Poulsen: Mwanzo mzuri


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version

AFADHALI kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ameanza kuwapa somo mashabiki na wachezaji wa soka kwa vitendo. Huu ni mwanzo nzuri kwa kocha kuonyesha mwelekeo wake mapema kwamba, habebi mizigo.

Ametema wachezaji saba “mastaa” kwa safari ya Algeria ambako atacheza na timu ya taifa hilo la ‘kiarabu’ 4 Septemba, 2010 katika mchezo wa kutafuta nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Hakuna Mtanzania aliyezoea kuona Jerry Tegete, Juma Jabu na Kelvin Yondani ‘Vidic’ wanatemwa katika kikosi cha Stars kwa sababu za kushuka viwango kwa zaidi ya miaka minne sasa. Labda kama wangekuwa majeruhi.

Baadhi ya mashabiki wa soka pamoja na wachezaji wenyewe hawakuridhishwa na tukio hilo. Wapo wanaoona Poulsen hakufanya uchaguzi sahihi. Kisa kuwatema Yondani, Uhuru na Tegete. Juma Kaseja na Athuman Idd Chuji wao wametemwa kutokana na majaraha, hakuna anayelalamika kuhusu wao.

Poulsen hataki kubeba wachezaji kwenye timu asiowatumia. Pia hataki kuchagua wachezaji kwa majina yao. Anataka jina lililothibitishwa na uwezo wake uwanjani.

Penye Idrissa Rajabu na Stephano Mwasika wenye uwezo wa kusaidia mashambulizi na kurudi haraka kulinda upande wa kushoto, Poulsen haoni nafasi ya Juma Jabu anayekatika mara kwa mara. Pia alipo Agrey Morris na Nadir Haroub haoni pa kumpanga Kelvin Yondani anayechanganyikiwa mashambulizi yanapomzidi.

Kwenye kiungo wapo, Erasto Nyoni, Henry Joseph, Nurdin Bakari, Abdi Kassim, Seleman Kassim, Shaban Nditi na Jabir Aziz, Poulsen kwa sasa haoni nafasi ya Abdulhalim Humud, labda baadaye atakapoacha kucheza na jukwaa.

Ingawa Jerrison Tegete ameifungia mabao mengi Stars nyuma ya Mrisho Ngassa kwa wachezaji wa hivi sasa, lakini Mdenishi haoni nafasi ya mchezaji laini kama yeye mbele ya watu ngangari kama John Boko, Mussa Hassan Mgosi, Nizar Khalfan, Ngassa na Danny Mrwanda.

Ni wakati wenu sasa kina Yondani, Humud, Tegete na Uhuru kuacha kujiona mko juu kuliko wengine. Fanyeni kazi uwanjani badala ya midomoni anavyosema Kocha Mkuu, Patrick Phiri.

Maximo alipochukua timu mwaka 2007, alisafiri na Tegete na baadaye David Naftari kila alipokwenda na Stars kwa lengo la kuwakomaza. Ni kweli wakati ule Tegete alikuwa kinda, pengine alistahili kukomazwa kwa njia hiyo, lakini sasa si kinda tena. Kama hajakomaa mpaka leo basi hakomai tena.

Nafasi ya kukomazwa haipo tena kwa Tegete, Naftari wala Kigi. Huu ni wakati wao kuonyesha uwezo uwanjani baada ya kukomazwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kocha Poulsen alipotaja kikosi cha wachezaji 27 wa Stars kwa mara ya kwanza aliwaita kikosini “wakorofi” kipa Juma Kaseja wa Simba na kiungo Athuman Idd wa Yanga. Huo ulikuwa mwanzo nzuri kwa Poulsen kuamua kuondoa msigano na mashabiki waliomchukia Maximo kwa kuwaengua nyota wao.

Poulsen alisema hawafahamu vizuri wachezaji wa Tanzania. Alisema kikosi alichokiita ni kile kilichokuwa kinatumiwa na mtangulizi wake, Marcio Maximo na kwamba wachezaji hao ametajiwa na makocha wake wasaidizi na mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni. Aliahidi kufanya mabadiliko kila anapoona kuna haja ya kufanya hivyo.

Mabadiliko aliyoahidi tumeanza kuyaona. Mashabiki wa soka tunatakiwa kumuunga mkono kocha wetu badala ya kuanza kumkosoa hata kama hatapata matokeo mazuri huko Algeria.

Tumeona katika mechi ya kirafiki dhizi ya Kenya timu jinsi ilivyocheza. Ingawa hatuwezi kumpima kocha kwa mchezo mmoja, tena akiwa na timu kwa wiki moja tu, lakini timu haikucheza vibaya. Hasa kipindi cha pili baada ya kocha kufanya mabadiliko yaliyokuwa na faida.

Kabla ya kuondoka kuelekea Algeria, Poulsen alikuwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo dhidi Waarabu hao, hasa kutokana na mwitikio wa wachezaji wake wanaocheza nje ya nchi.

Ingawa Stars itakuwa na nyota wake wanne wanaosakata soka la kulipwa kama Nizar Khalfan, Danny Mrwanda, Henry Joseph na Idrissa Rajab haitakuwa rahisi kuwatetemesha Waarabu waliojaza nyota wanaocheza Ulaya.

Wakati Stars ya Poulsen ikiwa na wachezaji wanne tu wanaocheza soka la kulipwa. Kikosi cha Algeria kina mchezaji mmoja tu anayecheza nyumbani, naye ni mlinda mlango, Mohamed Lamine anayechezea MC Algiers.

Pamoja na karibu kikosi chote cha Algeria kuundwa na nyota wanaocheza soka nje ya nchi yao, wachezaji na benchi la ufundi la Stars inabidi wawe makini na beki mkongwe anayecheza upande wa kushoto wa Algeria, Nadir Belhadj anayechezea Al-Sadd ya Qatar.

Viungo wa Stars kina Henry Joseph Shindika watakuwa na kazi ya ziada kuzuia kasi ya kiungo mkongwe, Karim Ziani mwenye miaka 28. Ziani anayeichezea Wolfsburgya Ujerumani, ameifungia timu yake ya taifa magoli 58.

Kocha mzalendo wa Algeria, Rabah Saadane amemjumuisha kikosini mashambuliaji hatari wa AEK Athens ya Ugiriki, Rafik Djebbour, aliyeifumgia timu yake ya taifa mabao 26.

0
No votes yet