Posho na umasikini wa ‘kutaga mayai’


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

KAULI ya waziri mkuu Mizengo Pinda, kwamba serikali “itaangalia upya suala zima la posho,” inaelekea kuzima joto la hoja muhimu.

Pinda alikuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake bungeni mjini Dodoma. Tangu hapo, ukimya umetawala.

Kabla ukimya haujaota ndevu, kuna haja ya kurejea mjadala, kukumbushia yaliyojiri na hata kujaribu kufuta ukimya huo. Tuanze kama ifuatavyo.

Unakumbuka kauli ya Pinda kabla ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake. Nakukumbusha. Alisema:
…wote tunajua kuwa hizi posho zenyewe wala hatuzili sisi wabunge; tukitoka tu hapo nje, utasikia una mgeni. Tunawagawia wananchi wanaokuja hapa na hawana nauli…

Huyo ni waziri mkuu ambaye amewahi kujiita na kuitwa “mtoto wa mkulima,” kwa madai kuwa hana makuu.

Kwa mujibu wa Pinda, fedha hizo (Sh.  70,000?), kwa siku kwa mbunge aliyehudhuria kikao, ni kidogo sana na hazistahili kuwa chanzo cha mjadala mkubwa.

Angalia upande mwingine. Huku kuna Hussein Bashe, mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM. Bashe anasema kama ifuatavyo:
Posho (ya Sh. 70,000) ni matofali 350 ya kuchoma, kwa bei ya kule kwetu (Nzega). Ukizidisha hiyo mara siku za vikao (mara wabunge zaidi ya 300), ni fedha nyingi. Tutapata mabweni, maabara; au (kwa) fedha hiyo, utakuwa umesaidia vijana wengi kulipiwa ada katika shule za Kata…(Jumatano, 15 June 2011) .

Waziri mkuu anasema Sh. 70,000 kwa siku si kiasi kikubwa cha fedha; lakini kijana wa UV-CCM anasema kiasi hicho ni mkombozi; tena kwa wengi.

Wakati kijana anaangalia kiasi hicho cha posho kwa kuhusisha mazingira na mafao ambayo mwananchi kijijini au mjini anaweza kupata (muktadha), waziri mkuu anaangalia posho hiyo kwa misingi ya “Kasimu wa Matumizi” – kutumbua na kujitutumua.

Hapa Pinda anatumia mtindo wa “Mabilioni ya Kikwete” ambayo inadaiwa yaligawiwa kwa wananchi, husasan vijana ili wayatumie katika kuanzisha na kuendesha ujasiriamali.

Mtindo wa Pinda wa kugawa nauli, kama ule wa mabilioni ya Kikwete; yote kwa pamoja haina tofauti na utaratibu wa mtawala wa zamani wa Ethiopia, Haile Selasie.

Mtawala huyo aliweka siku maalum kila wiki ya kupita mitaani akigawa fedha kwa “watu masikini.”

Ni hivi: Watu masikini ndani ya mfumo katili wa unyonyaji unaosimamiwa na mtawala; wanatupiwa sehemu ya mapato ya taifa yaliyoibwa na wachache walioko madarakani.

Mgao huo unaambatana na kejeli na kebehi; lakini pia unaambatana na majigambo kwa upande wa watawala kuwa wanasaidia wanyonge. Wanataka kuonyesha kuwa mgao huo ni fadhila kuu na siyo kutukuza wizi na ufisadi.

Kwa njia hii, umasikiti hauondoki. Hauwezi kuondoka kwa kuwa, kwanza fedha zinazotupiwa ni kidogo sana. Wakati mwingine hazitoshi mlo wa siku.

Pili, kiasi kinachotolewa hakilengi kuleta mabadiliko katika maisha ya wahusika, bali ni kishika roho kwa wakati huo ili “watumwa wa umasikini” waendelee kupepeta midomo yao kwa kutukuza wezi.

Tatu, fedha zinazogawiwa kwa masikini hazina uhusiano na mikakati na mipango ya nchi (kama ipo) ya kupambana na umasikini. Kwa hiyo zinalenga kukabili umasikini wa leo mchana; ule wa jioni na siku nyingine hadi Ijumaa ijayo, ni shauri yako.

Nne, “mgao” wa mitaani au nje ya bunge, hauna uhusiano wowote na ujenzi wa uwezo – kiuchumi au kijamii – wa wananchi masikini.

Badala yake, senti wanazotupiwa na wenye shibe, ambao nao wanakiri hazina maana sana kwao; zinasaidia kuua hata chembechembe za juhudi na hata matumaini ya masikini kukomboka.

Tano, masikini waliofanywa bubu kwa kutupiwa makombo kwa njia ya “nauli” nje ya bunge na “misaada ya barabarani,” hulegea akili na mwili; hupoteza fahamu na kushindwa kujitambua; hufa taratibu na mapema.  

Hapa, umasikini ambao watawala wamejengea mazingira bora ya kushamiri, huzaliana na kuenea. Huu ndio huitwa “umasikini unaotaga mayai.”

Lakini Bashe anatumia fikra isemayo fedha hizo zaweza kuwekezwa, hata kama ni katika eneo moja na dogo, katika kukabiliana na umasikini wa miundombinu ya kijamii – elimu na hata afya na usafiri na usafirishaji.

Ikiwa inatoka kwa kijana, ingawa wa chama cha siasa ambacho kimechoka, bado hoja hii ina mantiki na nguvu.

Hii ni hoja inayofanana na hoja nyingine za kupunguza matumizi ya serikali kwa manufaa ya jamii kwa jumla; kwa mfano matumizi ya magari ya kifahari, semina na warsha nyingi na safari za nje ya nchi zisizo na mafao.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndicho kiliibua hivi karibuni, hoja ya kuacha kutoa posho za vikao kwa wabunge na kupunguza matumizi; hadi kiongozi wa upinzani bungeni kurejesha gari la serikali.

Hoja ilikuwa hivi: Kwamba wabunge wanalipwa kile wanacholipwa kwa kuwa wabunge. Kuwa mbunge ni pamoja na kuhudhuria vikao vya bunge.

Ndani ya bunge ndimo wabunge wanafanyia uwakilishi wa waliowachagua; wanatungia sheria na wanapopitishia ushauri na usimamizi wa serikali.

Iweje basi vikao vya bunge, ambako wawakilishi wanapaswa kuthibitisha kuwa ndiko ilipo kazi yao kuu, vilipiwe posho?

Hoja inakwenda mbali. Kwamba wabunge hawataki kufanya kazi yao hadi walipwe posho. Ni kama ofisa wa serikali anayedai rushwa ili aweke saini mkataba wa nchi ya nje kuisaidia Tanzania (!)

Na ndivyo ilivyo. Hata wafadhili wa serikali wameliona hilo. Katika andishi lao ambalo lilinukuliwa na gazeti hili, Toleo Na. 249 la Julai 6 -12, 2011, wanatoa kauli inayobeza watendaji ambao, ama wanakwepa au wanachelewesha kukutana nao.

“Ninaelewa kuwa hizi ni nyakati za shughuli nyingi kwenu, lakini bila kuwepo majadiliano, hatuwezi kuwa makini katika kufanya kazi yetu ambayo, napenda kukukumbusha, kuwa ni kuwasaidia ninyi…” ameeleza mwenyekiti wa kikao cha wafadhili jijini Dar es Salaam.

Katikati ya umasikini mpevu na unaotaga mayai, kuna wanaotaka kulipwa ili wafanye kazi waliyoomba wenyewe.

Kuna wasiotaka kukutana na wafadhili ambao wanawaomba misaada ya fedha, mpaka warushiwe tusi au bezo ndipo akili ikae sawa.

Katika mazingira haya, siyo sahihi kuamini alichosema Pinda – “…kuangalia upya suala zima la posho,”
“Kuangalia upya” ni kufanya nini? “Suala zima” ni nini? Hivi ni vineno vinavyolenga kukimbia hoja iliyoko mezani.

Mjadala huu waweza kupata nguvu pale wabunge wanaouunga mkono watakapokusanya posho zao katika akaunti moja benki na iliyo wazi kwa kila mmoja kukagua.

Wachangiaji waweza kuamua baadaye jinsi fedha hizo zitakavyotumika. Wingi wake na mradi itakapotumika, ndivyo vitafumbua macho ya wengi kuwa Sh. 70,000 kila siku kwa wabunge zaidi ya 300, siyo “senti za nauli” kwa wapigakura kutoka jimboni.

0713 614872, ndimara@yahoo.com, www.ndimara.blogspot.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: