Posho ni mradi wa wakubwa?


Dk. Juma Sued's picture

Na Dk. Juma Sued - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

MJADALA juu ya posho za wabuge na watumishi wengine wa umma umepamba moto kwa serikali kupitia kwa waziri mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda, kueleza umma kwamba serikali ipo katika mchakato wa kuziangalia upya posho hizo.

Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, serikali iko tayari kuangalia pendekezo la kufuta posho mbalimbali wanazolipwa wabunge na watumishi wengine wa umma.

Kauli ya Pinda imetokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge wa upinzani, vyombo vya habari na baadhi ya asasi za kiraia zilizokuwa zikipiga kelele kushinikiza serikali kufuta posho za vikao kwa viongozi wa umma hasa wabunge na mawaziri.

Hata hivyo, Pinda hakueleza Bunge, ni lini serikali itatekeleza ahadi hiyo. Badala yake aliishia kusema, “Serikali imekubaliana na hoja hii.” Akaeleza, “inakwenda kuangalia jinsi ya kuziondoa au kuziingiza katika mishahara posho zinazolalamikiwa.”

Pamoja na kwamba suala la posho lilionekana ni suala la kundi fulani, lakini kila anayetakia mema taifa hili hawezi kukubaliana na utaratibu wa sasa wa serikali wa kugawa fedha za umma kama mali isiyokuwa na mwenyewe kwa kisingizio cha posho.

Kwa mfano, tuanze mjadala huu wa posho kwa kuangalia mawaziri na manaibu waziri. Hawa wamekopeshwa fedha na serikali kwa ajili ya kununua magari. Nusu ya fedha hizo zinalipwa na serikali yenyewe. Wamekopeshwa Sh. 90 milioni.

Mbali na kukopeshwa Sh. 90 milioni kununua magari, mawaziri na manaibu waziri wanatumia magari ya serikali hata kwa kazi zao binafsi. Mathalani, waziri na naibu waziri anatumia gari la serikali kwa kazi za jimbo lake la uchaguzi na hata kwa kazi za familia yake.

Viongozi hawa wa umma wanalipwa posho ya vikao vya Bunge na kamati zake. Wanalipwa posho ya matibabu, posho ya kujikimu ndani na nje ya nchi, pamoja na posho ya mafuta kwa hesabu ya lita 1,000 kwa mwezi. Bei ya kila lita ya mafuta wanayolipwa wabunge wakiwamo mawaziri na manaibu waziri, ni Sh. 2,500.

Mawaziri na manaibu waziri wanalipwa posho ya dereva. Lakini mawaziri na manaibu waziri, wanatumia magari ya serikali kwenda bungeni na katika majimbo yao ya uchaguzi, wakati wanalipwa na Bunge fedha ya posho kwa madereva wao.

Katika kila bajeti, serikali inatenga fedha kwa ajili ya mawaziri na manaibu waziri kutembelea majimbo yao ya uchaguzi. Ni tofauti na zile zinazotolewa na Bunge.

Posho za mafuta ya magari wanazolipwa viongozi wetu, wakiwamo wabunge, mawaziri na manaibu waziri, ni zaidi ya mara tatu ya posho wanazolipwa msaidizi wa ofisi au mshahara wa dereva anayeendesha gari la waziri au mbunge.

Mbali na mawaziri na manaibu wao, kuna spika wa Bunge. Huyu analipwa stahiki zote anazolipwa mbunge wa kawaida, ikiwamo mafuta, mkopo wa gari, posho ya vikao, posho ya matibabu na hata posho ya mavazi.

Wapo wanaosema hata akiendesha mkutano wa Bunge analipwa, tena si fedha haba. Wanasema kila spika au naibu spika ama mwenyekiti wa Bunge anapoendesha kikao anakuwa amejitengenezea Sh. 500,000 kwa kuendesha kikao hicho.

Lakini spika wa Bunge anatumia gari la serikali bungeni na nje ya Bunge. Spika wa Bunge anatumia dereva wa serikali bungeni na nje ya Bunge. Anatumia mafuta ya serikali.

Hata naibu spika naye analipwa hivyohivyo. Analipwa posho ya vikao, posho ya kujikimu, posho ya mafuta na dereva na hata posho ya kuendesha mkutano wa Bunge.

Spika na naibu spika wanaweza kuwa wanalipwa posho za mavazi wanapoenda nje ya nchi – maana yake hereni, bangili, saa, viatu, makatambuga na vinginevyo vinavyonunuliwa wakiwa huko – kwamba vyote hivyo vinatokana na fedha za wavuja jasho wa taifa hili.

Ukiachana na hilo kuna hili pia. Wapo baadhi ya viongozi wanalipwa zaidi ya posho mbili kwa siku. Kwa mfano, makamu wa rais wa Muungano, Dk. Mohammed Gharib Billali analipwa na serikali ya Zanzibar, stahiki zote ukiacha mshahara wa waziri kiongozi mstaafu.

Lakini Dk. Billali analipwa na serikali ya Muungano sitahiki zote hata akiwa Zanzibar. Hata makamu wa pili wa rais, Balozi Seif Iddi ni hivyo hivyo.

Balozi Seif ni mbunge wa Bunge la Muungano. Kwa nafasi yake hiyo analipwa posho ya mafuta, posho ya vikao vya Bunge na posho ya kamati za Bunge. Analipwa hata mshahara wa dereva wake.

Bali, Balozi Seif Iddi akija bungeni anakuja na ndege ya serikali iliyolipiwa mafuta na gharama zote na serikali ya Zanzibar. Analipwa stahiki zote na serikali yake. Nalo Bunge linamlipa. Wapo wengine wengi mfano wa Balozi Seif Iddi.

Kwa ujumla kwa watu wasioelewa ukubwa wa tatizo hili wanaweza kuona kilio hiki cha kutaka posho za vikao zifutwe, hakina maana. Lakini ukweli ni kwamba serikali yaweza kuokoa mamilioni ya shilingi kama itaweza kutimiza ahadi yake ya kuondoa posho.

Wala siyo kweli kwamba posho zote zilizotengwa na serikali hazizidi Sh. 29 bilioni. Inawezekana hapa kilichoangaliwa na posho za vikao, si posho za viongozi wakiwamo mawaziri ambao wanakomba huku na kule kwa pamoja – bungeni na serikalini.

Hizi ni posho za wabunge, mawaziri na manaibu waziri. Lakini nani anafahamu posho anayolipwa rais anaposafiri nje ya nchi kwa siku? Inawezekana kuna mtu kapata mtaji hapa, ndiyo maana pamoja na malalamiko kwamba rais anasafiri mara kwa mara, hakuna anayesikiliza kwa kuwa kuna mtaji wa kuzalisha fedha.

Nani anajua kama rais halipwi posho ya mavazi? Analipwa. Je, analipwa posho ya kikao anapokuwa nje ya nchi? Je, pale anapozungumza kwenye taasisi binafsi – siyo za kiserikali analipwa? Kama ndiyo kiasi gani?

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)