Pinda, Kikwete lao moja katika hili?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akiwasilisha bungeni mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu bungeni Dodoma Jumatatu wiki hii alisema:

“Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi yasiyo na tija, hususan ununuzi wa magari makubwa na ya kifahari ambayo  gharama za ununuzi na uendeshaji ni kubwa sana. Kuanzia mwaka 2012/2013, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa injini za magari ambayo yanaweza kununuliwa na Serikali Kuu na Taasisi zake pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000  kwa viongozi na  watendaji  wakuu na yasiyozidi CC 2,000 kwa watumishi wengine ambao wana stahili ya kutumia magari ya Serikali.

“Vilevile, ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya kanda vya magari ya Serikali au kila Ofisi itatenga magari machache yatakayotumika mikoani kwa shughuli za kikazi. Mwongozo wa utekelezaji utatolewa. Inategemewa kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya fedha za Serikali kwa kiwango kikubwa.” hii ni kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akiwasilisha bungeni mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu bungeni Dodoma Jumatatu wiki hii.”

Katika moja ya mikutano yake na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Pinda alipata kuweka wazi kuwa “kuna upinzani mkubwa sana katika kupunguza matumizi ya magari haya” kutoka kwa watendaji wa ngazi mbalimbali.

Lakini alichosema Pinda katika hotuba yake wiki hii ni sawa na kukataza ununuzi wa magari aina hiyo ambayo mengi huanzia cc 4,000 na kuendelea. Haya ni kama mlolongo wa Toyota Land Cruiser kama VX, VX V8, GX, Prado; mlolongo wa Nissan Patrol, Isuzu, Mitsubishi Pajero na mengine yanayofanana na hayo.

Kwa kifupi, magari haya ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi kwa sababu fedha ambazo zingeelekezwa kutatua kero zinaishia kuyaweka magari haya barabarani.

Kwa bahati mbaya sana, Pinda anaonekana kama hili ni suala lake binafsi. Ni wakubwa wachache sana, kama wapo, ambao wako pamoja na Pinda katika hili.

Ni vigumu sana kuelewa inakuwaje miaka minne sasa Pinda anazungumzia habari ya magari haya lakini hata ofisi yake inakuwa na ujasiri wa kuyaagiza na kumpa lake, ingawa alilikataa kwa kuwa aliona dhahiri ni sawa na kupigwa kibao usoni.

Pengine wakati wanaharakati wanapiga kelele juu ya udhaifu wa serikali juu ya ulevi huu wa magari, watumishi wengi wa umma wanaotumia magari haya wanaona kama vile wanapigwa vita; wanatafsiri harakati hizi na kile kinachojulikana kama ‘dua la kuku…’ au ‘sizitaki mbichi hizi’.

Mei 4, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri, baada ya kulazimika kuwaweka pembeni mawaziri sita na naibu mawaziri wawili kutokana na azimio la Bunge juu ya mawaziri wanane ambao walikuwa wametajwa kwa udhaifu wa aina mbalimbali katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2009/10.

Katika ripoti hiyo, ambayo Rais alikabidhiwa Machi 2011 naye kuipeleka bungeni mkutano wa Aprili 2011, kama katiba ya nchi inavyomtaka, alijua fika kuwa kuna madudu mengi ya ovyo humo ndani.

Hata kama hakusoma neno kwa neno, maelezo ambayo alipewa na CAG, Ludovick Utouh, yalitosha kujua kuwa mambo hayakuwa sawa kwa wasaidizi wake hasa katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.

Rais hakuchukua hatua zozote; aliona kuwa ripoti ya CAG ni sawa na ripoti nyingine nyingi tu ambazo amekuwa akiziwasilisha kwake naye kuzipeleka bungeni.

Lakini baada ya Kamati za Bunge, Kamati ya Fedha na Uchumi (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ile ya Mashirika ya Umma (POAC) kuungana na CAG juu ubadhirifu wa fedha za umma na madudu mengine na kisha kupitishwa kwa azimio la bunge juu ya mawaziri hao wanane, Rais Kikwete alijiona hana budi kuchukua hatua, lakini kwa picha inayoonekana kama ni kwa kushinikizwa.

Rais alikuwa na nafasi ya mwaka mmoja kuwapima mawaziri wake, kuwatafakari na kuchukua hatua kimya kimya bila kwanza kusubiri wabunge  wamvimbishie misuli ikiwa ni pamoja na kujaribu kumtikisa Waziri Mkuu wake, kwa kuanza mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye.

Hali hii inaacha somo moja dhahiri kwamba katika kujali kuhusu matumizi ya serikali ni wachache sana ndani ya mfumo wa serikali wanoajali.

Kwa kutazama tamko la Pinda bungeni wiki hii juu ya magari ya serikali, hakuna ubishi kwamba limelenga kusaidia kuokoa fedha za walipa kodi na kuwafanya watumishi wa umma waishi maisha yanayofanana na utumishi wao, siyo kugeuza ofisi hizo sehemu za kuponda raha.

Lakini tatizo ninaloliona hapa ni moja; Je, Rais Kikwete yuko pamoja na Pinda au anasubiri upepo ugeuke ndipo naye aingie kwenye vita ya kupinga mashangingi?

Itakumbukwa kuwa ni kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru, msafara wa rais umekuwa na aina ya magari tofauti na ilivyokuwa miaka yote ya Mercedes Benz, sasa ni BMW. Siku hizi msafara wa rais una jozi mbili za magari, Benz na BMW. Haya ni mabadiliko ya serikali ya awamu ya nne.

Lakini kuwako kwa BMW hakujaondoa pia mlolongo wa Toyota Land Cruiser hasa kwa safari za vijijini. Kwa hiyo, hii ni picha gani kwa wasaidizi wa Rais? Je, Rais naye yumo katika “dini hii” mpya ya kuacha ulevi wa matumizi yasiyokuwa ya lazima katika magari au ni dini ya Pinda tu?

Nilipata kusema huko nyuma kwamba katika nchi za Kiafrika, ambazo katiba za nchi zimetengeneza marais wenye nguvu kuliko hata wafalme, chochote atakacho Rais huyu huwa.

Kwa maneno mengine marais wa Afrika akiwamo wa Tanzania wana madaraka ya kisheria ya kuumba na kufanya lolote. Haya ni madaraka yaliyorundikwa kwenye sheria na katiba, wala hawahojiwi kokote.

Katika mazingira hayo, ninashindwa kujua ni kwa nini kuondoa mashangingi serikalini imekuwa kazi kubwa na nzito sana kama bwana mkubwa ana baraka zake katika maamuzi haya.

Katika hili nimeamua kuwa Tomaso, nimeamua kumpa Pinda pole kwamba vita hii ya kupambana na mashangingi serikalini kama bwana mkubwa hataonyesha kuunga mkono, Pinda mwaka mmoja ujao hatakuwa na cha kutuonyesha.

Serikali za Kiafrika hata kama hatutaki kuukubali ukweli ni mali ya marais wake, kwa Tanzania Rais Kikwete akitaka mashingingi yafikie mwisho leo yatafika, lakini kama hataki mzigo huu atabiringika nao Pinda hadi kijasho kimtoke kwa kuwa mwenye serikali yake hataki kuona kuna shida na kwa maana hiyo amejikalia kimya kana kwamba Pinda anacheza ngoma yake mwenywe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: