Pinda amtisha Rais Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda aweza kujiuzulu wakati wowote kwa kile kilichoelezwa ni “kulinda hadhi yake,” MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka mjini Dodoma zinasema iwapo Rais Jakaya Kikwete hatafukuza mawaziri watuhumiwa ufisadi na kushindwa kazi, basi Pinda aweza kujiuzulu.

Kwa siku nne mfululizo, wabunge wamemkoromea Pinda, wakitaka achukue hatua dhidi ya mawaziri wanane; la sivyo ang’atuke yeye.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, aliongoza mchakato wa kukusanya saini za wabunge ili kutoa hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu kwa kushindwa kusimamia mawaziri.

Mawaziri wanaotuhumiwa wametajwa katika ripoti za kamati tatu za kudumu za bunge zikinukuu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Ripoti ya CAG inayoonekana chachu kuu kwa wabunge kushinikiza mawaziri kujiuzulu, inaanika upotevu, wizi, ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi katika serikali na taasisi zake.

Lakini hadi juzi Jumatatu, wakati bunge likiahirishwa, Rais Kikwete alikuwa hajatoa neno juu ya shinikizo la wabunge kwa Pinda.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya rais kunyamazia malalamiko dhidi ya mawaziri wake, yaweza kumpotezea mtendaji mkuu anayeonekana msafi.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimesema tuhuma dhidi ya mawaziri na watendaji wengine serikalini ni za muda mrefu, lakini rais aliyewateua, ameamua kuwabeba.

Hata baada ya kuwa baadhi ya mawaziri wanatuhumiwa wizi, ubadhirifu wa fedha za umma na kushindwa kuwajibika kikazi, bado rais ameendelea kunyamazia.

Akizungumzia ukimya wa rais, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema, “…kama rais angefuata ushauri wangu wa kuvunja baraza la mawaziri mapema mwaka huu, haya ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu yasingekuja.”

Dk. Slaa aliyekuwa akihutubia mkutano wa hadhara jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, alisema, “Uozo wa serikali unatokana na baadhi ya mawaziri kufanya ubadhirifu kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua.”

Wiki hii zimepatikana taarifa kwamba mawaziri wawili wa Kikwete wamenunua nyumba za mabilioni ya shilingi jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao, miongoni mwa wanaoshinikizwa kujiuzulu, hawakupatikana kwa simu hadi tunakwenda mitamboni, ili watoe kauli kuhusu tuhuma hizo.

Hata hivyo, taarifa za upande unaotetea rais zinasema Pinda ndiye ameshindwa kutumia madaraka yake kudhibiti wabunge hadi wakafikia hatua ya kumkoromea.

Wabunge wenyewe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamtetea Pinda kwamba asingeweza kuzuia kauli za kupinga ubadhirifu, hata kama wenye nia tofauti walipata nafasi ya kujipenyeza.

Mbunge ambaye hakutaka kutajwa jina amesema, kuna waliopaza sauti eti kwa kuwa “rais alikataa kuwaongezea posho” huku wengine wakidai baadhi ya mawaziri wakifukuzwa, wao wanaweza kufikiriwa kupanda ngazi.

“Tatizo ni kwamba pamoja na shinikizo kwa waziri mkuu, bado rais haonekani kushtuka. Hii inaleta hisia kwamba naye anataka kumtosa,” amesema.

Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki) amesema kuchoka malalamiko ndiko kumewasukuma kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

“Wabunge wamechoka kuona mawaziri wana mali nyingi zisizolingana na vipato vyao. Wanatumia madaraka vibaya kula rushwa, na hakuna hatua zinazochukuliwa. Ndio maana tunataka kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.”

Amesema ingawa rais halazimishwi kutekeleza mambo anayoshauriwa, lakini kunyamazia hayo yote ni kama kumwangusha waziri mkuu wake.

“Inawezekana hii ikawa ni kumwangusha waziri mkuu; maana huwezi kujua hasa inapokuwa siyo mteule wake wa kwanza. Unajua chaguo lake la kwanza alikuwa Lowassa (Edward) na huyu akaja kama chaguo la pili,” alisema.

Pinda aliteuliwa mara ya kwanza Februari 2008, baada ya Lowassa kujiuzulu.

Mbunge wa Bunda, Alphaxard Lugola amesema, “…naona tulikofikia katika hili, tuko sahihi. Hatuna nia mbaya na chama chetu. Tunalenga kuisaidia serikali. Nawashangaa wenye chama chetu wanaotushutumu.”

Lugola amesema ameamua kuwaunga mkono wabunge waliotia saini azimio la kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu kwa kuwa si yeye peke yake, bali wabunge wote wanataka serikali iwe na nguvu na iwaondoe mawaziri walioshindwa kazi.

“Nashangaa wanatulaumu eti tunataka kuangusha serikali ya CCM. Hoja hii haikuletwa na wapinzani; imeletwa na kamati ya bunge. Sioni sababu ya kutoiunga mkono,” amesema.

Mbunge mwingine wa CCM, Deo Filikunjombe (Ludewa), amesema tangu aweke saini azimio la kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, “…napigiwa simu kila kona kunipongeza, lakini ajabu wengine kwenye chama wananuna.”

Amesema wabunge wamefikia hatua hiyo katika kutimiza wajibu wao wa kuisimamia serikali badala ya kuendelea kuishauri tu kama walivyokuwa wamezoea.

“Wabunge tumechoka. Hao mawaziri wanane unaosikia wanalalamikiwa ni wachache tu; wako wengi wenye matatizo makubwa. Na hatua unazoona sio mwisho wake. Tunataka kukaa kama bunge imara kuisimamia serikali,” ameeleza.

Katika mkutano wa saba wa bunge uliomalizika Jumatatu, wabunge wa CCM na wa upinzani walishikamana kutaka kumng’oa Pinda iwapo mawaziri watuhumiwa hawatajiuzulu au kufukuzwa.

Februari mwaka huu, taarifa zilisema Rais Kikwete alikuwa anakusudia kubadilisha mawaziri kwa sababu ya “kuyumba kwa serikali,” lakini hakufanya hivyo.

Taarifa zinasema inawezekana alisita kutokana na vyombo vya habari kufichua mkakati wake mapema.

Bunge liliahirikishwa bila mawaziri watuhumiwa kuonyesha dalili za kujiuzulu; baadhi wakiapa hawatajiuzulu.

Mawaziri hao ni Mustafa Mkulo wa wizara ya Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Afya, Dk. Hadji Mponda.

Maeneo makuu ambayo CAG ameripoti ubadhirifu na wizi ni pamoja na Wizara ya Afya (Sh. 10 bilioni), Mabilioni ya JK (Sh. 21 bilioni), ukwepaji kodi (Sh. 15.4 bilioni), Maliasili na Utalii (Sh. 875 milioni) na magari ya serikali (Sh. 5 trilioni).

Pia katika Shirika la Viwango (Sh. 29.3 bilioni), mishahara hewa (Sh. 1.8 bilioni), Tanesco (Sh. 600 bilioni), Bodi ya Pamba (Sh. 2 bilioni), ununuzi tata (Sh. 8 bilioni), Idara ya Mhasibu Mkuu (Sh. 49. bilioni) na udhamini wa serikali Sh. 3 bilioni.

Taarifa za kuaminika zinasema mawaziri husika walibanwa katika kikao cha wabunge wa CCM, Alhamisi iliyopita wakitakiwa kujiuzulu; la sivyo waziri mkuu ajiuzulu kwa kushindwa kuwawajibisha.

Pinda aliyeongoza kikao hicho, aliahidi juzi hiyo kuwa angeeleza hatua ambazo zimefikiwa katika kumaliza suala hilo. Hadi anatoa hoja ya kuahirisha bunge hakusema lolote.

Ukimya wake uliwaacha wabunge na dukuduku; na hata Spika Anne Makinda alipohoji wakati wa kupitisha hoja ya kuahirisha bunge, sauti za kukataa zilisikika kama zinawiana au kupita zile za kukubali.

Hata hivyo, kwa mamlaka yake alihitimisha, “Nafikiri walioafiki wameshinda.”

0
Your rating: None Average: 4 (6 votes)
Soma zaidi kuhusu: