Pinda anatutuliza huku anatuumiza?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametufungua macho wengi. Hili limejidhihirisha wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake bungeni, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika kujibu hoja za wabunge, Pinda alisema mengi ambayo mengine yaweza kumrudia yeye mwenyewe au serikali yake kama hayatatekelezwa.

Kwa mfano, waziri mkuu ameeleza kwamba haitoshi kuendelea kushabikia ripoti za Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa fedha za umma (CAG). Badala yake sasa, serikali imetoa maagizo kwa CAG kuwaripoti kwa vyombo vya dola watendaji wa serikali wanaotafuna fedha za umma ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pamoja na kwamba hili ni jambo zuri, nani anaweza kuthibitisha kwamba kesi zitafunguliwa na wahusika watapatikana na hatia katika mazingira haya ya serikali kuendeshwa kishikaji?

Kwa nini CAG asipewe meno zaidi ya kuchunguza na kisha kuleta mashitaka mahakamani, bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP)?

Ni kwa sababu uzoefu umeonyesha ni kwa kupitia kwa DPP, kesi nyingi zimezorota; wengi walioshitakiwa wameshinda kesi zao mahakamani kutokana na ujuzi mdogo walionao waendesha mashitaka na wapelelezi wanaojihusisha na kesi za udanganyifu katika masuala ya fedha.

Na hili si jambo geni. Kwa mfano, nchini Marekani, idara ya kodi nchini humo (IRS) inaendesha yenyewe kesi zake mahakamani pale itakapojiridhisha kuwa mtu binafsi au shirika limekwepa kodi.

Sasa kama hivyo ndivyo, kwa nini CAG ambaye anafanya uchunguzi wa kisayansi wa kipelelezi (forensic auditing) asiwe na uwezo wa kutumia ushahidi alionao kufungua mashtaka dhidi ya watu anaowashuku kutumia fedha vibaya au madaraka yao vibaya?

Binafsi nimechoka kuiona ofisi ya CAG inarudia kila mwaka kupendekeza mambo yale yale, akitoa maangalizo yale yale kwa viongozi wale wale huku akidai meno zaidi ya kufanya kazi yake. Hakuna nguvu kubwa kama kumpa uwezo wa kufungua mashtaka hadi ya kuhujumu uchumi yeye mwenyewe.

Kama kweli watu wanataka watu wawajibike ni vema serikali ikampa CAG madaraka ya kisheria ya kuleta mashtaka ikiwemo kutoa taarifa kwa kiongozi wa idara, wizara na taasisi za umma wanaoshindwa kusimamia mali ya taifa.

Tujiulize: Kwa nini serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaogopa kumpa nguvu hizi? Ni kwa sababu ya kuhofia kuumbuliwa kwa maswahiba zao? Nini basi?

Kisingizio pekee wanachotoa, ni kwamba itakuwaje yeye mwenyewe awe mchunguzi na mleta mashtaka? Inawezekana na kwa hakika, hili si jambo geni.

Pili, Pinda amelionya jeshi la polisi kwamba wasije kudhania kuwa wanaweza kunyopoa roho za Watanzania bila kufanyiwa uchunguzi. Binafsi kati ya yote aliyozungumza hili lilikuwa ni kubwa sana; wengi wetu kama kweli litatekelezwa limetupa faraja.

Amesema pale inapotokea uhai wa mtu umeondolewa, ni lazima taratibu za kisheria zichukuliwe. Vifo hasa vile ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya vyombo vya dola, ni lazima vichunguzwe. Ameanisha hata sheria inayoruhusu utaratibu wa kufanya uchunguzi wa vifo vya aina hii kuwa ni Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, (The Inquest Act).

Kutokana na hilo, waziri mkuu akahitimisha kuwa “katika madai yaliyowasilishwa na waheshimiwa wabunge, hususan kutoka kambi ya upinzani kuhusu mauaji yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa vyombo vya dola, ni vyema ikaeleweka kuwa, serikali haina nia ya kupuuza shutuma hizi za mauaji ya raia wake.”

Alisema katika kulishughulikia suala hili la mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa sasa serikali imefikia uamuzi wa kuvichunguza vifo hivyo kwa kupitia sheria hiyo husika.

Pinda bila kelele wala mbwembwe amesema kitu ambacho kilihitaji kupewa uzito mkubwa kwenye vyombo vya habari, kwamba vifo vyote ambavyo vimetokea kwa sababu ya matumizi ya nguvu au kifo cha raia kisicho cha kawaida kilichotokea akiwa chini ya uangalizi wa vyombo vya dola, vitachunguzwa na hatua zitachukuliwa.

Amesema waziri wa mambo ya ndani ya nchi atafafanua suala hili. Lakini kimsingi serikali imeshaanza mipango ya awali ya kushughulikia tatizo hili.

Kwa ufupi, kuanzia sasa polisi au vyombo vya usalama visije kufikiria kuwa vinaweza kutoa roho za Watanzania kwa kisingizio cha “kufuata amri” au “kulinda amani” bila kujali matokeo ya hicho wanachokitenda.

Na kwa vile huu ndio msimamo wa serikali ni matumaini ya wengi, kwamba wahusika watayachukulia maneno haya ya serikali kama deni. Kama sheria iliyotajwa ina matatizo au haijitoshelezi, ni wajibu wa watunga sheria kuifanyia mabadiliko ya haraka ili iendane na wakati uliyopo, ikiwamo kuendana na maendeleo ya sayansi ya vinasaba, uchunguzi na utunzaji wa ushahidi.

Je, hili nalo litatekelezwa? Jibu analo Pinda mwenyewe.

Tatu, pamoja na kwamba waziri mkuu amejaribu kujionyesha kuwa yeye siyo mtu wa kukanyaga bila kuangalia, siyo waziri mkuu anayeimbwa na kusifiwa kama waliomtangulia, lakini amemfikishia ujumbe kiana mtangulizi wake, Edward Lowassa.

Katika majibu yake kuhusu hoja ya maamuzi magumu iliyotolewa na Lowassa, Pinda angeweza kutupa madongo mazito ya kisiasa na kummaliza kabisa mwanasiasa huyo, lakini hakufanya hivyo.

Badala yake, Pinda alitoa jibu ambalo limepangwa vizuri, limetolewa kwa kufikiri na lililolenga kutuma ujumbe “do not tempt me” - usinijaribu. Kama Lowassa na wale wanaomuunga mkono wana hekima ya kisiasa basi wangeweza kusema sasa tuende taratibu.

Hivyo basi, kwa vyovyote itakavyokuwa Pinda ameonyesha alama mbalimbali katika za uongozi wake. Inahitaji kuangalia kwa karibu kuziona kwani kama mtu anatarajia kutakuwa na vikundi vya ngoma na magazeti kumsifia asitarajie.

Inaoenekana hapendi makuu wala kujionesha kuwa anafanya mambo kumfurahisha mtu fulani au kundi moja wapo. Wakati mwingine inafaa kumsikiliza kwa karibu. Anaweza kuwa anathibitisha msemo wa wahenga, “miti inayoanguka ndio inapiga kelele, inayokamaa huchanua taratibu na watu kuona matunda yake.”

Jingine ambalo limedhihirika ni kwamba Pinda ni mpiga mahesabu vizuri, hasa hesabu za kisiasa. Amejibu kwa ufasaha hoja za wabunge. Hakukebehi mchango wa upinzani hasa katika suala la posho na mauaji ya raia yanayofanya na jeshi la polisi. Kilichosalia sasa, ni utekelezaji wa kile alichokisema? Je, kitafanikiwa? Huo ndiyo mtihani kwake na chama chake.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: