Pinda kupandishwa kizimbani


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda huenda akaburuzwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, imefahamika. Hatua hiyo inaandaliwa na wakazi wa kijiji cha Mgusu, kata ya Mtakuja, Geita mkoani Mwanza

Wananchi wanamtuhumu Pinda kufunga shughuli za uchimbaji dhahabu katika kijiji cha Mgusu ambazo kwa muda mrefu zimekuwa chanzo chao kikuu cha mapato.

“Hivi sasa tunawasiliana na mwanasheria. Tukimaliza taratibu zinazotakiwa, tutamfungulia mashitaka waziri Mkuu Mizengo Pinda,” ameeleza mmoja wa wananchi anayepigania kufunguliwa kwa machimbo ya Mgusu.

Kabla ya kumfikisha Pinda mahakamani, viongozi wa wananchi wamepanga kuandamana mpaka ofisi za mkuu wa wilaya Geita.

Wakiongea na MwanaHALISI wiki iliyopita, wananchi mbalimbali katika eneo hilo wamesema Pinda hawatendei haki kwa kuwafungia muda mrefu sehemu anayojua ndiyo inayowafanya waendelee kuishi.

Waziri mkuu alienda kijijini Mgusu tarehe 3 Aprili 2009 na kuagiza kufungwa mara moja kwa shughuli za uchimbaji dhahabu.

Hatua ya Pinda ilifuatia ajali iliyotokea machimboni hapo na kusababisha wachimbaji saba kukuporomokewa kifusi na kupoteza maisha.

Alipokuwa akifunga machimbo hayo, waziri mkuu aliahidi kuyafungua baada ya siku 90, lakini ni karibu mwaka mzima sasa na haijulikani yatafunguliwa lini.

“Anachokifanya waziri mkuu si sahihi. Hatupingi kuyafunga machimbo, lakini kuyafunga kwa muda mrefu kiasi hiki, hawatendei haki wananchi wa Mgusu,” ameeleza kaimu mtendaji wa kijiji cha Mgusu, Diackar Balele.

Naye Peter Marco Malebo, mmoja wa wakazi wa Mgusu amemwambia mwandishi wa habari hizi, “Wananchi wa Mgusu wanahujumiwa.”

Amesema wananchi wanajua, kwa kuona na kuambiwa, kuwa kuna watu wanachimba dhahabu ndani ya eneo lililofungwa. “Hili ndilo linaleta hasira na chuki kwa wananchi,” ameeleza.

Huku akiongea kwa kujiamini, Malebo anauliza, “Kwani machimbo peke yake ndiyo yanasababisha vifo? Mbona bahari haifungwi na inaua watu kila siku? Mbona barabara hazifungwi na ndizo zinaongoza kwa mauaji? Hapa kuna watu wanafaidika.”

Alipoulizwa diwani wa kata ya Mtakuja, Suzana Mashala (CCM), kuhusu nia ya wananchi kumpeleka kizimbani waziri mkuu, alijibu “…hata mimi nimesikia hilo lakini sijathibitisha.”

Taarifa zilizoenea katika eneo lote la machimbo ya Mgusu zinasema haitakuwa rahisi kufungua machimbo hayo mapema kwa madai kuwa “kuna viongozi wilayani ambao wanafaidika.”

“Tulifukuzwa humo. Tukaambiwa machimbo yamefungwa; lakini tunaona magari yaliyojaza vifusi vya mchanga yakitoka machimboni, ingawa machimbo yanalindwa na askari wenye silaha,” anaeleza kijana mmoja wa umri wa miaka 34.

Kijana huyu aliyeomba jina lake lihifadhiwe, anamtuhumu mkuu wa wilaya (DC) Geita, Philemon Shelutete kujua kila kinachoendelea migodini.

“Kama mkuu wa wilaya sharti awe anajua nani wanachimba; wapi wanapeleka mchanga na vipi wanaruhusiwa na polisi wanaodaiwa kulinda migodi,” ameeleza kijana huyo.

“Katika hali hii, kama waziri mkuu atamsikiliza DC, basi machimbo hayo hayatafunguliwa mwaka huu wala mwakani,” amelalama kijana huyo ambaye amekiri kuwa alikuwa mmoja wa wachimbaji wadogo.

Naye DC Shelutete hakupatikana kupitia simu zake mbili za mkononi (0713 745330 na 0784 696987).

Katibu Tawala wilaya, Marco Bakebula alikataa kusema lolote kuhusu madai ya wachimbaji na kumweleza mwandishi huyu kuwa “mkuu wa wilaya yuko safarini Dar es Salaam.”

Machimbo ya Mgusu yamekuwa yakiendeshwa na wachimbaji wadogo waliokuwa wanatumia majembe, sululu na vichokonolezi vingine.

Mwalimu Anatoria Msamba ambaye amefundisha shule ya msingi Mgusu kwa miaka 16 sasa, anasema waziri mkuu akienda Mgusu hataamini kama ndipo alipokwenda mwaka jana.

“Alipokuja alikuta wakazi wake wana afya. Lakini leo hii, kila mmoja amechoka kutokana na hali ngumu ya maisha baada ya machimbo yaliyokuwa yanawapatia wananchi riziki, kufungiwa kwa muda mrefu,” anaeleza.

Kauli hiyo inaungwa mkono na viongozi wa vitongoji waliohojiwa wanaosema Pinda alikuta uchangamfu kutokana na kipato, lakini leo hii “hataamini macho yake.”

Kuchelewa kufunguliwa machimbo kumeathri rika zote kijijini Mgusu ambako kuna kaya 950 zenye wakazi wasiopungua 5,700 umbali wa kilometa 28 Magharibi mwa mji wa Geita.

Hapa hakuna mashamba. Kijiji chenye ukubwa wa kilometa 70 za mraba kinapakana na eneo la mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) unaoendeshwa na kampuni ya Anglo Gold Ashanti.

Ukikaribia kijijini Mgusu unakaribishwa na harufu ya njaa ambayo inathibitishwa na watoto wanaoonekana kuwa waathirika wa utapiamlo.

Hata sauti za watu wazima zinazokukaribisha, zimejaa mikwaruzo.

Wazee wanaonekana kuchoka; vijana wana sura za kukata tamaa. Ukiuliza kwa nini, utapewa jibu moja haraka, kwamba ni kutokana na kufungwa kwa mgodi uliowaneemesha kwa mapato.

Salima Saidi ni mamalishe aliyekuwa anafanya biashara ya uhakika kabla ya waziri mkuu kufunga mgodi.

Salma anasema alikuwa anapika kilo 16 za mchele na chakula hakibaki. Hivi sasa amepunguza kipimo na kupika kilo tano na wali unabaki kuwa ndaza.

Alikuwa anakanda kilo 14 za unga kwa ajili ya maandazi, lakini hivi sasa anakanda kilo sita na hayamaliziki. Alikuwa anatumia kilo 15 za mchele kuoka vitumbua, lakini sasa anatumia kilo saba.

Watoto 20 kati ya 72 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza, mpaka sasa wameshindwa kujiunga sekondari kutokana na kutokuwa hata na fedha kidogo kwa mahitaji muhimu shuleni.

Kaimu mtendaji wa kijiji, Diackar Balele anamwonyesha mwandishi majina ya wanafunzi wasioripoti shuleni ambayo alipelekewa na walimu wa sekondari ya kata.

“Ndugu yangu hali ndio kama unavyoiona. Sina cha kufanya kwa sababu najua kuwa wazazi wao wakati huu hawana uwezo wa kununua hata shati la shule,” anaeleza Balele.

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya msingi Mgusu, Jacob Michael anasema wao kazi yao ni kufundisha kwa bidii ili wanafunzi waweze kufaulu, swala la kujiunga na sekondari liko nje ya uwezo wao.

Mwalimu Jacob anasema mwaka huu hawatarajii kufaulisha wanafunzi wengi kama mwaka jana kutokana na watoto wengi kutohudhuria kwa sababu ya njaa iliyokumba kijiji.

Wanaotaka kumshitaki waziri mkuu wanamhusisha pia na njaa ambayo imekikumba kijiji.

“Mahudhurio ya wanafunzi hivi sasa yanatisha. Robo tatu ya wanafunzi hawahudhurii masomo kwa siku kutokana na njaa,” anaeleza mwalimu mmoja.

Mwalimu wa taaluma, Selelii Magida wa shule ya msingi Mgusu anasema kutokana na njaa, wameamua kubana vipindi ili masomo muhimu yafundishwe hadi saa tano.

“Baada ya hapo, karibu robo tatu ya wanafunzi wanakuwa wamesinzia,” anaeleza Selelii.

Bi. Mariam Josphat ni muuza maandazi shuleni. Baada ya kuona mwandishi anadadisi akauliza, “Wewe ni mwandishi? Unatoka wapi?

“Hebu tupelekee salamu zetu kwa waziri mkuu. Mwambie atoe amri ya kuufungua huu mgodi maana hali zetu zimekuwa mbaya mno,” alisema akimwelekezea mwandishi.

“Nilimwona Pinda analia bungeni; akililia albino. Akijua kuwa nasi hapa tunateseka kwa sababu yake, atabadili msimamo. Andika hayo,” aliagiza Bi. Mariam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: