Posho serikalini balaa


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

HUKU serikali ikigoma kuongeza maslahi ya madaktari na walimu kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha, serikali hiyohiyo inatoa malipo makubwa kwa watumishi wanapokuwa masomoni ndani na nje ya nchi.

Waraka wa Watumishi wa Serikali Na.1 wa mwaka 2009 ndio unaelekeza malipo yanayofikia asilimia 80 ya mshahara kulipwa kama posho ya kujikimu.

Waraka huo Kumb. Na. C/AC.17/45/01/E/69 wa 22 Januari, 2009, ulisainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, ulitumwa kwa makatibu wakuu, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa idara zinazojitegemea, wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa na miji.

Wakati mtumishi serikalini anaendelea kupata mshahara wake, amewekewa viwango vya posho ya kujikimu ya mafunzo vya hadi asilimia 80 ya mshahara wake akiwa ndani au nje ya nchi.

Baadhi ya watumishi walioongea na gazeti hili wamedai kuwa nafuu hiyo ndiyo imechochea malalamiko kuhusu nafasi za kusoma nje ya nchi, kuwa zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo na wakati mwingine maofisa walewale kwenda mara mbili au tatu mfululizo.

Waraka unaelekeza kuwa mbali na mahitaji muhimu wakati wa mafunzo, mtumishi atalipwa asilimia 80 ya posho ya kujikimu ya safari za kikazi nje ya nchi atakapokuwa katika mafunzo hayo.

Wenye mshahara wa ngazi ya LSS(P) 1-LSS(P) 6 wanalaipwa $ 336 kwa siku (sawa na Sh. 459,000) wakati wale wa viwango vya LSS(J)1- LSS(J) 3 wanalipwa Euro 260 kwa siku (sawa na Sh. 540,000) na wale wa viwango vya TGS H – TGS Q watalipwa Paundi 180 (sawa na Sh. 468,000). Kwa mafunzo mafupi yanayogharamiwa na serikali na wafadhili, viwango vya posho ni asilimia 20 ya mshahara wa muhusika. (Angalia majedwali).

Lakini kwa mafunzo yanayogharamiwa na wafadhili peke yake, posho ni asilimia 30 ya mshahara, huku mtumishi akiendelea kupokea mshahara wake.

Yambesi anasema katika waraka huo kuwa viwango vya posho za watumishi wanapokuwa mafunzoni, vimetolewa kulingana na tofauti ya mazingira ya mtumishi anapokuwa safarini kikazi na awapo safarini kwa mafunzo.

Utekelezaji wa waraka huo ulianza Januari mosi 2009 kwa utaratibu wa kusomwa pamoja na Nyaraka za Utumishi Na. 3 na 4 za mwaka 2008 kuhusu viwango vya posho ya kujikimu kwa safari za kikazi ndani na nje ya nchi.

Vilevile unasomwa pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 1 wa 2003 unaohusu utaratibu wa watumishi wa umma wanaojiunga na mafunzo ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), pamoja na kanuni za kudumu katika utumishi wa umma, toleo la mwaka 1994.

Kwa mafunzo ya muda mfupi yanayofanyika karibu na vituo vya kazi ambayo mtumishi atakuwa anakwenda mafunzoni na kurudi nyumbani atalipwa asilimia 50 ya posho ya kujikimu kwa safari za kikazi ndani ya nchi kwa ajili ya chakula cha mchana na usafiri.

Waraka huu “umefufuliwa” wakati serikali imekuwa ikificha nyongeza za mishahara na posho za vikao kwa wabunge huku ikikataa kuongezea watumishi wa kada nyingine mishahara inayokidhi mahitaji.

Wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alitangazia umma katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kuwa, serikali haina uwezo wa kulipa madaktari mshahara wanaotaka na kwamba asiyeweza kufanya kazi kwa mshahara wa sasa, atafute kwingine.

Alikuwa anarejea mgomo wa madaktari wakitaka kuboreshewa kwa maslahi yao na vitendeakazi vya kutosha na vya kisasa katika hospitali za serikali.

Serikali imekuwa ikivutana na vyama huru vya wafanyakazi vinavyotaka kuongezwa kwa mshahara wa kima cha chini kufikia Sh. 310,000 kwa mwezi badala ya kiwango cha sasa cha Sh. 150,000.

Katika bajeti iliyopitishwa hivi karibuni, serikali imepandisha kiwango cha mshahara wa kima chini kufikia Sh. 170,000 ambazo hazitakatwa kodi.

0
No votes yet