Prof. Bayikwa: Mbunge mfuatiliaji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version

WANANCHI katika eneo la Halmashauri ya wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, wana bahati ya kuwa na mbunge anayejua kufuatilia matumizi ya fedha kwa ajili ya maendeleo yao.

Huyu ni Profesa Feetham Filipo Banyikwa (61), anayeongea taratibu, kwa ufasaha na kujiamini. Anatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI hivi karibuni mjini Dodoma, Banyikwa anasema msimamo wake wa kutaka fedha za umma zitumike kama zilivyopangwa tayari umemletea matatizo na baadhi ya viongozi wenzake katika halmashauri.

"Tabia yangu hii imeleta mtafaruku katika halmashauri. Hakuna maelewano kati ya mbunge na mkurugenzi na mingoni mwa baadhi ya madiwani," anasema.

Anasema baadhi ya watu katika halmashauri hawataki kufuata taratibu za matumizi ya fedha za umma; hawataki kutumia fedha hizo kwa kazi iliyokusudiwa.

"Lakini kwa kuwa mimi sikugombea ubunge kwa sababu ya kutokuwa na kazi, hili nitalisimamia kwa nguvu zangu zote. Wala katika hili, hakuna mwenye ubavu wa kunizuia," anasema.

Akiongea kwa uchungu, Banyikwa anasema Halmashauri ya Ngara imetumia zaidi ya Sh. 800 milioni zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) bila kufuata taratibu.

Anasema, "Pale Ngara, kakuna mwenye uhakika wa kueleza Sh. 800 milioni zilivyotumika. Fedha hizo zilitolewa na TASAF kati ya mwaka 2002 na 2005. Hakuna kumbukumbu sahihi. Ni ubabaishaji mtupu."

Kutokana na ubadhilifu huo wa fedha, anasema ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) imetoa hati ya mashaka kwa halmashauri yake kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2008.

Wakati hesabu za halmashauri zinaonyesha kwamba fedha hizo zimetumika kama zilivyopangwa, Banyikwa anasema baadhi ya waliotoa huduma kwa halmashauri, bado hawajalipwa kile wanachoita "fedha za gharama kwa huduma walizozitoa."

Anasema hata miradi iliyotekelezwa kwa fedha hizo haijulikani. Vijiji vilivyofaidika na miradi hiyo navyo havijulikani; hata ripoti ya matumizi ya fedha hizo bado haijaandikwa.

Mara baada ya mbunge Banyikwa kuchaguliwa, kazi yake ya kwanza aliyojipa ilikuwa kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kama zilivyokusudiwa. Anasema ni kwa njia hiyo tu maendeleo yataweza kupatikana.

Anasema hilo ndilo jambo ambalo amekuwa akilizungumza siku zote kabla na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini wenzake katika halmashauri walikuwa wakipinga kuwepo ubadhilifu wa fedha za TASAF.

Anasema chanzo cha yote hayo, ni mbunge aliyekuwapo ambaye anadai kuwa hakuwa na uwezo wa kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri.

Banyikwa anasema alipata taarifa za matumizi mabaya ya fedha kupitia kumbukumbu zilizopo katika ofisi ya halmashauri ya Ngara na TASAF makao makuu.

Anasema, "Baada ya CAG kutoa taarifa yake ambayo imethibitisha kile nilichokuwa nikikieleza, wahusika wanaweza kusimama na kukana madai yangu?" anahoji.

Pamoja na kwamba Banyikwa hataki kuingia kwa undani kuzungumzia kilichoisibu Ngara, lakini taarifa za CAG zinazoishia 30 Juni 2008 zinaonyesha, "Ngara imepata hati ya mashaka" katika maeneo yafutayo:

Kwanza, uwasilishaji wa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za maendeleo zisizokuwa sahihi. Katika hili, serikali ilitenga Sh. 8.4 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo wilayani humo.

Pili, kukosekana kwa nyaraka mbalimbali zikiwamo mikataba, pamoja na michanganuo ya thamani ya vyeti vya malipo. Kiasi cha Sh. 62,971,520 zilitengwa katika eneo hilo.

Tatu, kushindwa kuonyesha matumizi ya Sh. 913,285,806 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na shule. Fedha hizo hazikuonyeshwa katika hesabu za matumizi ya maendeleo.

Nne, halmashauri imeshindwa kuonyesha umri wa wadaiwa wa Sh. 13,390,000 milioni; vifaa visivyoingizwa vitabuni vimetumia zaidi ya Sh. 11. 1 milioni.

Tano, halmashauri imepewa hati chafu kutokana na kushindwa kurejesha hazina fedha za mishahara zinazokadiriwa kufikia Sh. 7,043,970.

Akizungumzia miradi ya maendeleo, Banyikwa anasema katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya ubunge wake, tayari amefanya mambo mengi makubwa. Anataja ufuatiliaji wake kwa mradi wa umeme, kutoka Ngara hadi Kabaga.

Mradi huo ambao tayari umeanza, umesambaza umeme katika vijiji mbalimbali vikiwamo Muhweza, Murugalama, Ngundusi na Kabanga mjini.

"Si hivyo tu, bali nimefuatilia na kusimamia ujenzi wa sekondari mbili za Kabanga na Lukole ambazo ni za Kidato cha Tano na Sita. Nimesimamia upatikanaji wa kivuko kipya cha Rusumo ambacho hivi karibuni kitaangizwa na serikali," anasema.

Anasema kivuko cha sasa chenye uwezo wa kubeba watu 50 na tani 10 za magari hakitoshelezi mahitaji ya eneo hilo.

Profesa Banyikwa anasema serikali ya wilaya imeagiza matrekta 30 ambayo yatasaidia kuboresha kilimo chini ya mfuko wa mradi wa ASDP.

Anasema fedha za awamu ya pili zilitolewa mwaka 2005 ambapo wilaya ya Ngara ilitengewa Sh. 1.2 bilioni. Fedha hizo zilizotolewa wakati yeye akiwa tayari mbunge zimetumika kama zilivyopangwa ikiwa nipamoja na kujenga shule 18 za kata.

Profesa Banyikwa alizaliwa 3 Oktoba 1947 katika kijiji cha Murugalama, wilaya ya Ngara, mkoani Kagera na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Mabawe, Ngara kuanzia mwaka 1955 hadi 1958.

Mwaka 1959 hadi 1962 alijiunga na elimu ya kati katika shule ya Mulugwanza na kisha Sekondari ya Livingstone mkoani Kigoma kutoka mwaka 1963 hadi 1966. Mwaka 1967 hadi 1968 alijiunga na shule ya Sekondari ya Kibaha, Pwani kwa masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1969 ambako alihitimu shahada ya kwanza katika baolojia mwaka 1972 ambapo alikwenda kufundisha shule ya Sekondari ya Mazengo, Dodoma.

Mwaka 1973 alirudi tena UDSM kwa ajili ya kusomea digrii ya uzamili (M.A) na nyingine ya uzamivu (PhD) mwaka 1976. Kisha akafundisha chuoni hapo kama mkufunzi wa Idara ya Elimu Mimea kwa miaka 15. Aliondoka hapo mwaka 1990.

Anasema baada ya kuondoka UDSM alijiunga na taasisi ya utafiti ya Tanzania Wild Life Institute, Serengeti kwa ajili ya kufanya utafiti wa wanyamapori katika mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Profesa Banyikwa alikaa katika asasi hiyo hadi mwaka 2005 alipoamua kujitosa katika siasa kwa kugombea ubunge katika jimbo la Ngara. Anatarajia kutetea nafasi yake katikauchaguzi mkuu ujao.

0
No votes yet