Pinda: La Mkapa limekushinda


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

UTETEZI wa rais mstaafu wa Benjamin Mkapa ambao ulifanywa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake, Ijumaa iliyopita, haukubaliki.

Huu unahusu hatua ya Mkapa ya kujimilikisha mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira. Endapo tutakubali utetezi uliofanywa na Pinda, bila ya kuuhoji, basi utakuwa umejenga msingi mbaya wa utawala wa sheria nchini.

Pinda anasema, “Nimesikia maoni ya wabunge wengi waliokuwa wakimtetea Mkapa, nami naungana nao kumtetea mzee huyo. Maana tujiulize, kama kweli Mkapa ni fisadi, basi tuangalie ufisadi wake uko wapi? Je, anamiliki akaunti zenye dola nje ya nchi? Ana ndege zake zinazoruka hapa nchini? Sasa ufisadi wake uko wapi?”

Kwa kauli ya Pinda, utadhania tatizo la Mkapa na Kiwira ni kuweka fedha nje ya nchi au kununua ndege. Sijui ni nani ambaye amedai kuwa Mkapa ana akaunti za dola nje ya nchi; na sikumbuki ni nani aliyedai kuwa Mkapa ana ndege zinazoruka nchini.

Na jinsi ambavyo Pinda ameapa kulishughulikia suala la Kiwira na kurudisha hisa serikalini, ni kana kwamba watu walikuwa wanalalamika hisa kutokuwa serikalini. Yote mawili si kweli. Na hivyo majibu yake na utetezi wake wa Mkapa haujajibu madai mazito dhidi ya Mkapa.

Lakini pia utetezi kuwa anamjua sana Rais Mkapa na kuwa ni mtu mwadilifu, mcha Mungu na kuwa “hadi leo anapendwa na kutambulika kimataifa kama kiongozi mwadilifu,” hauna msingi katika kujibu tuhuma.

Suala la Kiwira halihusu kama Mkapa anaenda kanisani au haendi; halihusiani kama anasali Rozari au hasali; na halihusu kama jumuiya ya kimataifa inamtambua kuwa mwadilifu au la.

Kutumia maneno hayo bungeni kwa hakika ilikuwa ni kujaribu kukwepa hoja; yaani baadala ya kujibu tuhuma unaingiza ndani mambo ambayo hayahusiani na tuhuma hizo.

Ninachosema ni kuwa licha ya serikali kutangaza kuwa hisa hizo za Kiwira zitarudishwa serikalini; bado majibu ya waziri mkuu hayakugusa na hayajagusa hata chembe tuhuma nzito zinazomhusisha Mkapa na Kiwira.

Suala la Mkapa na Kiwira linahusiana na mambo makubwa mawili ambayo yananifanya nikatae, nipinge na kukejeli utetezi dhaifu wa Pinda juu ya Mkapa.

Tatizo la kwanza kabisa la Mkapa na Kiwira ni lilelile ambalo leo hii limetumika kuwafikisha mahakamani Daniel Yona na Basil Mramba. Ni matumizi mabaya ya madaraka kwa lengo la kujinufaisha binafsi.

Rais hatakiwi kutumia madaraka yake vibaya. Kwa vile mtu ni rais, haina maana anaweza kufanya jambo lolote kwa mtu yeyote na kwa namna yoyote. Urais haumfanyi raia wa Tanzania kuwa nje ya sheria.

Akiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkapa akijua hali ya tatizo la nishati nchini, akijua kuwepo kwa mkaa wa mawe kule Kiwira na hali ya mgodi wa Kiwira, anatuhumiwa kutumia wadhifa wake pamoja na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona kujiuzia mgodi wa Kiwira.

Hapa tatizo siyo bei. Tatizo ni kuwa kama rais hakutakiwa kutumia nafasi yake kujinufaisha yeye na familia yake kwa kutumia habari au taarifa ambazo Mtanzania wa kawaida asingeweza kuzipata.

Hivyo, tatizo la kwanza ambalo Pinda hakuligusa juu ya Mkapa ni matumizi mabaya ya madaraka.

Pili, Mkapa anatuhumiwa kuvunja sheria ya Maadili ya Umma ambayo, pamoja na mabadiliko yake ya 2001 ambayo yeye aliyaridhia, vinaongoza mwenendo wa viongozi kadhaa wa umma.

Sheria iko wazi, kwamba kiongozi yeyote hatajiweka katika nafasi ambayo maslahi yake binafsi yanagongana na wajibu wake katika nafasi hiyo.

Ina maana, rais ambaye anaongoza Baraza la Mawaziri, ambapo maamuzi mbalimbali ya serikali yanachukuliwa, hatakiwi kuanzisha biashara ya aina fulani kutokana na taarifa anazozipata kwenye vikao hivyo.

Vivyo hivyo kwa Waziri wa Nishati na Madini. Hapaswi kuwa mmiliki wa kampuni ya kuzalisha umeme ambayo inaiuzia umeme serikali. Pinda hajazingatia haya katika taarifa yake.

Waziri wa Nishati na Madini wa wakati ule, Daniel Yona akijua kinachoendelea Kiwira na akiwa anatoa taarifa kwa bosi wake (Mkapa), wanadaiwa kujipatia mgodi wa Kiwira kwa bei ya chee na hivyo kulisababishia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi na kuingia kwenye mgongano wa maslahi.

Tuhuma hizi hazizimwi kwa kutuonesha kiwanja cha mpira, kutuonesha miradi mbalimbali, au kututangazia jinsi gani wazungu wanamwona Mkapa kuwa mwadilifu. Kukwepa kuzungumzia madai haya kunathibitisha jinsi gani Pinda asivyotaka kuwa mkweli na asivyotaka suala la Mkapa limalizike salama.

Pamoja na serikali kutangaza kuwa hisa za Kiwira zitarudishwa serikalini, swali ambalo halijajibiwa ni zitarudishwa vipi? Je, itabidi serikali inunue hisa hizo kutoka kwa Mkapa na wenzake?

Kama ni ndivyo, itanunua kwa misingi ya ushindani au itakuwa ni mnunuzi pekee? Kama bado Mkapa anatuhumiwa kufanya kosa la kuvunja sheria na Katiba, kwa nini serikali ikae naye kupanga jinsi ya kununua badala ya kuitaifisha?

Kama serikali itaamua kununua zile asilimia 85 kutoka kwa Mkapa na wenzake, si itakuwa imefanya kile hasa ambacho tunakipinga, ambacho ni kumpatia yeye na ndugu zake, utajiri kinyume cha sheria?

Kwa vile hakuna uwezekano wa wabunge wa CCM kumshitaki aliyekuwa mwenyekiti wao, na kwa sababu serikali ya sasa haijali sheria yanapokuja masuala ya vigogo bali mapenzi ya viongozi fulani fulani, napendekeza yafuatayo ili tulimalize hili la Kiwira bila ya kuvunja sheria wala kuhalalisha matumizi mabaya ya madaraka.

Kwanza, serikali itaifishe hisa zote za Kiwira na kuzirudisha serikalini bila kumlipa mtu hata mmoja.

Anayeona ameonewa aende mahakamani.

Pili, Mkapa aitishe mkutano wa waandishi wa habari na kukiri suala hili la Kiwira, kukiri kupotoka na kuomba radhi.

Tatu, serikali ihakikishe Kiwira hairudishwi mikononi mwa mtu yeyote binafsi ambaye ama yuko serikalini sasa hivi au amewahi kuwa serikalini miaka 15 iliyopita.

Nne, Kiwira iwe chini ya Tanesco. Mradi urudishwe serikalini bure na wale wote walioingiza fedha zao humo kinyemela wahesabike wamepata hasara ya milele.

Tano, serikali ihakikishe inalipa malimbikizo ya mishahara na malipo mengine ya watumishi wa Kiwira isipokuwa menejimenti ambayo Mkapa na wenzake ndio watakiwe kuwalipa.

Tukifanya hayo, huko tuendako, hatutaona aibu kuwazungumzia viongozi wastaafu kana kwamba walikuwa wafalme.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: