Polisi wamkamata waziri bafuni


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

POLISI mkoa wa Dar es Salaam, wameingia kwenye kashfa nyingine. Sasa wanatuhumiwa kumkamata Arcado Ntagazwa (66), mwanasiasa mashuhuri nchini akiwa mtupu bafuni, nyumbani kwake Kimara B ‘Temboni.’

Taarifa zinasema askari polisi watano wakiwa na silaha za moto, walimvamia nyumbani kwa Ntagazwa, asubuhi ya Jumatano 8 Februari 2012 na kuvunja mlango wa chumba chake kabla ya kumweka chini ya ulinzi.

Mashuhuda wa tukio hilo wanasema askari polisi wakiongozwa mkuu wa wilaya ya kipolisi ya Mbezi kwa Yusuph, wilayani Kinondoni, OC-CID Gerald, lilivuta mamia ya watu.

Mmoja wa wafanyakazi wa Ntagazwa aliyelazimishwa na polisi kuingia nao ndani alisema, “Polisi wameingia hapa kama wamekuja kukamata jambazi. Huwezi kuamini kama walikuwa wamekuja kumkamata raia, tena ambaye amewahi kuwa waziri mwandamizi serikalini.”

Anasema mara baada ya askari hao kuingia ndani, Ntagazwa alipiga kelele kwa ukali akisema “yaani unaingia ndani kuniangalia nikiwa mtupu tena naoga…  

“Yule polisi akasema, nitakutia pingu. Mzee akasema nifunge hiyo pingu kama mimi ni mhaini.”

Baadaye mzee huyo alitoka bafuni na kuvaa nguo zake, lakini aligoma kuondoka nyumbani kwa sharti la kutengenezewa mlango wake.

Mlango huo ulitengenezwa, ndipo mwanasiasa huyo, alipokubali kwenda kituoni kwani alijihakikishia chumba chake kiko salama baada ya kukifunga.

OC-CID Gerald amekiri kumkamata Ntagazwa katika mazingira hayo. Lakini alisema, “Huyu bwana alikuwa msumbufu.”

“Kwanza kuna siku mbili kabla, aliitwa kituo kikuu Dar es Salaam. Aliitikia wito, lakini baadaye alijiamulia kuondoka chini ya ulinzi. Siku hiyo ya terehe 8 Februari 2012, alifuatwa na askari tangu asubuhi saa 11 alfajiri.

“Mimi kwa cheo changu, huwa nakwenda kumkatama mtu ikibidi. Kuna askari wa kawaida na hata mgambo wanaweza kwenda kumkamata mtu. Sasa siku hiyo alipigiwa simu aamke na kwamba anahitajika kituoni. Hakutoka. Polisi walimweleza kwamba wako nje wanamsubiri hakutoka.

“Tangu saa 11, 12…saa 1 asubuhi mtu hatoki. Basi nikaenda mwenyewe na kumpitia mtendaji wa mtaa hadi nyumbani kwa huyo mzee na kugonga mlango. Hakufungua. Hivyo tukausukuma mlango kwa nguvu na kumkuta ndani.

Mara baada ya kuchukuliwa maelezo hapo kwenye kituo cha Polisi-Mbezi kwa Yusuph, Ntagazwa alipelekwa kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ambako siku hiyo alilala rumande.

“Tulimkuta anamaliza kupiga simu, kisha akaingia  bafuni. Yaani mtu anasema anaoga tangu saa 11 alfajiri. Unajua tumeingia pale ndani kama saa tatu hivi, eti muda wote anaoga. Tukaona hapana. Tukaingia ndani na kumkamata,” ameeleza.

Anasema, “Mimi nasema hata kama tungemkuta anajisaidia, tungemkamata…”

Ntagazwa ambaye alifanyakazi ya uwaziri chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi na Benjamin, amethibitisha kukamatwa na polisi.

“Pamoja na kwamba aliniomba radhi kwa vitendo alivyonifanyia, yule kijana aliniomba radhi. Nami nimesamehe. Lakini nimemwambia neno moja, sitasahau,” amesema Ntagazwa kwa sauti ya uchungu.

Ntagazwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Kibondo mkoani Kigoma kwa miaka 25 mfululizo (1980-1995), aliyeshika nafasi ya naibu waziri wa fedha kati ya 1983 hadi 1985 na baadaye kuhudumu kwa nafasi tofauti katika serikali za za awamu ya pili na tatu.

Mwaka 2011 alijiunga na Chama cha Demekrsia na Maendeleo (CHADEMA) na kugombea ubunge jimboni Muhambwe.

Akizungumzia hatua hiyo, Ntagazwa anasema, “Sikushtuka kulala ndani…kuna wengi wamelala ndani bila makosa.”

“Kuna watu wanafurahia wengine wadhalilishwe. Hili ni jambo la hatari,” alisema.

Kukamatwa kwa Ntagazwa kunatokana na deni la kuchapa fulana 5,000 walizoagiza kutoka kampuni ya Visual Storm.

Alisema, akiwa mmoja wa wadhamini wa taaisi inayofahamika kwa jina la The Registered Trustees of Social and Political Development’ (AFORD), Ntagazwa anasema wa waliagiza fulana hizo kutoka nchini China kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, kwa gharama ya sh 74 milioni.

Kazi ya michoro ‘designing’ walimpa Dk. Webhale Ntagazwa ambaye ni kijana wake wa kiume.

“Baada ya Dk. Webhale ku-design. Kazi hiyo ya tulimpa Noel Severe anayemiliki kampuni ya Visual Storm…  

“Lakini kabla ya siku ya kumbukumbu ya Nyerere kufika, michoro ya T-shirt zetu za AFORD ilitolewa katika gazeti la Mtanzania likidaiwa kuwa fulana hizo zilikuwa zinahusiana na Chama cha Jamii-CCJ (sasa CCK).

“Tukio hilo lilifanya wafadhili wetu watuite na kusitisha ufadhili wao, hali iliyotufanya tushindwe kuwalipa watengeneza fulana kwa wakati,” anasema.

Akasema walichofanya AFORD ni kutoa taarifa polisi kwa hati RB No. CD/RB/882/2010 na CD/RB/335/2010 na kwa mkuu wa jeshi hilo , Inspekta Jenerali kupitia barua ya Februari 16, 2010 iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Julius Miselya.

Taarifa hiyo ilikuwa ni kulalamika kupotea kwa baadhi ya fulana zetu sambamba na magazeti kuhusika kuvunja udhamini wao, kwa taarifa isiyo ya kweli.

Kwa mujibu wa Ntagazwa, IGP Mwema aliagiza uchunguzi ufanyika chini ya wapelelezi Benett na Ernest, lakini hakuona matunda ya upelelezi wao.

Wakati AFORD wakisubiri kukamilika kwa upepelezi huo kazi hiyo walipewa wapelelezi wengine, Robert na Albogast Kashaija ambao waliwageuka, wakidai walalamikaji, Ntagazwa na Miselya ni matapeli.

Alisema wapelelezi hao walidai kuwa Ntagazwa na Miselya wamejipatia mali kwa njia ya udanganyifu, hivyo wanapaswa kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Hata hivyo, Ntagazwa hakupelewa kortini baada ya familia kuingilia kati na kufanya makubaliano ya kulipa fedha inayodaiwa na kampuni ya Visual Storm, ifikapo 27 Machi 2012.

“Kinachoshangazwa ni kwamba ninashtakiwa kama mtu binafsi wakati mimi ni mmoja wa wadhamini wa taasisi yenye uongozi wake.

“Na AFORD, inaweza kushitakiwa kwa kesi ya madai, si jinai kwa sababu kilichofanyika ni kuvunjwa kwa mkataba wa malipo.

“Sitaki kuamini kama kuhama CCM kwenda CHADEMA ndio kiini. Hapa kuna jambo ambalo polisi naona inataka kujidhalilisha kuonyesha taswira mbaya mbele ya jamii,” alisema.

Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam , Suleiman Kova alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, “Sisi tumekubaliana nao wayamalize na wakishindwa basi sheria itafuata mkondo wake.”

Severe ambaye kampuni yake iliagiza fulana hizo, alisema, “ Kwanza nipo Mbeya kikazi. Haya mambo ni ya kiofisi. Nikija Dar nitakutafuta nikueleze hasa kilichotokea. Siwezi kuyazungumza kwenye simu.”

0
No votes yet