Polisi ishike wauaji haraka


editor's picture

Na editor - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI imetakiwa kukamata wahusika halisi wa mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge na dreva wa teksi ili wafikishwe mahakamani.

Huo ndio ujumbe muhimu uliotolewa na Jaji Salum Massati wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, wakati akisoma hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikikabili maofisa wa jeshi la polisi.

Jaji Massati alitoa ujumbe huo akiridhika kwamba kadri alivyosikiliza ushahidi na baada ya kuutathmini, ameridhika kuwa serikali imeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya maofisa hao wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Abdallah Zombe.

Hii ni fedheha serikali kubainika imepeleka mahakamani watu wasiohusika na mauaji.

Kinachosumbua zaidi katika kadhia hii, ni gharama zilizotumika kufungua kesi, kukusanya ushahidi na kuuwasilisha mahakamani. Mchakato huu umekula fedha nyingi za umma.

Sasa kutambua kuwa kumbe serikali ilikuwa inazunguka mbuyu tu, inasikitisha. Si uongo kwamba nje ya kizimba cha mahakama kuna mtu au watu wanatanua wakati ndio walioua wafanyabiashara.

Zipo taarifa kuwa mmoja wao baada ya mauaji na aliposikia kuna uchunguzi umeanza ili kutafuta ukweli wa tukio la kuua raia, alisafiri hadi Zanzibar iliko familia yake na kutumia isivyo kawaida yake.

Mwisho wa matanuzi yake, aliaga ndugu na jamaa zake na kutokomea bila kueleza kwa uhakika amepanga safari ya sehemu gani.

Jina la askari huyu limetajwa wakati kesi ya akina ACP Zombe ikirindima mahakamani. Kwa vipi tusijenge mashaka kwamba ni kweli "muuaji au wauaji" hawakukamatwa?

Sasa, baada ya ujumbe wa mahakama kwa serikali, hatutarajii kuwa serikali itaziba masikio na kufumba macho na ikakata rufaa kupinga hukumu ya Jaji Massati, ingawa ina haki ya kufanya hivyo maana mkondo wa sheria unaruhusu.

Badala yake, tungependa kazi ianze sasa ya kukamata "muuaji" au "wauaji" hao na kuwafikisha mahakamani. Tunatoa rai hii kwa sababu inasadikika wanajulikana kwa majina na tunaamini polisi ina uwezo wa kuwafikia popote walipo.

Mara kadhaa viongozi wakubwa wa kiserikali, wakiwemo wa polisi, wamesikika wakisema hadharani serikali ina mkono mrefu ambao waweza kumfikia yeyote akitakiwa. Kwa hili, tunataka serikali itake sasa.

Ni kwa serikali kuchukua hatua muhimu hiyo tu ndipo itasalimika na shutuma zilizoanza kutolewa na wananchi kwamba imedanganya Watanzania na ulimwengu kwa kushika wasohusika.

0
No votes yet