Polisi wanajimaliza


editor's picture

Na editor - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

POLISI wameamua kufa watakavyo. Wanajimaliza kwa kushiriki kuua wananchi wasiokuwa na hatia. Ni wananchi walewale ambao kila siku Polisi inataka washirikiane na jeshi ili kufanikisha Mpango wa Polisi Jamii au ulinzi shirikishi.

Mara nyingi makamanda wa mikoa na wakubwa waliopo makao makuu Dar es Salaam hukana tuhuma kwamba askari wao wameua raia.

Utasikia kamanda wa mkoa (RPC) anasema “tunafanya uchunguzi maana taarifa nilizopata kwa wasaidizi wangu zinasema alifariki baada ya kujisikia vibaya wakati vijana wangu wanamhoji kituoni.”

Lakini, ni nadra kamanda kuja tena hadharani na kutangazia umma matokeo ya uchunguzi uliofanywa kuhusu tukio la mauaji ya raia.

Hawakufanya hivyo tukio la mauaji ya raia yaliyotokea mapema mwaka jana katika kituo cha polisi cha Mbagala.

Hata alipouawa kwa risasi kijana dereva wa teksi wa Kimara mwaka jana, hakuna taarifa iliyotolewa baada ya uchunguzi. Hatujui polisi waliotuhumiwa walihusika au vipi.

Anayekula nyama ya mtu haonji mara moja. Polisi wa kituo cha Chang’ombe, yalipo makao makuu ya mkoa wa kipolisi wa Temeke, Dar es Salaam, wamemuua Musa Juma, kijana aliyetarajia kuoa siku ya pili tu kabla ya tukio.

Kamishna Suleiman Kova anasema kijana huyo alifariki dunia baada ya kulalamika alikuwa anajisikia vibaya na kupelekwa Hospitali ya Wilaya Temeke ambako alifia.

Haiwezekani. Mtu amekamatwa mitaani au nyumbani; afikishwe kituo cha polisi na ahojiwe na polisi haohao halafu ghafla polisi waseme amefariki kwa “kujisikia vibaya.”

Ndugu wasipolalamika imepita. Bali wakilalamika na kutaka hatua za kisheria zifuatwe kuchunguza mwili wa marehemu ndugu yao, ndipo Polisi huanza kutapatapa.

Ukweli n ikwamba kwa muda mrefu sasa polisi wanashiriki kuua raia. Huko ni kuvunja sheria za nchi na za haki za msingi za binadamu. Na hakuna mtu anayeruhusiwa kuua.

Kisheria nchini petu, anayeruhusiwa kuua ni yule ambaye amethibitishwa na sheria kutekeleza adhabu ya kunyongwa ambayo mahakama ilimhukumu adhabu hiyo baada ya kumtia hatiani.

Anayeua mwenzake pasina uhalali, ni mwendawazimu. Iwapo ana akili timamu, huambiwa amechanganyikiwa.

Polisi wetu wamechanganyikiwa nao? Kwanini wanawageuka raia na kuwaua na siyo majambazi na wahalifu wengine wanaotanua?

Huu ni uovu mkubwa ambao tunataka ukomeshwe. Inspekta Jenerali Said Mwema ongoza vita vya kufuta uovu huu.

Inakera kuona walinzi wa raia na mali zao wanaua raia haohao; na ukabaini matukio hayo yanaongezeka tu.

0
No votes yet