Polisi sasa wageuka chinjachinja


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version

TAKWIMU zilizokusanywa na kambi ya upinzani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zinazonyesha mauaji ya raia wasio na hatia wakiwa mikononi mwa polisi yameendelea kuongezeka.

Matukio yaliyorekodiwa kwa kumbukumbu za baadaye yanaonyesha mwaka 2008, watu watano waliouawa na polisi; mwaka 2009 watu 15 na mwaka 2010 waliouawa walifikia 52.

Taarifa ya Mwenendo wa Haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2010 ndiyo imetumiwa na upinzani katika ripoti yao.

Katika kipindi cha miezi mitatu mwaka 2011, kuanzia Januari hadi Mei, tayari watu tisa (9) waliuawa na polisi katika eneo moja tu la Nyamongo, wilayani Tarime mkoa wa Mara. Miili ya watu hao waliouawa na polisi ilitupwa barabarani na kutelekezwa.

Tukio maarufu la mauaji ni lililofanywa na polisi ni la 5 Januari 2011 ambapo  watu watatu – Denis Michael, Ismail Omary na Paul Njuguna Kaiyele waliuawa kwa risasi na wengine 21 kujeruhiwa vibaya waliposhiriki maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mjini Arusha.

Tarehe 16 Mei 2011, polisi waliua watu watano katika eneo la Mgodi wa North Mara wilayani Tarime ambao unamilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold.

Kutokana na mauaji hayo, idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo tangu mwaka 2009 hadi Juni 2011 ilifika 34.   Kana kwamba hiyo haitoshi, tarehe 9 Juni, 2011 kijana Nyaitore mkazi wa Nyangoto alipigwa risasi ya bega na polisi wa mgodi na kulazwa hospitali ya Sungusungu.

Kwingineko huko Nachingwea, Mei, 2011 katika kijiji cha Namanga, askari wa wanyama pori walimpiga risasi kwenye miguu yote   Juma James (27). Wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya, kijana mmoja aliuawa kwa risasi eneo la Ubaruku.

Tarehe 28 Mei 2011  polisi walimuua Juma Saidi na kujeruhi wengine kadhaa katika kijiji cha Usinge, wilayani Urambo mkoa wa Tabora.

Kabla ya kufanya mauaji hayo, polisi walitembeza kipigo kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Shela na wenzake tarehe 26 Mei 2011.

Tarehe Aprili 2011, mkazi wa kijiji cha Mwanza Buriga kata ya Kukirango wilaya ya Musoma vijijini, Mwabia Zome (40) aliuawa kwa kupigwa risasi chini ya titi la kushoto na askari magereza wa gereza la Kiabakari.

Mnamo tarehe 5 Februari 2011 askari wa Wanyama Pori katika Hifadhi ya Selous waliua watu wawili na kujeruhi mmoja wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani. Waliokufa ni Hamisi Boy na Mohamed Suta huku Mohamed Kigwiso akiachwa anauguza majeraha.

Zipo taarifa kuwa askari wilayani Kisarawe waliua raia na miili yao ikatupwa mtoni ili iliwe na mamba. Majina ya waliokumbwa na ukatili huo ni Majengo, Mohamed Kibavu, Adamu Feruzi, Semeni Abdala Kube, Hemed Kassim, Mzee Hussein, Ramadhani Mgeto na Bwana Mkala.

Taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu 2011 ukurasa wa 17 na 18 kipengele cha 2.1.2, inaonyesha kwamba kuanzia Januari hadi Desemba takriban watu 25 walifia mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa ulinzi. Vilevile, matukio hayo yaliwaacha zaidi ya watu 50 wakiwa na majeraha.

Walengwa wengine ni wanasiasa. Tarehe 28 Mei 011 Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Magdalena Sakaya na viongozi wengine walitiwa mahabusu moja wanaume na wanawake na ‘wakanyimwa’ dhamana.

Sakaya pamoja na wenzake 10, walipewa masharti magumu ya dhamana, na waliposhindwa walirudishwa mahabusu ambako walikaa kwa siku 21.

Takriban viongozi wote wakuu wa CHADEMA wana kesi walizobambikiwa na polisi kama vile kufanya mikutano bila kibali au kuhutubia hata baada ya kumalizika muda uliopangwa. Lengo la kesi hizi ni kuwakosesha raha ili wasifanye kazi zao kwa umakini.

Serikali ya CCM imekuwa ikitumia mbinu hizi tangu mwaka 1992 uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi. CCM hutumia polisi kukandamiza upinzani usiibuke na kunawiri.

Kuna wakati polisi wanahusika katika kupiga, kuvuruga mikutano na kutesa na wakati mwingine polisi hukaa kando wakishuhudia au kusimamia wafuasi wa CCM wakiwapiga wapinzani.

Mathalani polisi wametumika hivi karibuni kumekuwa na manyanyaso na mauaji na wafuasi wa upinzani bila polisi kuchukua hatua.

Wabunge wawili wa CHADEMA, Highness Kiwia wa  Ilemelela na Salvatory Machemli wa Ukerewe walikatwa mapanga wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Kirumba, Ilemela mkoani Mwanza huku polisi wakizuia magari ya wabunge hao wasikimbie.

Waliotembeza mkong’oto huo na kuwajeruhi vibaya wabunge hao ni wafuasi wa CCM. Ushahidi mwingine ni manyanyaso wanayofanyiwa wafuasi wa CHADEMA katika wilaya ya Kilosa.

Katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, katika kijiji cha Bermi wilayani Babati na baadhi ya maeneo ya Meatu wamebambikiwa kesi mbalimbali.

Katika uchaguzi mdogo za Igunga mkoani Tabora, polisi hawakutaka kufuatilia waliomuua kada wa CHADEMA, Mbwana Masoud; na hata katika Arumeru Mashariki, polisi walichukua hatua za kufuatilia wauaji wa Msafiri Mbwambo baada ya CHADEMA kuiapiza polisi.

Vilevile polisi walisuasua kufuatilia na kuwakamata wafuasi wa CCM waliovamia na kucharanga mapanga wafuasi wa CHADEMA katika mkutano ulioandaliwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Hata hukumu za mahakama ni za kibaguzi. Mathalani Tundu Lisu amezuiwa kufika Tarime kana kwamba ni mhalifu wa kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi ana kazi ya kurekebisha rekodi hiyo, lakini kwa vile naye ni zao la CCM, hatarajiwi kufuta rekodi hii chafu.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)