Pinda na danadana kuhusu Zanzibar


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Kutoka Bungeni

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezidi kupiga “danadana” ahadi yake ya kulipa kifuta machozi kwa familia zilizopoteza raia wakati wa maandamano yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) kudai uchaguzi mpya baada ya ule wa 2000 kuvurugwa kwa nia ya “kupendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia bunge wiki iliyopita kwamba suala la serikali kulipa kifuta machozi kutokana na maafa yaliyotokea wakati huo, ufumbuzi wake unaendelea kufuatiliwa.

Pinda alisema suala hilo limekuwa likiendelea kufuatiliwa ingawa linakabiliwa na vikwazo; bado ufumbuzi muafaka haujapatikana. Hata Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikieleza visingizio chungu nzima vya kushindwa kutimiza ahadi yake.

Askari wa Serikali ya Muungano, hasahasa polisi, pamoja na vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walipiga risasi waandamanaji Unguja na Pemba na kuua watu wasiopungua 23 kama ilivyothibitishwa na Tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Hashim Mbita.

CUF walipinga idadi hiyo kwa kusisitiza kuwa kwa walivyotafiti wao nchi nzima ambako maandamano yalifanyika pia Dar es Salaam na maeneo mengine, zaidi ya watu 70 waliuawa.

Mauaji hayo yaliyochafua taswira nzuri ya Tanzania ya kuwa nchi ya amani ambayo haijazalisha wakimbizi katika historia yake kwa watu kadhaa kukimbilia nchini Kenya na baadaye Somalia, yalishutumiwa kote duniani na mataifa na mashirika ya watetezi wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa makubaliano ya muafaka yaliyofikiwa na vyama hivyo viwili mwaka 2002, ambayo yalisaidia kuzima hisia za chuki zilizokuwa zimezama nyoyoni mwa wananchi Zanzibar, serikali ingeanzisha mfuko maalum ambao ungechangiwa na wafadhili kwa ajili ya malipo ya kifuta machozi kwa familia za watu waliouawa katika maandamano hayo.

Mbali na mauaji yaliyotokea, vikosi vya serikali vilituhumiwa kwa utesaji na udhalilishaji wananchi wakiwemo wanawake ambao baadhi walibakwa mbele ya waume na watoto zao.

Wabunge wa CCM wanapojikomba

KILEKILE wanachokililia wabunge wa kambi ya upinzani, ndio hichohicho wanachokidai wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – maendeleo katika maeneo yao.

Wabunge wa upinzani wanapojadili hoja za serikali, pamoja na mambo mengine ya kitaifa, hugusia matatizo yanayokabili majimbo yao, na hivyo ndivyo wafanyavyo wabunge wa CCM pamoja na kuunga mkono mia kwa mia kwa hoja zote za serikali.

Ufuatiliaji wa gazeti hili kwa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni wiki iliyopita, umebaini kumbe hata wabunge wa CCM wanaoshutumu wabunge wenzao wa upinzani kwa kuikosoa serikali, nao majimboni kwao hakuko sawa.

Tena, wabunge wa CCM hujikuta wakilazimika kupoza shutuma za upinzani kwa serikali, kwa kutangulia kuwaponda wapinzani na mwishoni, wakitamka, “sasa nakwenda jimboni ambako, tuna matatizo mengi….umasikini.”

Staili hii ya wabunge wa CCM kujikomba kwa serikali, imejidhihirisha wakati Kapteni John Komba (Mbinga Magharibi) alipochangia hoja ya bajeti ya serikali kama walivyofanya Jenista Mhagama (Peramiho), Deogratias Ntukamazima (Ngara), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki) na Ali Kessy (Nkasi).

Wabunge wa upinzani walioibana serikali kwa udhaifu wa kutowajibika, kupitia makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni pamoja na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini, CHADEMA), aliyetaka msimamo imara wa serikali kuhusu alichokiita “Operesheni haramu” ya kusaka wananchi wa Kigoma na kuwatangaza kuwa si raia halali wa Tanzania.

Zitto ambaye pia ni naibu kiongozi wa upinzani bungeni na waziri kivuli wa fedha na uchumi, aliliambia bunge kuwa operesheni hiyo ni ya kihuni na inapaswa kukoma ili wananchi wa mkoa wa Kigoma waishi kwa amani na kutafuta maendeleo kwa kuwa mkoa wao umeachwa nyuma na serikali tangu uhuru.

“Mkoa wa Kigoma wamekosa nini. Mbona wananyanyaswa pasina sababu za msingi. Hizi operesheni za kuwasomba kwa malori na kuwatoa nje ya mkoa huku wakitangazwa si raia wa Tanzania ni haramu na zikome,” alisema, akimwelekea Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Serikali yauma, yapuliza TANESCO

SERIKALI haitatoa tena dhamana kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuliwezesha kupata mkopo wa fedha za kusaidia miradi yake ya maendeleo.

Hii imethibitishwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akijibu hoja bungeni wakati bunge likiwa limekaa kama Kamati ya Matumizi kupitisha makadirio ya matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu na TAMISEMI.

Waziri Prof. Muhongo alisema badala ya kutoa dhamana hiyo kwa TANESCO, serikali imetafuta njia nyingine ya kusaidia shirika hilo kujiendesha ikiwemo kuliwezesha kupata mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme.

“Ukitoa dhamana kwa mkopo wanaotaka kukopa, shirika litabaki na fedha zisizozidi Sh. 3 bilioni. Hizi hazitaifikisha TANESCO popote. Sasa tumetafuta njia… mnaona sasa tuna umeme wa kutosha bila ya kuwepo mgao. Tutaendelea kulisaidia hivo,” aliliambia bunge.

Prof. Muhongo alisema tatizo kubwa lililopo TANESCO kwa sasa ni kukabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni kiasi kwamba hata wakikopeshwa fedha walizotaka kupitia dhamana ya serikali, wakizipata itakuwa ni sawa na “kumwaga glasi ya maji baharini.”

Waziri alikuwa ameulizwa ni lini serikali itatoa dhamana kwa TANESCO ili ipate mkopo wa Sh. 408 bilioni za kuendeshea shughuli zake. Mkopo huo ulitarajiwa kutoka Citi Bank Limited ya Uingereza.

Katika maelezo yake ya awali, mbunge alisema TANESCO ina hali ngumu kifedha wakati serikali iliahidi mwaka jana kutekeleza mpango wa dharura kupatikana umeme wa kutosha.

Wakati ikijiahidi kushawishi wabunge wapitishe mpango wake huo, serikali iliahidi kuipatia TANESCO dhamana ili kukopa kwa benki hiyo kwa niaba ya benki za umma za National Micro-Finance (NMB) na National Bank of Commerce (NBC).

Kauli mpya ya serikali inakuja huku taarifa za ndani ya TANESCO zikithibitisha kuwa taratibu zote za kupatikana kwa mkopo huo zimekamilika na kinachosubiriwa ilikuwa ni dhamana hiyo.

Kwa hatua hiyo, TANESCO itaendelea kuchechemea kwa kuwa mapato yanayopatikana kutokana na kuuza umeme kwa wateja, hayatoshelezi kugharamia shughuli za uendeshaji pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo.

TANESCO imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya fedha kutokana na kulazimika kulipa fedha nyingi kulipia mafuta ya mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme (IPP).

Jumapili iliyopita, Waziri Prof. Muhongo alizindua rasmi kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kilichojengwa kwa mkopo wa Dola 124,895,988 uliodhaminiwa na serikali ya Norway kupitia kampuni ya GEIK ya nchi hiyo. Benki iitwayo HSBC ndiyo waliotoa mkopo wakati wakandarasi ni kampuni ya Jacobsen Electro AS pia ya Norway.

Kituo hicho – Ubungo II – kilichopo Ubungo, nyuma ya jengo la makao makuu ya TANESCO, kina uwezo wa kuzalisha megawati 105 na tayari kimeanza tangu Juni mosi, kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.

Kuzinduliwa kwa kituo hicho katika sherehe iliyofana, kunaongeza umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi kuwa sasa megawati 544 na hivyo kupunguza utegemezi wa umeme unaozalishwa kwa kutumia maji na mafuta ambao kwa jumla unafikia asilimia 60 (41 kwa maji na 19 kwa dizeli).

Hatua hiyo inaonyesha sasa umeme unaozalishwa nchini kwa njia zote tatu ni megawati 1,375 na Waziri Prof. Muhongo amesema kuongezeka kwa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi katika mikoa ya kusini, kutaongeza uzalishaji wa umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Injinia William Mhando alisema katika hafla hiyo kituo hicho chenye mashine tatu, kinamilikiwa na serikali kupitia TANESCO kwa asilimia 100.

Alisema mashine hizo za aina ya STG 800, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 35, zimetengenezwa na kampuni ya Sweden, SIEMENS.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: