Polisi inawataka nini Wazanzibari?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KAMA wapo Watanzania waliobisha ushiriki kamili wa Jeshi la Polisi katika kufanya uhalifu dhidi ya binadamu Zanzibar, kwa matukio ya 26-27 Mei, basi watafakari matukio mapya ya 17 Juni.

Katika matukio yale, askari wa polisi walipewa silaha na kusukumiza risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi. Wakashambulia ofisi za mawakili, gari za wananchi na nyumba za viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI).

Ni matukio ambayo hadi leo, polisi haijayatolea taarifa licha ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi.

Wananchi walipoteza mali zao: gari zilizoharibiwa kwa mabomu; na Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) wanaolalamikia kitendo cha polisi kuteketeza kwa mabomu ofisi za wanachama wao zilizoko Amani.

Bado Polisi haijaeleza chochote kuhusu vitendo vyao hivyo vilivyoonyesha dhahiri kuwageuka wananchi ambao kwa mujibu wa sheria na utendaji wa jeshi hilo, wanapaswa kuwalinda wao kama binadamu pamoja na mali zao.

Mpaka hapo, picha iliyojengwa kuhusu matukio hayo, ni kwamba Uamsho ndio walihusika kuhujumu mali za wananchi. Ni Uamsho pia wanaotajwa kuchoma makanisa wawili, lile la Assemblies of God (TAG) la Kariakoo na jingine la Mwanakwerekwe.

Ni aibu kuwa Polisi walichosema katika kadhia yote ile, ni hicho tu. Kwa bahati mbaya wanaoelewa dhamira mbaya za jeshi hili wanajua upi mchele wa kuchukua, na zipi pumba za kupuuza.

Kwa kuwa ni wao waliolikoroga, wataendelea kulinywa wao wenyewe. Wanasubiriwa wakatoe ushahidi wa tuhuma zao dhidi ya Uamsho.

Lakini, kama vile matukio hayo ni madogo na ya kuzua na ambayo wanaamini hayathibitishi vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu, Jeshi la Polisi likaingia tena katika utendaji wa ovyo wiki tatu tu baadaye – tarehe 17 Juni.

Polisi wake wenye silaha walikatiza msafara mrefu wa gari, pikipiki na vespa wa wafuasi wa Uamsho waliokuwa wakienda kijiji cha Donge ambako taasisi hiyo iliandaa mhadhara wa kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano.

Mhadhara huo uliokuwa umeruhusiwa kwa mujibu wa sheria, ulisimamishwa eneo la Mahonda, Msikiti wa Ijumaa, mita 100 hivi kutoka kilipo kituo cha Polisi Mahonda.

Mpaka wanafanikiwa kutawanya wafuasi wa Uamsho kwa mabomu ya machozi, risasi za mipira na marungu, watu kadhaa waliachwa wameumia na mali nyingi kuharibiwa.

Polisi, wakijua kuwa Uamsho wana vibali vyote vya kufanya mhadhara msikitini Donge Pwani, walijipanga baina ya msikiti wa Ijumaa na kituo cha polisi, wakataka wana Uamsho warudi mjini.

Mhadhara umekusudiwa kufanyika Donge, Polisi wanazuia msafara Mahonda, mwanzo wa jimbo la Donge, ambalo wanasiasa wanaojifanya wafalme, wanataka jimbo hilo liwe bikira kisiasa pamoja na mfumo wa vyama vingi kuishi kwa mwaka wa 20 sasa.

Polisi wanajua Uamsho hawajavunja sheria, wana umma mkubwa wa watu unawafuata nyuma na kila waendako kuhadhir, kuwazuia katikati ya safari yao ni kuwachochea wakasirike.

Wana Uamsho wakasita. Wakashuka kwenye gari zao na vyombo vyao vingine. Wakabaki hapo kusubiri viongozi wao waje kutoa uamuzi. Kwa kuwa pale waliposimamishwa na polisi, pembeni kuna msikiti mkubwa, wakaamua baadhi yao kuingia msikitini kwa ajili ya sala na dua.

Viongozi walipofika Mahonda, na kupata taarifa ya kilichotokea na kinachoendelea, nao wakaamua kushuka. Wakawafuata viongozi wa polisi ili kujadiliana nao. Ndipo wanapewa taarifa ya amri ya mkuu wa mkoa kuzuia mhadhara Donge.

Lahaula, kufa hakuna breki. Palepale milio ya risasi za mipira na mabomu ya machozi ikaanza kurindima. Askari wakaingia msikitini bila ya kuvua viatu – hatua ya kunajisi msikiti. Wakapiga watu na kuwatupia matusi.

Mtu mmoja waliyemkuta chooni akijisaidia, alitukanwa kwa matusi ya nguoni. Akalazimishwa kutoka na kupita katikati ya msikiti bila ya kunawa au kusafisha miguu yake; huku akisindikizwa na askari ambaye naye hakuvua viatu vyake ambavyo wakati huu vilikuwa vimenasa uchafu.

Polisi wakaingia upande wa wanawake na kuwapiga huku wakiwavua nguo na kuwatusi na kuwadhalilisha. Ni matendo yaliyoonyesha uchokozi wa dhahiri dhidi ya dini.

Kuthibitisha kuwa polisi walishapanga ubaya, walisasambua mitaa ya Mahonda wanamokaa raia na kupita wakipiga wanaume huku wakiwavua nguo wanawake.

Hawakuchoka. Polisi wengine walitumwa kwenda hadi Donge ambako mhadhara ungefanyika na kupiga watu hata wale ambao walikutwa wakizungumza barazani kwao. Watu wazima nao hawakusalimika. Walipigwa na kutukanwa.

Polisi hawakuchoka. Walizunguka miji Mkokotoni, Kivunge, Mkwajuni, Gamba na Chaani. Mote humo wakipiga risasi za mipira na mabomu ya machozi. Wakitukana watu wazima wanaume na wanawake.

Sasa mhadhara ulikuwa umepangwa kufanyika Donge, vyereje polisi washambulie wananchi hata vijiji vingine hivyo? Ndio kule kupanga ubaya na uhalifu dhidi ya binadamu.

Leo, idadi ya watu wapatao 40 wanatajwa kuwa wanauguza majeraha ya risasi, mabomu na marungu. Wengi wengine wameumizwa kwa mateke.

Haji Khatib Ali wa Mahonda amechakazwa mguu kwa risasi na mzee Thabit Shaka wa Fukuchani amechakazwa tako kwa bomu.

Askari walimpiga mtu mwingine lakini risasi ikaduru ilipokutana na simu iliyokuwa kwenye mfuko wa suruali na kunusuru kumchakaza paja. Simu hiyo ilipasuka na kusambaratika.

Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu. Ni uchokozi na uchochezi dhidi ya akili za wananchi wema wanaoipenda amani, wanaotii viongozi wa serikali yao ya umoja wa kitaifa.

Vitendo vya polisi vinasikitisha. Na athari zake ni kupandikiza uhasama kati ya askari na raia. Kuna askari hawajarudi makwao tangu hapo kwa kuhofia kushughulikiwa na wananchi kwa kuwa wameonekana wakipiga watu na kuripua kwa mabomu vespa na pikipiki zao.

Pia walipondaponda baiskeli za wananchi wanaoishi Mahonda waliokuwa wakisubiri nao kuondoka na msafara kutoka Mahonda kwenda Donge. Huko ni kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu. Hawi radhi kwa mambo haya.

Tatizo kubwa la Jeshi la Polisi sasa ni kujichukulia sheria mkononi na kushambulia raia na kuharibu mali zao. Tatizo jingine ni kule kufanya yote hayo, halafu wakaeneza uongo kwa ulimwengu kuwa wanadhibiti wakorofi.

Katika matendo hayo, ni nani hasa mkorofi? Polisi wameamua kuasi raia.

Sasa watu wa Donge wanauliza: Wao ni nchi gani? Inatumia sheria zilizo tofauti na sehemu nyingine ya nchi yao au wao wana taifa jingine?

Wanayauliza maswali haya kwa viongozi wao – mwakilishi Ali Juma Shamhuna, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Polisi wanalia sasa maana shutuma zote zimewaelekea.

0
No votes yet