Polisi waache ushabiki


editor's picture

Na editor - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MARA baada ya kuanza rasmi kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, tulitoa angalizo kwa vyombo vya dola vijipange vilivyo ili kuhakikisha vinalinda usalama wa watu wakati wa kampeni.

Vilevile tulitoa rai kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha wanasimamia kanuni na taratibu usiwepo ukiukwaji wakati wa kampeni.

Tulitoa angalizo hilo tukijua wazi kuwa vyombo hivyo ndivyo vilivyopewa dhamana kuhakikisha wagombea wanasafiri na kuwafikia wapigakura kwa uhuru na pia wanamwaga sera bila kuvunja sheria.

Katika kipindi chote cha kampeni, polisi ni muhimu zaidi kwani ndio wanapaswa kuhakikisha unakuwepo usalama wa watu wanaohudhuria mikutano hiyo.

Polisi ndio wanapaswa kujipanga kuweka ulinzi katika barabara wanazopita wanapokwenda kwenye viwanja vya mikutano, wanapokuwa kwenye mikutano hiyo na wanaporudi nyumbani.

Lakini insikitisha kusikia kwamba, baada ya kampeni kuanza vizuri na wananchi kuonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa kuhudhuria mikutano, kusikiliza sera na kuondoka bila kusababisha fujo, polisi wa mjini Mwanza, kwa sababu wanazozijua wao walivamia mkutano na kutaka kuutwanga mabomu wiki iliyopita.

Ripoti mbalimbali kutoka Mwanza zinaonyesha kuwa maelefu ya wananchi waliohudhuria mkutano ule wa kampeni wa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawakufanya fujo.

Lakini polisi, kwa sababu wanazozijua wao, badala ya kuongoza msafara wa watu hao, waligeuka na kutaka kuzusha vurugu ili wapate sababu ya kupiga mabomu ya kutoa machozi.

Tunajua kwamba polisi bado wanasumbuliwa na itikadi za siasa na wanakereka kuona upinzani ukizidi kupata nguvu.

Tunapenda kuwashauri polisi kwa mara nyingine kuwa wananchi katika maeneo mbalimbali wametimiza wajibu wao wa kuhudhuria mikutano hiyo, kwa amani na kusikiliza sera kwa hamasa kubwa.

Wajibu wao ubaki kulinda usalama uliopo wa watu na mali zao na waongoze misafara ya watu wanapoondoka kwani, kwa kawaida hufika viwanjani mmoja mmoja lakini huondoka kwa makundi.

Polisi wanapotishia kuchukua virungu au wanapotishia kutumia mabomu ya kutoa machozi wajue wanawapiga wananchi wenzao, raia wema wa nchi hii, wafanyakazi, wakulima au nguvu kazi ya nchi hii.

Tunalaani vitisho vilivyotolewa na askari polisi wa jijini Mwanza kwani huo ni ukiukwaji wa wajibu wao wa kuwa walinzi wema. Tunawataka waache ushabiki na upendeleo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: