Pinda: Mtoto hatupwi


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version

BAADHI yetu tulitabiri mapema, kwamba mpasuko wa kisiasa Visiwani Zanzibar usipodhibitiwa, ungeambukiza Muungano wetu.

Sasa utabiri huu umetimia. Wazanzibari, bila kujali tofauti zao za kisisiasa, wameungana kudai taifa lao. Wanataka itamkwe kinagaubaga, kwamba "Zanzibar ni nchi."

Hakika, anayepaswa kulaumiwa katika hili ni sisi wenyewe. Kwamba wakati tunajua kuwa gonjwa hili ni kikatiba, tunataja kulitatua kisiasa!

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameendelea kufanya kosa hilo hilo. Pinda badala ya kujibu hoja, amelirudisha suala hilo kwa chama chake-Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pinda alibanwa bungeni, akitakiwa kutoa ufafanuzi wa kipi kilicho juu ya kingine, kati ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ulioridhiwa na Mabunge ya Tanganyika na Zanzibar, na kuwa Sheria ya Muungano (Act of Union) na kuzaa Katiba ya Muungano, na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.

Pinda, kama mwanasheria, anafahamu tatizo hili ni suala la kikatiba. Anajua kuwa katiba sio mali ya chama cha siasa.

Hakuna anayeweza kuhoji uhalali wa Muungano; wala anayegomba kuwapo kwake.

Kinachogomba hapa, ni aina Muungano unaotakiwa. Kinachoongeza mtafaruku zaidi ni hatua ya watetezi wa Muungano, kukataa kukiri yaliyomo katika mkataba wa Muungano na sheria ya Muungano, ambazo ndio msingi mkuu uliotakiwa kulindwa.

Profesa Issa Shivji amefafanua vizuri jambo hili. Sitaki kulirudia. Tufike mahali tukiri udhaifu uliopo kwenye muundo wa sasa na mapungufu ya Katiba yetu badala ya jazba za kisiasa.

Hizi ni enzi za nguvu ya hoja na si enzi tena za hoja ya nguvu. Ni enzi za Sayansi na Teknolojia inayoibua makosa ya nyuma na kuyarekebisha.

Nilazima tubadilike. Njia nzuri ni kukiri udhaifu, vinginevyo tutazalisha gharika ya kujitakia na tusioweza kuizuia kwa viganja vyetu.

Hatua ya Waziri Mkuu Pinda, kulikabidhi suala hili kwa CCM, ni kulikimbia tatizo. Kamwe haliwezi kupatiwa ufumbuzi wa tafsiri na wanasheria wakuu wa nchi hizi mbili.

Kwanza, tayari yule mmoja amekwishatoa msimamo wake, anasema Zanzibar ni nchi. Lakini pili, wote wawili hawana uwezo wa kutoa tafsri.

Ufumbuzi uko kwenye Katiba, ibara ya 126, inatakiwa itolewe tafsiri na Mahakama Maalum ya Kikatiba.

Tangu mwaka 1964, mambo ya Muungano yaliongezwa kutoka 11 hadi 23 bila mawasiliano na upande wa pili wa Muungano.

Hii ina maana kwamba, mmoja kati ya wabia katika ushirika huu, alijichukulia mamlaka ya upande wa pili kwa maana ya kupunguzia mamlaka ya Serikali ya Zanzibar.

Kwa sababu hii, kilio cha Wazanzibari cha nchi yao kutaka kumezwa, kilikuwa cha kweli.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya mambo yaliongezwa hayakuheshimiwa na Zanzibar, kwani iliendelea na inaendelea mpaka sasa kujifanyia mambo yake.

Kwa mfano, wakati suala la fedha za kigeni lilipofanywa kuwa jambo la Muungano mwaka 1965, Zanzibar iligoma na ikaendelea kushikilia na kutunza Akaunti ya fedha zake za kigeni.

Wapo wanaosema kwamba chimbuko la mgogoro limetokana na uamuzi wa kuongeza mambo ya Muungno kutoka 11 hadi 23, bila kufuata taratibu.

Katiba ya Muungano nayo ina mapungufu mengi yaliopaswa kuhojiwa wakati ule na sasa pia.

Kwa mfano, hadi katiba hiyo ikitungwa, Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ilikuwa ikitumika kama Katiba ya mpito ya Muungano kwa kufanyiwa marekebisho ili kuingiza mambo ya Muungano, wakati Muungano ukisubiri kupata Katiba yake.

Mwaka 1965, Katiba hiyo ilirekebishwa kwa kuingiza na kukifanya Chama Cha Tanganyika African National Union (TANU) kuwa chama pekee cha siasa nchini chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja.

Hatua hiyo inatafriwa kuwa ni ukiukwaji wa Mkataba wa Muungano, kwa sababu vyama vya siasa havikuwa mambo ya Muungano. Je ilifanyikaje?

Sheria ya Muungano Na. 22 ya mwaka 1965 iliweka utaratibu wa kutunga Katiba. Ilianza na uteuzi wa Tume ya Katiba, ambapo iliundwa baada ya Rais wa Muungano kushauriana na Rais wa Zanzibar.

Kisha kwa kushauriana na rais wa Zanzibar, Rais wa Muungano angeunda Bunge la Katiba ili kupokea mapendekezo ya Tume na kupitisha Katiba. Hili lilitakiwa kufanyika kabla ya 26 Machi, 1965.

Lengo la utaratibu huu lilikuwa ni kuruhusu ushiriki wa watu wa pande zote za Muungano katika kutoa mawazo na kutunga katiba yao.

Lakini kwa sababu zinazofahamika, Tume wala Bunge la Katiba halikuundwa wala kuitishwa, badala yake Kamati ya watu 20 ya vyama vya TANU na Afro- Shirazi Party (ASP) iliyoteuliwa kupendekeza kuunganishwa kwa vyama hivyo, ndiyo iliyogeuzwa kuwa Tume ya kupendekeza Katiba.

Vivyo hivyo, Bunge la kawaida la wakati huo liligeuzwa kuwa ndilo Bunge la kutunga Katiba, tofauti na lililokusudiwa katika Sheria ya Muungano.

Utata zaidi unaibuka. Kwamba mapendekezo ya ile iliyoitwa, "Tume ya Katiba" hayakuwasilishwa kwenye "Bunge ka Katiba" kama ilivyotakiwa na Sheria ya Muungano, badala yake yaliwasilishwa kwenye Halmashauri Kuu (NEC) mpya ya CCM.

Na pale mapendekezo hayo yalipofikishwa kwenye "Bunge la Katiba," waziri mkuu wa wakati huo, aliwaambia wajumbe waziwazi kwamba kwa kuwa, rasimu ya katiba hiyo tayari ilikuwa imepitishwa na NEC hawakuwa na sabau tena ya kuijadili bali kuipitisha tu bila kuhoji.

Tatizo lililopo mbele yetu sio dalili za sasa za ugonjwa wa Muungano, au kwa Wazanzibar kudai waitwe ni "nchi," bali tatizo ni ugonjwa wa zamani, yaani muundo wa Muungano.

Tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa kutibu tu dalili za ugonjwa, bali tunatakiwa kuuvalia njuga ugonjwa wenyewe kwa kuangalia nyuma.

Huko ndiko tutaona muundo wa Muungano uliokusudiwa ni upi. Kama una matatizo, tujadiliane upya kwa njia ya kidemokrasia na kwa haki, badala ya kujaribu kuuwa au kuubakiza kwa mbinu za ujanja wa porini na jazba zisizojenga.

Iliwezekana kutumia mbinu hizi enzi za chama kimoja, lakini sio leo. Tunawauliza akina Ally Juma Shamuhuna, Raza na wengine wa aina yao wanaothamini jazba, walikuwa wapi wakati Rais Aboud Jumbe Mwinyi alipopigwa buti mwaka 1984 kwa kutumia haki yake ya Kikatiba kutaka kutolewa ufafanuzi juu ya Muundo sahihi wa Muungano?

Sakata la muundo wa Muungano lilijitokeza hata wakati wa Tume ya Jaji Nyalali. Kwa mtazamo wa wakati huo (1992) na pengine hadi sasa, ilipendekeza kuwapo kwa Muungano wa serikali tatu. Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na serikali ya Shirikisho.

Lakini, kama kawaida, CCM na serikali yake, badala ya kulipa uzito pendekezo hilo, walilitupilia mbali bila udadisi makini. Wakaendelea na muundo wa serikali mbili, wakisema wanaelekea kwenye serikali moja.

Pengine ni kwa sababu hii kwamba Waziri Mkuu Pinda, licha ya kuelewa udhaifu na mapungufu yote ya Muungano, anaogopa kutenda ile "dhambi kuu."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: