Pinda naye ‘Kassim wa Matumizi’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

OFISI ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda imetumia zaidi ya Sh. 174.5 milioni kwa kile ambacho kimeelezwa kuwa “mchakato wa kufanikisha bajeti yake,” MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limeona, idara ya sera na mipango (DPP) ya ofisi ya waziri mkuu imetumia Sh. 49 milioni kwa kile kilichoitwa, “maandalizi ya bajeti.”

Idara nyingine iliyopewa fedha za maandalizi ya bajeti, ni idara ya elimu ambayo imechotewa Sh. 14,925,000 zilizotumika kwa ajili ya posho za wafanyakazi ambao walilipwa Sh. 12,025,000.

Haikuelezwa wafanyakazi hao walikuwa wangapi na walilipwa kila mmoja kiasi gani. Kiasi kingine cha Sh. 12,025,000 kililipwa kama gharama za mafuta.

Matumizi haya yameelezwa kuwa ya kulipa posho za wafanyakazi walioshiriki kwenye maandalizi ya bajeti hiyo (Sh. 15,655,000); kuchapishia vitabu vya hotuba ya bajeti (Sh. 6,400,000); chakula cha wafanyakazi (Sh. 20,000,000) na uchapishaji bajeti katika gazeti (Sh. 7 milioni).

Mamilioni mengine yamelipwa katika idara ya DSC ambapo nyaraka zinaonyesha idara hiyo imelipwa Sh. 4 milioni kwa ajili ya posho, Sh. 1,140 kwa ajili ya mafuta na Sh. 1.2 milioni kwa ajili ya vifaa vya ofisi.

Idara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (DRA) imetunia Sh. 17.9 milioni.

Taarifa zinaonyesha Sh. 21,810,000 zilitumika kulipa posho wafanyakazi saba wa idara hiyo; Sh. 17,980,000 zikiwa gharama za kuendesha kikao cha waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu na wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kilichofanyika 18 Mei 2011 na Sh. 1.6 milioni zikiwa gharama ya mafuta ya magari mawili.

Haijafahamika mara moja magari hayo yalitumika kwa kazi ipi; yalikodishwa kwa nani, au yalitoka wapi na kwenda wapi.

Nako kwenye idara ya serikali za mitaa kumepelekwa Sh. 10,755,000 ambazo nyaraka zinaonyesha zimetumika kulipia posho wafanyakazi wake watano.

Idara ya DICT imepewa Sh. 26 milioni, huku mhasibu mkuu akilipwa Sh.5.6 milioni kwa ajili ya kulipa posho za wafanyakazi watano. Kama fedha hizi zimegawiwa kwa kiwango sawa, kila mfanyakazi atakuwa amelipwa zaidi ya Sh. 1 milioni.

Kwenye idara ya utawala na rasilimali watu (DAHRM), serikali imelipa Sh. 20 milioni. Mamilioni hayo yamelipwa kama posho za wafanyakazi 12 (Sh.11.7 milioni), viburudisho (Sh. 1,800,000), vifaa vya ofisini (Sh. 600,000), gharama za mafuta (Sh. 2,900,000) na “chakula cha jioni” (Sh. 3 milioni).

Haijaweza kufahamika mara moja kwa nini serikali imetumia mamilioni hayo ya fedha kulipia posho za wafanyakazi wake, chakula, usafiri na mafuta ya magari, wakati ambapo wafanyakazi hao ni waajiri wa serikali na wamelipwa posho za kujikumu na nauli.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja mwezi mmoja baada ya wabunge wa CHADEMA kutaka serikali kufuta posho za wafanyakazi wa umma wakiwamo wabunge kwa kile kilichoelezwa, “kuelekeza fedha hizo katika kazi za maendeleo.”

Aidha, kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki mbili baada ya mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo kumtuhumu bungeni katibu mkuu wizara ya nishati na madini, David Jairo kuchangisha fedha “kugharamia bajeti.”

Shelukindo aliliambia Bunge kuwa Jairo amechangisha taasisi zilizoko chini ya ofisi yake karibu Sh. 1 bilioni kwa matumizi ambayo hayajaweza kuelekezwa, jambo ambalo lilimfanya Pinda kuonyesha masikitiko yake hadi kutaka kumfuta kazi mteule huyo wa rais.

Kwa mujibu wa dokezo lililotoka kwa ADPP, T. Bangadanshwa tarehe 21 Julai 2011 kwenda kwa Fanuel Mbonde, mchanganuo wa fedha hizo unaonyesha Sh. 15,665,000 zililipwa kwa ajili ya posho ya wafanyakazi, Sh. 6,400,000 zilitumika kuchapishia vitabu vya bajeti na Sh. 20,000,000 malipo kwa ajili ya chakula.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: