Pinda anafuata nyayo za Lowassa?


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 12 March 2008

Printer-friendly version
Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda

KATIKA kipindi cha miaka kumi ya utawala wake wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan Mwinnyi alifanya kazi na mawaziri wakuu watatu – yaani mara mbili alijikuta analazimika kuwabadilisha watendaji wake wakuu.

Awamu ya tatu, rais Benjamin Mkapa haikuona badiliko lolote la waziri mkuu. Frederick Sumaye, alimaliza kipindi chote cha miaka kumi ya utawala wa Mkapa, jambo ambalo kinaweza kuleta hisia kuwa Mkapa alikuwa makini zaidi katika kuchagua msaidizi wake mkuu.

Hisia hii inaweza kuwa potofu, kutokana na ukweli kwamba ni katika kipindi hicho ndipo kashfa nyingi za ufisadi zinazoibuliwa sasa zilianzia? Inawezekana kwamba Sumaye hakuhusika moja kwa moja na zahama hii inayolikabili taifa.

Nimelazimika kukumbushia yaliyojiri huko nyuma – kwa sababu kubwa moja: Katika kipindi cha miaka miwili tu, Jakaya Kikwete, rais wa Awamu ya Nne amelazimika kumbadilisha waziri wake mkuu, tena si kwa sababu na namna Ali Hassan Mwinyi alivyobadilisha. Huyu kambadilisha kutokana na kashfa nzito zilizohusu ufisadi zilizokuwa zikimkabili – yeye na mawaziri wawili wengine.

Na bado kuna miaka minane mbele yake, kitu ambacho kinaweza kuleta hisia kwamba katika kasi hii atajikuta kabadilisha mawaziri wakuu mara tatu au zaidi. Nami ninaamini kabisa itakuwa ni hivyo tu, tuombe uhai.

Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda ametajwa kuwa ni "Bwana Msafi" kwamba hajatajwa, hata katika minong'ono, kwamba aliwahi kukumbwa kwa kashfa hii au ile, hususan katika masuala ya ufisadi.

Nakimbilia kutaja "ufisadi" kwa sababu siku hizi ndiyo suala ambalo limeletwa mbele ya macho ya umma. Kwa ujumla ninaweza kusema sasa wananchi wamepa mwamko wa kuwatathmini viongozi wao katika masuala ya ufisadi – yaani iwapo anahusika na kashfa yoyote ile ya ufisadi.

Hali kadhalika Pinda ametajwa kuwa ni mzoefu mkubwa katika uongozi wa umma (public service) – na hasa katika ngazi ya juu kabisa (akiwa Ikulu kwa miaka zaidi ya 20) sifa ambayo inaendana vyema na wadhifa wa uwaziri mkuu – maana waziri mkuu ni mtu wa vitendo.

Na kwa upande mwingine Pinda ana uzoefu mkubwa katika masuala ya tawala za mikoa na za serikali za mitaa kwani ameongoza wizara hiyo kwa miaka miwili iliyopita. Kwa ujumla, chaguo la Kikwete linaonekana kuwa halina dosari kabisa. Je, hiyo ni hakika?

Mimi nasema la, sifa zote hizo hazibashirii kabisa kwamba utendaji kazi wa Pinda utakuwa wa kutukuta. Nasema hivi kwa sababu mfumo wa uongozi katika nchi hii, chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni mfumo unaoendeshwa na viongozi.

Hali hii haitoi nafasi kwa kiongozi yoyote yule katika ngazi za juu kutoa mchango wake mzuri kwa taifa lake hata kama ana dhamira hiyo. Mfumo hauruhusu kiongozi mmoja mmoja kuwa shujaa (hero) katika utendaji wake wa kazi.

Ni lazima kiongozi afuate mfumo uliopo – ambao umeshaonekana ni mbovu hasa katika masuala ya vita dhidi ufisadi. Hivi wananchi hawawezi, kwa mfano, kujiuliza: kwa nini ndani ya utawala wa CCM, hakuna viongozi wa aina ya Kabwe Zitto, Dk. Willibrod Slaa au Chacha Wangwe?

Mwananchi gani, anayelitakia mema taifa lake, atabisha kwamba mchango ulionyeshwa na viongozi kama hawa ndiyo unaotakiwa katika taifa?

Inawezekana, kwa dhati kabisa, utawala wa CCM ungependa kumnasa mtu kama Kabwe na kumuingiza katika uongozi wake. Lakini pengine si katika kumuendeleza katika hayo anayosimamia, ni katika kumnyamazisha, kumbadilisha na kuwa mtu wa hovyo kama walivyo wenyewe.

Tumewaona baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliohama vyama hivyo na kujiunga na CCM. Mara baada ya kufika huko wakaanza kuongea lugha tofauti na ile waliyokuwa nayo awali. Watu makini wamekuwa wanajiuliza, wamelishwa nini hawa?

Si kwamba viongozi shupavu na jasiri hawamo ndani ya chama hiki, hapana. Wapo tena wengi sana, lakini tatizo kubwa ni mfumo unaominya mawazo ya wengi.

Turudi kwa Pinda ambaye ni "Bwana Msafi." Je, ataendelea kuwa hivyo hivyo? Mkapa, wakati anaingia madarakani mwaka 1995 alikuwa ni "Bwana Msafi" – hakuwa na dosari yoyote hasa katika kashfa za ufisadi au uongozui mbovu. Lakini tazama jinsi alivyojikuta anabadilika, hasa katika miaka yake ya mwisho, na sasa hivi anakabiliwa na tuhuma nzito nzito za ufisadi na utumiaji mbaya madaraka.

Ishukuriwe tu kwamba CCM inazingatia vikomo vya vipindi vya utawala wa marais (presidential term limits) na ile hali ya kulindana kulikokithiri, ama sivyo kiongozi kama Mkapa angeweza kung'ang'ania madaraka bila ukomo kwa kuhofia kwamba akiachia ngazi atajikuta katika wakati mgumu, pengine hata kusimamishwa kizimbani.

Aliyekuwa rais wa Kenya, Daniel arap Moi ni mfano mzuri wa kiongozi ninaosema, na hadi sasa hatuwezi kusema kwa hakika kuwa amepona kushitakiwa.

Kwa hivyo Pinda atajikuta tu anasukumwa na mfumo uliopo, hata kama ana mazuri gani anayotarajia kuwafanyia wananchi. Atasukumwa na mfumo unaokumbatia ufisadi, kuwalinda mafisadi, kula nao sahani moja n.k.

Kwa mbali sana, na kwa kiasi fulani, haya ninayosema yanaanza kujionyesha. Katika ziara yake mkoani Rukwa wiki iliyopita, Pinda, katika mkutano wa hadhara, alimsimamisha kazi Afisa Mtendaji wa Kata katika Wilaya ya Nkansi kwa kosa la kutowajibika.

Bahati nzuri halikuwa katika masuala ya ufisadi. Huyu ni afisa wa ngazi ya chini kabisa katika Wizara ya tawala za mikoa na Serikali za Mitaa, wizara ambayo Pinda aliiongoza kwa miaka miwili iliyopita.

Swali: Hivi kweli Pinda hakuona pa kuanzia isipokuwa kwa "sisimizi" huyo? Hivi katika Wizara hiyo, ambayo inasimamia halmashauri zote nchini (zipatazo 130) ni "sisimizi" huyo tu ndiyo "kafara" (victim) wa kwanza wa hasira za Pinda?

Simtetei afisa huyo wa Kata, na pengine ni kweli alikuwa ana hatia. Lakini ninachotaka kusema ni kwamba iwapo Pinda angemfumbia macho huyo na kuanzia kwa "tembo" ningesema naam, kweli sasa tumepata Waziri Mkuu, au tuseme tumepata Edward Sokoine mwingine.

Lakini kwa hatua yake hii ya sasa, tena ya kumsimamisha kazi afisa wa serikali katika mkutano wa hadhara, kunaweza kumtia doa "Bwana Msafi," na kwamba wengi wanaweza kulinganisha utendaji wake wa kazi na mtangulizi wake, Edward Lowassa.

Ikumbukwe kwamba wakati Lowassa akiwa Waziri Mkuu, Pinda alikuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Lowassa. Kwa maneno mengine, Pinda na Lowassa wanafahamiana vya kutosha. Kufahamiana huko, kunaweza kuchangia Pinda akafuata nyayo za Lowassa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: