Pole Kanumba, lakini...


Elijah Kitosi's picture

Na Elijah Kitosi - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Steven Kanumba

MENGI yamesemwa kuhusu kilichotokea ndani ya onyesho la 'Big Brother Africa Revolution' na hasa mwaliko aliopata wa mwigizaji kutoka Tanzania, Steven Kanumba 'The Great'.

Tayari ametoa masikitiko yake kwa kile alichokuiita kashfa kutoka kwa Watanzania mbalimbali waliotoa maoni yao.

Kanumba aliingia kwenye jumba hilo kama mmoja wa wasanii wanne kutoka Afrika waliokaa kwa saa 24. Yeye hakuwa mshiriki wa Big Brother.

Mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na kulakiwa na mamia wa mashabiki wake na 'wazalendo' wachache, Kanumba alionekana mwenye furaha kubwa lakini iliyokuwa na fadhaa.

Naamini kwa upeo wake, hasa kutokana na kuwepo kwenye sanaa kwa muda mrefu, Kanumba alipata picha kwamba lazima kutakuwa na 'zengwe'.

Bila shaka hakuamini kulakiwa na mashabiki wake wachache ikilinganishwa na kina la Latoya, Mwisho Mwampamba Mwisho Mwampamba (Namba 2) na Richard Bezuidenhou (Mshindi wa mwaka 2008).

Baada ya yote hayo, tujadili sababu za msingi kuhusu chanzo cha maneno yote yaliyozagaa na shutuma kali kutoka kwa Kanumba.

Kwanza kabisa napenda kutoa msimamo wangu kwamba naungana kwa kiasi kidogo na maneno yaliyozagaa yanayorejea kile kilichotokea kwenye jumba la Big Brother Africa.

Sikubaliani hata kidogo kwamba suala la Kanumba limeongezwa chumvi pengine ama kwa kutaka kumchafua Kanumba au kuweka msisimko kwa kile kinachosemwa.

Nakubaliana na uhalisia wa kile kilichotokea kwenye uzinduzi wa shindano hilo la Big Brother Africa, si kwa kutaka kumsafisha Kanumba bali kujaribu kumjenga ili aweze kufika mbali.

Kanumba hakuzungumza Kiingereza kizuri kama ambavyo mwenyewe alikiri katika kujibu shutuma zilizozagaa mitaani.

Katika kujibu mapigo, akisema Kiingereza ni lugha aliyojifunza shuleni na ni lugha yake ya tatu ya mawasiliano baada ya Kiswahili na Kisukuma.

Pili, Kanumba aliendelea kufafanua kuwa Kiingereza hakikuwa kigezo cha kuteuliwa ama kushiriki kwenye Shindano hilo la Big Brother Africa jambo ambalo nakubaliana naye.

Mwisho alimalizia kwa kukanusha vikali suala la kwamba yeye alivaa 'topu' badala ya shati kama ilivyovumishwa mitaani.

Kwa haya yote, Kanumba ameonyesha kwamba hajakomaa hivyo hajiamini kama yeye ni 'The Great'.

Unapokuwa mtu maarufu, jambo moja kuu ni kukukabili changamoto na kukubali kukosolewa kama ambavyo unazipokea sifa kem kem mambo yanapokunyookea.

Jambo hili sijaliona kwa Kanumba. Kwa kiasi kikubwa Kanumba 'alichemsha' katika saa zake 24 za kukaa ndani ya jumba la Big Brother Africa. Kuanzia maisha ya kawaida, mavazi na hata lugha.

Nilipofuatilia kwa makini niligundua kwamba Kanumba alichemsha tangu dakika za mwanzo tu za kukaa kwenye jumba lile. Yaani alikuwa akiwaogopa washiriki wengine.

Muda mwingi aliutumia kuwakimbia wenzake kama si kushangaa na mara nyingine kusaidia wenzake kucheka kwa sauti kubwa kama afanyavyo kwenye filamu zake. Pengine alijua upungufu wake.

Kuhusu mavazi, Kanumba hakuvaa 'topu' kama ilivyovumishwa, lakini sitaki kufuta kauli kwamba 'alichemsha' kwa kuvaa shati lake la 'pink' ambalo baadaye aliligawa kwa mshiriki mwenzake kama ukumbusho.

Naweza kusema kwamba Kanumba hakuwa na mshauri na kama alikuwepo basi alizembea wajibu wake.

Vile vile Kanumba alichemsha kwa kushindwa kuitangaza nchi yake japo yeye alitamani kupata mapokezi ya kitaifa.

Alichotakiwa kufanya, pengine iwe fundisho kwa wengine watakaopata nafasi kama hii ni haya. Kwenda na mavazi ya Kitanzania ama pengine hata fulana zenye bendera ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya kunadi nchi.

Dosari nyingine niliyogundua kwa Kanumba ni kushindwa kwake kutofautisha 'shooting' ya filamu na kuonyesha maisha yako halisi ya kila siku, yaani jinsi unavyoishi huko utokako kama 'hobbies' na vipaji mbalimbali ulivyonavyo.

Wakati wenzake wakionekana kufanya usafi hapa na pale ndani wakati wa asubuhi, huku wengine wakiandaa kifungua kinywa alimradi wako 'bize', Kanumba alikuwa nje ya jengo kwa shughuli ambazo labda atatueleza baada ya kusoma makala hii.

Hata alipoingia ndani, Kanumba hakuonekana mwenye kufikiria chochote zaidi ya kwenda moja kwa moja kwenye jokofu na kumimina juisi kwenye glasi yake na kisha kuelekea nje taratibu kama anafanya 'shooting' ya filamu fulani.

Ikumbukwe hayo yote aliyafanya bila kutamka chochote. Kama si kuwakwepa wenzake ni nini? Labda jibu analo mwenyewe.

Kipindi ambacho wenzake wanaonyesha vipaji kwa kuruka sarakasi na baadhi yao kuimba, Kanumba yeye alitumia muda huo kujilaza kwenye sofa akiwatazama tu.

Baada ya muda alionekana kama kupitiwa na usingizi. Sikumuelewa vizuri japo tafsiri ya haraka niliyoipata pale ni kwamba labda kipaji chake kililala.

Kuna mengi aliyochemka 'The Great' Kanumba, japo sitaki kuzama kwenye suala la lugha ya Kiingereza kwa kuwa hata mimi si mtaalamu wa lugha.

Nadhani hilo tuwaachie wataalamu watatoa maksi kwa kadri ya utaalamu wao.

Lakini yote yaliyosemwa kuhusu Kanumba yawe ya kweli au ni ya uzushi alitakiwa kuyapokea na kuwaachia mashabiki na mashuhuda kufanya kazi ya kuchambua 'pumba na mchele'. Zote hizo kwangu ni changamoto zenye lengo la kumpandisha matawi ya juu.

Napenda kumpa pole Kanumba na kwamba kamwe hawezi kuwa msanii maarufu bila kupitia hali anayopitia sasa. Hili lichukuliwe kama somo kwa wasanii wengine wenye ndoto za kutaka kufikia ngazi ya kimataifa.

Wakati umefika sasa kwa wasanii wetu kuondoa hisia potofu za kujiweka mahali ambapo hawajafikia. Vyuo vipo vingi mno ambavyo vinafundisha lugha mbalimbali za kimataifa, pesa wanapata lakini kila kukicha kazi kubadili wasichana na kuwazia kununua magari ya kifahari.

Tukumbuke usemi wa wahenga 'Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji kichwani'. Kanumba kaanza, nani atafuatia? Pole Kanumba kwa kuumizwa na yote, lakini hiyo ndio dawa ya mapungufu uliyonayo. Rafiki wa kweli ni yule anayekueleza upungufu wako!

0
No votes yet