Prof Lipumba: ‘Rais’ bora anyekosa kura za kutosha


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Profesa Ibrahim Lipumba

WIKI iliyopita nilieleza kwa ujumla sifa za aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ikilinganishwa na waliokuwa wapinzani wake katika uchaguzi uliopita.

Pamoja na ubora wa Prof. Lipumba, ambaye Tanzania haitapata bahati kuongozwa naye, upo udhaifu mkubwa tena wa kimkakati ndani ya CUF, ambao ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia asiwe anapate kura za kutosha katika kila uchaguzi.

Kwa mtazamo wa baadhi ya wafuasi wa CUF, hasa wale waliosoma makala iliyopita, vyombo vya habari nchini vinapendelea kuandika habari za vyama viwili; Chama Cha Mapinduzi (CCM) na na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wote walionipigia simu wakilalamikia tabia ya vyombo vya habari kupendelea CCM na CHADEMA, niliwauliza swali moja; nani alikuwa meneja kampeni kitaifa wa CUF?

Nilipowauliza nani alikuwa meneja wa kampeni wa CCM, walinijibu Abdulrahman Kinana na nilipouliza nani alikuwa meneja kampeni za CHADEMA, walijibu Prof. Mwesiga Baregu.

Hakuna hata mtu mmoja aliyejibu kwa usahihi swali hilo. Waliokaribia walimtaja Said Miraji, ambaye kwa kweli alikuwa meneja kampeni wa Prof. Lipumba katika uchaguzi huo.

Meneja kampeni za CUF kitaifa, hakuwa mwingine isipokuwa Naibu Katibu mkuu wa CUF (Bara), Joram Bashange.

Ikiwa wananchi walikuwa wanawafahamu Kinana na Prof. Baregu, nini kilizuia wasimfahamu Bashange?

Jibu ni rahisi, Bashange hakufanya kazi yake ipasavyo kupitia vyombo vya habari wakati wa kampeni.

Wakati Kinana na Prof. Baregu walikuwa wepesi kuita wanahabari kufafanua shutuma dhidi ya wapinzani na kuzima propaganda dhidi ya vyama vyao, Bashange hakuwa na cha kusema
Watu walitaka vyombo vya habari viandike nini kuihusu CUF iwapo wenyewe hawakuwa na kitu cha kusema?

Wapo waliosema kuwa hata kama Bashange angekuwa anaitisha mikutano, taarifa zisingetoka kwa vile vyombo vya habari na hasa “magazeti” hayakipendi chama cha CUF.

Hivi ni kweli magazeti yasingeandika pale Bashange anapokanusha kwamba CUF si chama cha chuki, udini na fitina? Dongo hilo limerushwa na CCM wakati wote wa kampeni.

Katika kampeni CCM iliamua kutumia silaha zake zote bila kujali kama kuna watu wataumia au laa, ndiyo maana Kinana na Prof Baregu walikuwa wanaitisha mikutano kila wiki na kila ilipolazimu. Hiyo ndiyo kazi ya wenyeviti na mameneja wa kampeni.

Kitendo cha mwenyekiti kukaa kimya wakati chama ‘kinajeruhiwa’ kwa kampeni chafu za udini unawafanya watu waamini uongo na wakiogope chama. Wananchi wakiamini uongo na kukiogopa chama mgombea urais si atakuwa anapoteza muda bure?

Mathalani, siku chache kabla kampeni hazijafungwa rasmi, mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alirusha makombora mazito dhidi ya CCM katika mdahalo uliorushwa kupitia ITV.

Kinana hakupata usingizi. Aliitisha haraka mkutano wa waandishi wa habari, likiwemo MwanaHALISI ili ajibu hoja za Dk. Slaa na alifanya hivyo kwa lengo la kushawishi wapigakura.

Bashange alikuwa ametulia tuli ofisini kwake “akifanya kazi za chama.” Si kwamba Bashange hakufanya chochote wakati wa kampeni lakini alichofanya hakikuendana na kilichotakiwa kufanya.

Kimkakati CUF lazima wakiri kwamba walifanya kosa kumteua Bashange kuwa meneja kampeni.

Duniani kote, hakuna chama cha siasa kinachomteua mtu mwenye wadhifa ndani ya chama kuwa meneja wa kampeni.

Meneja kampeni wa Barack Obama alikuwa David Axelrod ambaye hakuwa na wadhifa wowote kwenye chama cha Democrat zaidi ya kuwa mwanachama.

Kinana na Baregu hawana nyadhifa zozote nzito ndani ya vyama vyao zaidi ya uanachama na ujumbe wa kamati kuu.

Kwa hiyo, kitaifa, CUF ilifanya kosa la mwaka kumteua naibu katibu mkuu wa chama kushika wadhifa huo. Huyu angeachwa kufanya kazi za chama chake na mzigo huo ungemwangukia mtu mwingine.

Kosa jingine linamhusu Bashange mwenyewe. Katika dunia ya leo, nafasi ya meneja kampeni inataka mtu ambaye anafahamika tayari na mwenye mtandao mpana ndani na nje ya sekta ya habari.

Kinana amefanya kazi ya umeneja kampeni kwa miaka 15 sasa. Anajua la kufanya na anafahamiana na walau mtu mmoja katika vyombo vya habari vikubwa hapa nchini.

Hali iko hivyo hivyo kwa Baregu ambaye amejijengea jina tayari kama msomi na mwanaharakati. Karibu wana habari wote wanamfahamu Baregu.

Bashange hafahamiki. Hana mvuto kwa watu. Na hata kama anazungumza, hawezi kupewa uzito kama ule ambao angeweza kupewa mtu kama Baregu.

CUF ingeweza kabisa kumteua mtu kama Hamad Rashid Mohamed kuwa kampeni meneja wao. Ingawa mwenyewe alikuwa mgombea ubunge katika jimbo la Wawi, angelazimishwa kubeba mzigo huo.

Hamad hana wadhifa wowote wa kichama zaidi ya kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho. Jimbo la Wawi ni la CUF tu hata kama Hamad angefanya kampeni kwa wiki mbili.

Ni wazi waandishi wa habari wangependa kutaka kumsikiliza Hamad ana nini kuliko Bashange. Na mwanasiasa huyo, kwa sababu ya mazoea yake na wana habari, angekuwa anajua nini kingefaa kuwa habari.

Kwa hiyo, kwa kuwa na meneja kampeni asiye maarufu na uzoefu wa siasa za kitaifa, CUF ilikuwa imejipanga kuhakikisha Prof. Lipumba hapati kura za kutosha katika uchaguzi uliopita.

Nina ushahidi wa kutosha kueleza kwamba Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, hakujua kwamba Prof. Lipumba alikuwa anafunga kampeni Dar es Salaam hadi alipoambiwa siku hiyohiyo.

Yeye alikuwa na ratiba zake Kaskazini Unguja. Iwapo makamu mwenyekiti wa chama hajui hata siku ambayo chama chake kinafunga kampeni, hapo kuna tatizo la oganaizesheni ya mambo ya kampeni.

Kuna taarifa pia kwamba ratiba ya kampeni ya Lipumba ilipangwa vibaya. Kuna maeneo alikaa muda mrefu na mengine hakufanya kazi ya kutosha.

Kuna viongozi wa CUF waliwahi kueleza namna Prof. Lipumba mwenyewe alivyoshangazwa na ratiba hiyo. Haikuzingatia jografia ya nchi na kuna maeneo alipita wakati akienda kwingine huku maeneo hayo akiwa hajafanya kampeni.

Jumamosi ya Oktoba 30 mwaka huu, Lipumba alifunga kampeni zake katika viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam.

Dk. Slaa alifungia kampeni mkoani Mbeya. Matokeo yake CHADEMA imepata wabunge wawili mkoani Mbeya na imefanya vizuri katika mkoa huo kiujumla.

Prof. Lipumba hakuwa na sababu za kufanya mkutano Kidongo Chekundu wakati alishafunga kampeni kitaifa katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Kama angeshauriwa vizuri angeweza kwenda kufunga kampeni zake ama Tanga, Lindi, Mtwara au Kondoa; maeneo ambayo ana ngome na kurejea Dar es Salaam kupiga kura yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: