Polisi waua kibaka, walinda wezi


Anthony Mayunga's picture

Na Anthony Mayunga - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version

JESHI la polisi linaendesha madarasa mawili makubwa. Darasa la kwanza linahusu utoaji wa mafunzo kwa jamii ili washiriki katika ulinzi wao na mali zao.

Katika darasa hili, polisi wanafundisha namna umma unavyoweza kushirikishwa kusaidia polisi kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na utulivu. Polisi wanaamini wananchi ndio walinzi wa amani na utulivu na kwamba wao hudhibiti uhalifu.

Polisi wanakwenda mpaka vijijini kutoa elimu hiyo kwa jamii ili wajue namna ya kushirikiana na polisi kubaini wahalifu na kutoa taarifa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mwasisi na msimamizi mkuu wa darasa hili, ambalo lilizinduliwa mwaka 2006 ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Said Mwema. Wakufunzi wa darasa hili ni makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini.

Darasa la pili si zuri; polisi wanafundisha ukatili kwa vitendo. Mara polisi wanapoacha darasa la Polisi Jamii, IJP Mwema na makamanda wa mikoa na wilaya husimamia darasa la ukatili dhidi ya wananchi.

Wakati polisi hufundisha kuwakamata na kuwatia ndani wezi wa kuku, polisi wameshindwa kutumia intelejensia kujua mtandao wa wizi wa fedha za umma kupitia mikataba mbalimbali.

Wakati polisi wanafundisha namna ya kuwashirikisha wananchi kubaini uhalifu, wao ni wa kwanza kufyatua risasi za moto, maji ya washawasha dhidi ya wananchi wasio na hatia. Kisa? Wameandamana.

Tumeshuhudia polisi wakigeuka kuwa wauaji wakubwa wa raia na kupora mali zao. Darasa la mauaji ya vijana watatu walioandamana kule Arusha, lilitetewa na Kamishna wa Mafunzo na Operesheni, Charles Chagonja.

Wilayani Serengeti jeshi hilo limefanikiwa kuua watu watatu kwa muda mfupi sawa na Arusha. Chagonja hakusikika akitoa visingizio vyovyote kwamba ilikuwa katika kuhami kituo kisitekwe kama walivyodai kule Arusha.

Polisi wanapofikia kukamata raia, kupiga na kuua kwa risasi za moto zawadi pekee kubwa wanayopewa ni uhamisho. Funzo linalopatikana hapa ni kwamba hiyo ni ahsante kwa weledi wa kuua.

Serengeti

Hapa Serengeti Watanzania wanataka kupata majibu ya askari waliohusika kumuua Machota James (18) Novemba 15, 2010 kwa madai aliiba kuku wa askari.

Darasa hili zuri. Kwanza hawakumkamata na kuku na pili hapakuwa na jalada lililokuwa limefunguliwa kuhusu kupotea kwa kuku. Inakuwaje walalamikaji wahusike kumsaka mtuhumiwa, kumkamata na kuhukumu kwa kumpiga hadi kuua?

Polisi wakafanya jambo jingine la ziada; wao wakapora kuku sokoni, kwa madai kuwa mtuhumiwa alikuwa akiwauzia wachuuzi hao. Hii ndiyo polisi jamii.

Unyama wote huo uliongozwa na askari mwenye cheo cha inspekta msaidizi ambaye tuzo kubwa aliyopata ni kuhamishiwa mkoa wa Manyara. Halafu polisi wadogo wakatumwa kwenda kupoza familia ya wafiwa kwa kuipa Sh. 300,000.

Hiyo ni hongo. Kama polisi wanaofundisha kukataa rushwa, wanapohonga watu waliofanyiwa unyama mkubwa kama huo, jamii itarajie nini kutoka darasa la Polisi Jamii?

Wakati wananchi wakitafakari unyama huo ambao Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz alisema anafuatilia, polisi walimuua kwa risasi Hamisi
Mhoni  wa kijiji cha Matare nyumbani kwake wakidai wanasaka majangili waliohusika kuua faru George.

Hata kabla machozi hayajakauka polisi wakamchinja kwa risasi, Chacha Mwita wa Bonchugu kwa madai ya kusaka wauaji wa faru George.

Thamani ya faru huyo, kwa mujibu wa polisi, ni kubwa kuliko uhai wa watu ndiyo maana wanasikitika faru George kuuawa na siyo kupotea kwa uhai wa raia wa nchi.

Polisi wauaji wa Bonchugu, katika utetezi wao walidai  eti alianguka aliporuka ndani ya gari ili atoroke. Kama alikuwa mhalifu iweje ndugu zake waliokamatwa naye waachiwe mara tu baada ya kufariki kwa kijana huyo?

Polisi

Kwa unyama kama huu au ukatili dhidi ya binadamu bila sababu za msingi, polisi watakuwa wanatarajia nini kama wao wenyewe hawawezi kuonyesha ubora wa Polisi Jamii?

Kama polisi wanaendelea kujipambanua kuwa si rafiki wa raia, watapata ushirikiano kutoka kwa nani kubaini wahalifu?

Mbona jamii haioni nguvu kubwa ikitumika dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni (EPA) kutoka Benki Kuu (BoT)?

Kwa nini polisi hawatumii nguvu na intelejensia kujua na kuchukulia hatua wamiliki wa kampuni za Kagoda, Deep Green zilizochota mabilioni ya shilingi kutoka EPA?

Kwa nini polisi wameshindwa kutumia intelejensia au nguvu kujua uhuni uliofanywa na viongozi wa ngazi ya juu kuingia mikataba inayohujumu uchumi kama huu wa Richmond/ Dowans unaoitoa jasho serikali?

Matukio hayo ya polisi kuua watu kwa risasi ni kati ya uhalifu unaofanywa na dola dhidi ya raia wema. Machi 29, 2010 askari mmoja wa gereza la Tabora B, alimpiga kwa risasi mhasibu wa Shule ya Sekondari Kisangura eti kwa kosa la ng’ombe wake kuingia eneo la gereza.

Mhasibu huyo alifichwa polisi bila kufika mahakamani hadi Novemba mwaka jana alipoachiwa kwa maelezo kuwa mwanasheria mkuu ameona hana kosa.

Vitendo vya polisi kufanya ukatili dhidi ya wananchi vimekuwa vikiongezeka kila siku kiasi cha kufanya darasa la Polisi Jamii kukosa maana, kuhamasisha uadui na kukosa ushirikiano.

Aidha, vitendo hivi vinathibitisha usemi kwamba kazi ya polisi ni kuua na kulinda tabaka tawala na matajiri.

Mmoja ameuawa kwa kuiba kuku wa polisi, wawili wameuawa wakati wa kusaka walioua faru, mwingine amepigwa risa kwa kosa la ng’ombe kuingia eneo lisiloruhusiwa na vijana wa CHADEMA wakauawa na makumi wengine kujeruhiwa kwa madai ya kufanya maandamano bila kibali.

Ndani ya darasa la Polisi Jamii, polisi ni watu wema wanaojali na kuthamini utu wa raia, lakini nje ya darasa hilo, polisi ni wauaji. Inatisha.

<p> Mwandishi wa makala haya &nbsp;amejitambulisha kuwa yeye ni msomaji wa Mwanahalisi na anapatikana kwa simu: 0759891849</p>
0
No votes yet