Pinda ni shokabuzoba ya serikali ya JK


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KATIKA gari kuna chombo kiitwacho shock absorber (shokabzoba); madereva mitaani wanaziita ‘shokap’. Kazi kubwa ni kuongeza mneso wa gari na kupunguza mtikisiko mkubwa likiingia kwenye mashimo mashimo au barabara mbovu.

Shokap zikiharibika mneso kwenye gari unakosekana na hivyo likiingia kwenye mashimo hudunda na kurusha sana na huweza kusababisha vifaa vingine kuharibika.

Rais Jakaya Kikwete aligundua kwamba gari (serikali) alilokuwa anaendesha halikuwa na shokap bora (Waziri mkuu madhubuti) ndiyo maana lilishindwa kuhimili katika barabara iliyojaa mashimo ya EPA na kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Mwaka 2008 Kikwete akiwa ameelemewa na shutuma dhidi ya gari lake kwamba lilikuwa linajigonga ovyo na kurusha roho za abiria (wananchi), alituliza akili mwaka 2008 akaagiza shokap mpya. Alimteua Mizengo Peter Kayanza Pinda kuwa waziri mkuu.

Pinda ametumika kama shokap mwenye jukumu kubwa la kuzuia mihemuko ya watu iliyokuwa inatikisa serikali yake katika kashfa za Meremeta/ Tangold, pamoja na madai ya Mahakama ya kadhi na Katiba mpya.

Staili ya Pinda kwanza ni kusoma hoja zinazotolewa na wananchi dhidi ya serikali, kupima uzito wake, kusoma aina ya watu wanaotoa hoja ili ajibu kulingana na kaliba yao. Pili husoma kiwango cha mhemko wa wananchi katika uwasilishaji hoja.

Halafu huingia kwenye kabati la majibu na kuchomoa anayoona yanafaa kwa wakati ule. Majibu yake huwa hayatoi ufumbuzi wa mwisho ila kuteka hoja iliyopo na pale anapokuwa amezidiwa ‘humwaga chozi’ basi.

Katika baadhi ya maeneo Pinda huwalainisha wakosoaji wa serikali kwa kukubali udhaifu au husema serikali imeliona hilo na inalitafutia ufumbuzi wa kudumu huku akitoa angalizo baadhi ya mambo huhitaji muda mrefu.

Pinda, hjajatoa ufumbuzi wa kudumu juu ya matatizo makubwa ya kifisadi yaliyoikumba serikali isipokuwa kauli njema ya matumaini.

Kwa staili hiyo Pinda amefanikiwa kupunguza kelele au kuziba kwa viganja shutuma au malalamiko. Mpaka lini?

Pinda maarufu kama Mtoto wa Mkulima amefanya kazi Ikulu hivyo anajua mambo mengi ya kiutawala, mazuri na mabaya. 

Anajua kampuni nyingi bomu zilivyoruhusiwa kama Meremeta, namna ilivyoingizwa nchini IPTL na hata mkubwa mmoja alivyojigawia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa kisingizio cha uwekezaji.

Baadaye akaingia katika siasa, akateuliwa Waziri wa nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi). Hivyo wakati inaibuka kashfa ya Richmond iliyoporomosha heshima ya gari la Kikwete hadi kumwangusha mtangulizi wake Edward Lowassa, yeye alikuwa serikalini.

Mwanasheria Pinda ndiye msaada pekee katika serikali ya Kikwete kuzima, kupoza, kulainisha mioyo ya watu waliochoshwa na ufisadi unaopaliliwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kikwete alimteua Pinda katika kipindi ambacho watu walikuwa wakihoji kama kweli mkuu huyo wa nchi ni ‘Chaguo la Mungu’ kama walivyosema maaskofu.

Pinda aliteuliwa katika kipindi ambacho shokap ya kwanza ilivunjika na kuharibika kabisa baada ya kuingia katika shimo la Richmond. Kwa mwonekano serikali iliporomoka pale.

Pinda alilainisha mioyo ya wabunge na wananchi kwa kukiri udhaifu wa serikali kiutendaji, akaahidi kufanyia kazi mapendekezo ya Bunge. Badala yake kilichofanyika ni kusafisha baadhi ya watuhumiwa, na hata waliopaswa kuadhibiwa waliachwa ufike muda wao wa kustaafu.

Kuhusu wizi wa mabilioni ya fedha uliofanywa kupitia kampuni ya Meremeta, alidai suala hilo linahusiana na siri za Jeshi la Wananchi na kwa hiyo hawezi kutoa siri hizo. Hii ni mbinu inayotumiwa na serikali kuficha, maana hata wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje ‘EPA’ ilidaiwa fedha zilichukuliwa kwa masuala ya usalama wa taifa.

Alitoa majibu hayo kunyamazisha wabunge huku akijua muundo wa kampuni hiyo haukuwa unahusiana na jeshi. Vilevile alitoa majibu hayo akijua uchimbaji wa madini si siri. Wabunge wamebaki wakijiumauma!

Kuhusu mkuu wa nchi mstaafu kujiuzuia Kiwira, Pinda alisema jamii ichunguze kwanza dhamira ya kiongozi huyo kama kweli alikuwa na nia ya ufisadi. Alisema kwa kadri anavyojua yeye zile zilikuwa juhudi za kuokoa mgodi huo!

“Kama kweli ni fisadi ilitakiwa tuone ana madege mangapi, ana mabilioni katika mabenki. Jamani, mimi naamini kwamba dhamira ya kiongozi huyu ilikuwa safi tu na kuondoa kiwingu hiki serikali inauchukua tena mgodi huo,” alisema Pinda.

Majibu hayo hayakufuta mtikisiko bungeni ila yalisaidia kufunika udadisi wa wabunge maana mpaka mtu awe na madege ndipo astahili kuitwa mhujumu uchumi.

Kikwete mwenyewe aliwapa msamaha waliokwapua mabilioni ya fedha katika EPA kwamba warejeshe ili wasishtakiwe. Hata hivyo watu wanaendelea kuhoji mpaka leo iweze wezi wa mabilioni wasamehewe wakati sheria hiyo inatumika kuwafunga wezi wa kuku?

Pinda alitumika kama shokap serikali ilipowasilisha Bajeti ya mwaka 2009/ 2010 ikifuta msamaha wa kodi ambao taasisi za dini zilikuwa zinanufaika. Ukaibuka mtikisiko mkubwa nchi nzima na bungeni.

Pinda alihangaika usiku na mchana kufanya vikao na maimam na maaskofu Dar es Salaam na Dodoma kwa lengo la kupata ufumbuzi. Alituliza hasira za watu kwa kuahidi kumshauri rais urejeshwe utaratibu wa zamani —alifanikiwa.

Kuhusu shutuma dhidi ya kauli yake kwamba aliruhusu watu wajichukulie sheria mkononi kuua wauaji wa maalbino, Pinda hakuwa na jibu wala utetezi muafaka isipokuwa kulia kwa nia ya kuonyesha uchungu wa alichokiona Mwanza.

Katikati kipindi ambacho watu wanajadili hoja nzito juu ya mustakabali wa nchi, Pinda, kwa busara na umakini, ameibuka na kuteka hoja ya katiba mpya kwa lengo la kupunguza hasira za watu dhidi ya serikali na hasa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani aliyedai suala la katiba mpya halipo na wanaotaka ni watu wa barabarani watembeao kwa miguu.

Pinda amejitokeza tena na kusema kuwa hata serikalini wanalijadili na hakuna kigugumizi akisema atamshauri Rais kuunda timu ya kushughulikia suala la katiba kama wananchi wanavyojadili.

Bila shaka Pinda amepima kasi na wingi wa maoni ya watu mashuhuri nchini, wasomi, viongozi wakuu wastaafu, majaji na wanasiasa akaona mjadala huu haukwepeki.

Amepima uzito wa hatua iliyochukuliwa na wabunge wa Chadema kumsusia Rais Kikwete alipozindua Bunge mwezi uliopita ikiwa ni njia ya kushinikiza Katiba mpya na kuundwa upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Akarejea nyuma jinsi hoja ya katiba mpya ilivyojadiliwa kwa kina mwaka jana wakati wa kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, Nyerere iliyoandaliwa na Tasisi ya Mwalimu Nyerere.

Hapa Pinda amefanya kazi yake kama shokap kutuliza munkari tu ili watu wadhani serikali yao ni sikivu. Kama serikali imeliona na inataka kulifanyia kazi Pinda ajue kinachojadiliwa, kupendekezwa na kuhitajika kwa sasa ni KATIBA MPYA, siyo VIRAKA kama anavyodai.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: