Polisi wajibu hoja za Mwakyembe


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Dk.  Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela

JESHI la Polisi nchini lina wataalam wa kutengeneza migogoro. Mgogoro mojawapo unaotokana na utaalam kama huo ni ule unaohusu matokeo ya uchunguzi wa ajali iliyompata Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela,  eneo la Ihemi, Ifunda, mkoani Iringa, 21 Mei, mwaka huu.

Mgogoro na utata wa matokeo ya uchunguzi vinajitokeza kwenye ripoti ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, James Kombe aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kuchunguza mazingira na chanzo cha ajali hiyo.

Ni vema kwamba tayari polisi wameeleza kuwa wanatazama upya ripoti yao na kuchanganua madai mazito ya Mwakyembe ili kuona la kufanya. Kwani awali Kombe alimwonya Dk. Mwakyembe kwamba asitoe kauli kuhusu ajali iliyompata.

Inakuwaje mtu aliyejikwaa kidole asipige kelele kutokana na maumivu aliyoyapata na badala yake asubiri polisi ndio wamsemee? Kwanini akatazwe kuelezea jinsi alivyojikwaa? Hivi ni vitisho.

Kombe anasema Dk. Mwakyembe asitoe kauli katika mambo ambayo hana utaalam nayo. Kuna utaalam gani kwa mtu kuelezea jinsi alivyoingiliwa na vibaka nyumbani kwake na kuporwa mali?

Vitisho vya aina hii kwa kiongozi wa wananchi kama Dk. Mwakyembe vinaweza kuwa na athari kubwa zaidi kwa wananchi wa kawaida. Wananchi wanaweza kutishika zaidi na kauli za akina afande Kombe, mithili ya vifaranga mbele ya mwewe.

Kombe anasema wakati ajali ikitokea, Dk. Mwakyembe alikuwa amesinzia. Nani anaweza kujua kama mbunge huyo alikuwa amesinzia kama si Mwakyembe mwenyewe au dereva wake?

Bila kumhoji mhusika, polisi walipata wapi taarifa ya kusinzia ambayo hata dereva wake, Joseph Msuya anaikana? Hii nini kama si uundaji mgogoro kwa kutumia visingizio vya utalaam?

Kombe anaeleza kwenye taarifa yake kwamba, kama Dk. Mwakyembe angekuwa hakulala, na kukaa kawaida, basi angepata madhara makubwa zaidi. Ati kulala kwake kumemponya. Masalale!

Katika taarifa yake ya 28 Mei mwaka huu, Dk. Mwakyembe anasema alikuwa macho. Aliona kilichokuwa kinatokea. Kombe anasema nini kuhusu hoja hii?

Kombe anasema uchunguzi wao umebaini kuwa ajali ilitokana na uzembe wa dereva Msuya. Kwamba Msuya anastahili kushitakiwa kwa makosa matatu: kuendesha gari kwa kasi, kushindwa kulimudu gari hilo na kumsababishia maumivu Mwakyembe.

Lakini Dk. Mwakyembe anahoji kwa nini Kombe na wenzake wanakimbilia kutoa uamuzi mkali wa kumshitaki dereva wake wakati hawakupewa fursa ya kusikilizwa.

Hili la polisi kutomhoji Dk. Mwakyembe linaleta utata. Ripoti ilipaswa kuwa na maelezo yake rasmi na kamili. Je, ina maana Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema, hakuwapa hadidu za rejea?

Kombe anasema ajali zinapotokea “viongozi” waviachie vyombo vinavyohusika kuchunguza, badala ya wao kugeuka kuwa wachunguzi na kuligawa taifa kwa uchunguzi wao.

Ni nani kaligawa taifa kama si ripoti inayozua maswali mengi kama hii? Kwa vyovyote vile, ripoti iliyosomwa na afande James Kombe mjini Iringa, ina walakini. Imekosa majibu ya maswali ya wengi.

Kuna maswali mengi yanayojitokeza ambayo Kombe na wenzake wameamua kuyafumbia macho na kuyazibia masikio, ama kwa makusudi au kwa sababu nyingine wanazozijua wenyewe.

Kuna jambo jingine linalijitokeza. Ni lile la dereva kusimamisha magari ili yasaidie kuwapeleka hopsitalini wakati pale kuna askari wa usalama barabarani.

Kwa jinsi ninavyofahamu, askari wa trafiki  anaposimamisha gari, ni nadra kwa dereva kupitiliza. Huweza kutokea lakini hiyo inatkuwa inatokana na kuwapo madereva wakorofi.

Ni kwa nini basi trafiki aliyekuwapo kwenye tukio hakuweza kufanikiwa kusimamisha hata gari moja, tena kwenye barabara kuu, hadi dereva wa Mwakyembe afanye juhudi za nyongeza?

Kuna maswali mengi. Mbona tumekosa kupata maelezo kuhusu dereva wa lori lililotajwa kwenye eneo la ajali? Lilikuwa likiendeshwa na nani? Kwa nini hatuelezwi kama alihojiwa?

Lilikuwa limetoka wapi na linakwenda wapi? Kwa shughuli zipi? Ni mali ya nani? Mwenye mali ana maelezo gani? Yuko wapi? Anafanya nini? Dereva yuko wapi hivi sasa? Anafanya nini? Lori liko wapi? Je, linaendelea na safari zake? Kwenda wapi? Kwa shughuli zipi?

Dk. Mwakyembe anasema, “Nina mashaka makubwa kama IGP Saidi Mwema…aliiona taarifa hiyo ya Kombe mapema kabla ya kusomwa.” Mimi pia nina shaka.

Ninayo mashaka kwa sababu ninafahamu IGP Mwema ni mtendaji mzuri. Kuna shauri lililomhusu mfanyakazi mwenzangu lililofikishwa kwake mwaka 1996. Wakati huo alikuwa ni Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kijana yule, ambaye alikuwa ni raia wa Zaire, alikuwa amekamatwa na polisi kwa madai ya kuomba rushwa. Katika maelezo yake alisingizia kuwa mabosi wake ndio waliokuwa wamemtuma kuchukua pesa.

Kwa kuwa suala hilo lilikuwa mbele ya Mwema, lilifanyiwa utafiti wa kina na kutupiliwa mbali. Isitoshe, raia huyo wa Zaire alikuwa ametoroka nchini na kurejea kwao Kisangani.

Nilifurahia jinsi alivyolighulikia suala letu kwa haki. Nilidhani tungekabiliana na mtu katili mithili ya Aldolf Hitler, kumbe ni Martin Luther King. Wakazi wa Mkoa wa Mbeya, na hasa Kyela, wanaweza kuniunga mkono.

Ninajua kamati ilikuwa na wataalam, kwani iliwahusisha maofisa wa Wizara ya Miundombinu, TANROADS, Wataalam wa Ufundi wa Magari, na daktari mmoja.

Lakini hawastahili kutumia utalaam huo kuzusha migogoro kama huu unaomhusu Dk. Mwakyembe na dereva wake. Wanatakiwa kutoa majibu kwa hoja za Dk. Mwakyembe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: