouma na kupuliza; zinazotoa kwa mkono mmoja na kunyakua kwa mwingine. Zinazozuia na kunyakua uhuru.

Pinda siyo mtoto wa mkulima tu; ni mtoto wa mazingira yote haya tujadiliyo. Hawezi kuyakimbia. Hawezi kujitenga. Hawezi kuacha kuathiriwa na hali hii.

Leo Pinda katangaza fedha alizonazo kwenye akaunti yake. Hakutangaza fedha za akaunti ya mke wake. Akaunti ya mtoto wake je?

Mke wa rais aliyemaliza muda wake alikuwa na mkoba ulioingiza fedha nyingi alizojua zilikuwa za nini; zilitumika wapi na nani alinufaika nazo.

Hata rais wa sasa mke wake ana mkoba unaoitwa wa maendeleo ya akina mama. Akina mama wa wapi; wepi na kwa shughuli zipi? Je, mke wa Peter yumo humu naye?

Bali kwa sasa twaweza kukubaliana na Mizengo Pinda kuwa anacho kile alichosema anacho. Lakini kuna waliosema HAPANA. Kwa hao kazi ndio imeanza.

Pinda atachimbwa na vyombo vya habari. Aviruhusu. Hata kama hana uwezo wa kuviruhusu, basi avivumilie. Kwanza ajue kwa nini aliulizwa na kwa nini waliouliza hawawezi kuwa na taarifa zaidi ya alizotoa?

Uaminifu wa Pinda sharti uandamane na juhudi zake za wazi za kurahisisha upatikanaji wa taarifa za viongozi wote.

Sheria inayotaka viongozi wataje mali zao iseme hivi: Kila mmoja atakayetaka kupata taarifa za viongozi katika kamisheni, aombe na apewe katika kipindi cha siku saba; na bila sharti la nyongeza.

Hapo basi! Subiri mfumuko wa ukweli usiopingika. Huenda Pinda akaitisha kikao kingine kusema ana hisa katika biashara yake na mke wake au na mtoto wake. Nani ajuaye.

Kuna wanaosema Pinda amejiweka pabaya. Atachimbwa. Kuchimbwa nini bwana? Ameishayavulia; atayaoga.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: