Pinda atajwa mauaji Arusha


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

JITIHADA za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuepusha maafa mjini Arusha, zilihujumiwa na serikali, MwanaHALISI limeelezwa.

Vyanzo vya taarifa vinasema kabla ya CHADEMA kuitisha upya mkutano na maandamano ambamo polisi waliua watu watatu, katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa alitaka kufanyike mkutano wa pamoja kati ya chama chake na waziri mkuu, Mizengo Pinda.

Mkutano huo ungejadili na kutafuta suluhu kwa migogoro iliyoibuka katika manispaa za Arusha, Mwanza, Kigoma Ujiji na Hai, mkoani Kilimanjaro.

Katika miji yote mikubwa ambako CHADEMA ilizoa ushindi au ilipata viti vingi vya madiwani, kuliibuka migogoro juu ya nani awe meya; hata pale ambako ushindi ulikuwa wazi kwa chama hicho, kama ilivyokuwa Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, ombi la Dk. Slaa kutaka kukutana na Pinda liliwasilishwa serikalini kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.

Uamuzi wa Dk. Slaa kutaka kukutana na Pinda ulifikiwa kutokana na ombi la Tendwa la kutaka uongozi wa CHADEMA kufuta maandamano yao yaliyokuwa yamepangwa kufanyika 30 Desemba mwaka jana.

Waziri mmoja ndani ya serikali amelieleza MwanaHALISI, “Ndugu yangu, lakuvunda halina ubani. Dk. Slaa alifanya kila liwezekanalo kuepusha maafa. Lakini viongozi wa serikali yetu, si wasikivu. Badala ya kutumia busara, wametumia mabavu.”

Amesema tarehe 22 Desemba mwaka jana, Dk. Slaa, Tendwa, Mbowe (mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA) na Inpekta Jenelali wa Polisi, Saidi Mwema, walijadili namna ya kumaliza migogoro “…hasa Arusha, lakini wapi, serikali haikutaka kusikiliza.”

MwanaHALISI limeelezwa kuwa mazungumzo ya viongozi hao wanne yalilenga kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro ya uongozi katika manispaa na halmashauri zenye madiwani wengi wa upinzani ili kuepusha migogoro na hata umwagaji damu.

Gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja, sababu ya serikali kukataa au kuchelewa kuzungumza na CHADEMA, ingawa kuna taarifa kuwa mazungumzo hayo yalikwamishwa na msimamo wa Yusuph Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Makamba amekuwa akisisitiza kuwa uchaguzi wa meya katika manispaa ya Arusha umemalizika; na mjadala juu ya suala hilo umefungwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alikiri siku moja baada ya mauaji ya Arusha, kuwapo mazungumzo aliyoita ya chini kwa chini ili kumaliza mgogoro wa kisiasa mkoani Arusha.

Akionekana kujitua tukio hilo, Nahodha alisema, “…kilichotokea Arusha ni mgogoro wa kisiasa, unahitaji kutatuliwa kisiasa pia. Sote tuna wajibu wa kulinda amani katika taifa letu…”

Alisema, “Zilikuwepo juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Arusha, ambazo zilikuwa zikifanyika chinichini, lakini kutokana na hali ilivyo sasa, itabidi usuluhishi huo kufanyika kwa uwazi,” alieleza Nahodha ambaye amepata uzoefu wa mgogoro kama huo visiwani Zanzibar.

Katika barua yake ya 22 Desemba 2010, Dk. Slaa alisema chama chake kimekubali kufuta maandamano kiliyoitisha 30 Desemba 2010 na kumtaka msajili wa vyama kuratibu mazungumzo ya kutafuta suluhu katika migogoro hiyo.

“…Kwa kuheshimu mazungumzo kati yetu (Dk. Slaa/Tendwa) ya mchana wa leo tarehe 22 Desemba 2010; na mazungumzo kati yako na Mheshimiwa Freeman Mbowe na IGP kwa nyakati tofauti siku na tarehe hiyohiyo… tunakubali kusitisha mkutano uliopangwa lakini kwa masharti…” inaeleza barua ya Dk. Slaa.

Barua ya Dk. Slaa, Kumb. Na. C/HQ/ADM/MSJ/04/45 iliyotumwa kwa Tendwa ilikuwa na kichwa cha maneno kisemacho, “Mkutano na waziri mkuu kuhusu migogoro inayotokana na uchaguzi wa mameya na wenyeviti wa halmashauri.”

Masharti ambayo Dk. Slaa aliyataja ni kuwa na “mkutano wa ngazi ya juu, na ikiwezekana ahusike pia waziri mkuu, viongozi wa TAMISEMI, utakaoratibiwa na Msajili wa Vyama kwa siku na mahali utakapotuelekeza wewe.”

Pili, Dk. Slaa anaeleza, “Kati ya leo na tarehe 5 Januari 2011 kusifanyike uchaguzi wowote wa Mameya au Mwenyekiti katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispa ya Arusha, Manispa ya Kigoma/Ujiji na Halmashauri ya Hai.”

Hata hivyo, Dk. Slaa anaonya, “Iwapo hadi tarehe 4 Januari hakuna hatua yoyote kuhusu majadiliano yaliyokusudiwa, au hujuma itaendelea kufanyika, basi CHADEMA tutalazimika kuitisha maandamano ya amani 5 Januari 2011…”

Anasema, “Polisi wenyewe ni watuhumiwa katika matukio ya Arusha na hivyo kama hapatakuwa na maridhiano yoyote ifikapo tarehe 5 Januari 2011, basi serikali itakuwa imetulazimisha kuchukua hatua hiyo.”

Alisema uchaguzi wa wenyeviti na mameya hao  umevurugika kutokana na maelekezo kutoka ngazi za juu za serikali, jambo ambalo amesema limesababisha uvunjifu wa amani.

Anasema pamoja na yeye na chama chake kujitahidi kutuliza wapenzi wao, hata baada ya wananchi kupigwa mabomu ya machozi na polisi bila sababu mkoani Arusha, lakini serikali imekuwa haitaki kusikiliza kilio chao.

Alitaka wakati suluhu inatafutwa, serikali ianze kuchukua hatua dhidi ya watumishi wake wanaotuhumiwa kuvuruga uchaguzi na kusababisha hali ya mashaka nchini.

Waliotakiwa kuwajibishwa ni pamoja na  mkurugenzi wa Manispa ya Arusha anayetuhumiwa kuendesha uchaguzi kinyume cha taratibu.

Wengine ni viongozi wa Tamisemi walioingilia uchaguzi katika mji wa Kigoma/Ujiji na mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha (OCD) aliyeingia ndani ya ukumbi wa mkutano wa baraza la madiwani kumshambulia mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema.

Alionya kuwa chama chake hakitaendelea kuvumilia kitendo cha kukamatwa kwa mbunge ndani ya kikao halali; na “vivyo hivyo, kitendo cha wakurugenzi na Tamisemi kupindisha taratibu zilizowekwa nacho hakitavumiliwa.”

Akiandika kwa msisitizo, Dk. Slaa alisema, “Ni vema serikali sasa ikajua hivyo; CHADEMA itafanya mkutano na waandishi wa habari kuwaomba wananchi wa Arusha watulie hadi watakapojulishwa hatua zaidi, iwapo serikali haitakuwa imechukua hatua.”

Inaelezwa kwamba baada ya muda uliotolewa na CHADEMA kupuuzwa na serikali, ndipo chama hicho kiliamua kuitisha maandamano ya amani na mkutano wa hadhara kama ambavyo walikubaliana katika mazungumzo ya awali kati ya Mwema, Mbowe, Dk. Slaa na Tendwa.

Hata hivyo, saa chache kabla ya maandamano hayo kufanyika, IGP Mwema alifuta maandamano hayo kwa kile alichodai, “Kupata taarifa za kiintelijensia zinazoonyesha kutatokea vurugu wakati wa kufanyika kwake.” 

Hatua hiyo ya IGP ndiyo ilisababisha mtafaruku mkubwa ambapo jeshi la polisi lilishambulia viongozi, wanachama, wafuasi, mashabiki wa chama na wananchi kwa kutumia risasi za moto, mabomu ya machozi na maji ya washawasha.

Maandamano yaliyoitishwa na CHADEMA yalilenga kushinikiza kufanyika upya kwa uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Arusha baada ya uchaguzi wake kukiuka taratibu.

Aidha, maandamano yalilenga kuhamasisha wananchi kote nchini kushiriki katika kutoa maoni yao bila woga kuhusiana na hoja mbichi ya kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.

Shambulizi dhidi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA limefanyika miezi miwili baada ya wabunge wa chama hicho kutoka nje ya Bunge huku Rais Jakaya Kikwete akihutubia taifa.

CHADEMA walidai kuwa hatua hiyo ililenga kushinikiza kuandikwa kwa katiba mpya, kuunda tume ya kuchunguza wizi katika uchaguzi uliopita na kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi. 

Katika tukio la mauaji la Arusha wiki iliyopita, gazeti la Serikali, HabariLeo, limeeleza kuwa serikali ilitumia polisi, mgambo na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kupambana na wafuasi wa CHADEMA.

Katika tukio hilo, viongozi mbalimbali wa CHADEMA akiwamo Dk. Slaa, Mbowe, mbunge wa Moshi Mjini Philimon Ndesamburo, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na mbunge wa Rombo, Josep Selasini, walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kufanya maandamano bila ruhusa ya polisi.

Naye mchumba wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi alijeruhiwa kichwani na kuvuja damu nyingi, huku watu wengine watatu walipigwa risasi za moto na kujeruhiwa sehemu mbalimbalai mwilini.

Tangu CHADEMA ianike orodha ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi chini ya kile walichoita, “List of Shame” – chama hicho kimekuwa thabiti katika kuibua ufisadi nchini, jambo ambalo limekera utawala.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: