Prof. Lipumba: Huu ni wakati wa kujenga CUF


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MIAKA miwili iliyopita, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe aliwahi kufunga safari kwenda nyumbani kwa aliyekuwa kiongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, Julius Mtatiro.

Lengo la Mbowe katika safari hiyo, halikuwa jingine zaidi ya kumshawishi Mtatiro ajiunge na CHADEMA kwa vile tayari alikuwa amemwona kijana huyo angemfaa kwenye chama chake. Hakufanikiwa, lakini angalau alijaribu.

Zaidi ya Mtatiro, Mbowe amefanya juhudi kubwa za kuvutia vijana wengi wasomi wajiunge na chama chake. Matokeo yake, CHADEMA sasa kimegeuka kuwa chama kimbilio kwa vijana wasomi nchini.

Lakini sivyo ilivyo. Katika mazingira ya kawaida kabisa, CUF inayoongozwa na profesa wa uchumi ambaye anaheshimika duniani kote, Ibrahim Lipumba, alipaswa kuchukua juhudi kama hizo ili chama hicho kiwe pia kimbilio la vijana wasomi, lakini kiko kimya.

Prof. Lipumba, katika miaka yake takriban 10 ya uongozi wake ndani ya CUF, hajafanya juhudi za maana za kuhakikisha anavutia vijana wengi zaidi kujiunga na chama chake. Hata Mtatiro ni kwa sababu ya mapenzi binafsi.

Athari zake ni hizi, kama ataamua kuachana na siasa leo, CUF haina mtu ambaye anaweza kupewa uenyekiti wa chama hicho kutoka Tanzania Bara na watu wasiwe na matatizo naye.

Kama hali itaendelea kuwa kama ilivyo sasa, Lipumba itabidi tu awe mgombea urais wa CUF mwaka 2015 kwa sababu hajatengeneza ndani ya chama au hajavuta ndani ya chama watu ambao angeweza kusema ni matunda yake kwa lengo la kukijenga chama.

Hawa akina Jakaya Kikwete ambao tunawaona leo, wamekuja kuwa viongozi kwa sababu akina Pius Msekwa walifanya juhudi za makusudi za kuwavutia CCM wakati walipomaliza masomo yao ya chuo kikuu.

Hakuna taarifa hata kutoka ndani ya chama kwamba kuna siku Prof. Lipumba alifunga safari kwenda kwa kijana asiyefahamika sana kumshawishi ajiunge na CUF. Hii si kawaida yake na kwa namna hii hakitendei haki chama chake.

Damu ya chama chochote cha siasa ni vijana. Vijana ndio wanaokihakikishia chama mustakabali wake katika kipindi cha miaka 20 hadi 30 ijayo.

Wakati Msekwa alipokuwa akiwashawishi akina Kikwete wajiunge na CCM mwanzoni mwa miaka ya 1970, kichwani kwake alijua hao ndiyo watakuwa viongozi wa chama miaka 20 ijayo. Na hata alipoteuliwa kuwa makamu mwenyekiti, Msekwa alipita vyuoni kupata vijana na kutengeneza matawi ya vyuo jirani.

Vijana ambao Mbowe amewashawishi kujiunga na CHADEMA mwaka 2008, ndio wanashika hatamu katika matawi na watakuja kuwa na viongozi wakuu miaka michache baadaye.

Kutoingiza wanachama wapya ndani ya CUF kumemfanya Prof. Lipumba aendelee kusikiliza watu walewale, wenye mawazo yaleyale ndani ya chama hicho, jambo linalofanya mambo yawe mabaya zaidi.

Ndiyo maana chama hicho kimegoma kutumia helikopta kwenye kampeni zake za urais kikidai walengwa katika kampeni wako chini si angani? Je hii ni hoja ya kuitumia katika nchi isiyo na miundombinu mizuri?

Akiwa mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba aliruhusu ratiba ya kampeni ya chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita ipangwe kutoka Zanzibar.

Yeye alikuja kushtukia ratiba imepangwa na ilikuwa mbaya kimkakati. Akiwa mtu anayeifahamu vizuri jiografia ya nchi na mwenyekiti wa chama, alipaswa kuwa na nguvu ya kuikataa ratiba hiyo na kuifumua ili itengenezwe upya, lakini hakufanya hivyo, kosa ambalo limemgharimu.

Prof. Lipumba ni mtu anayependa kusikiliza watu. Tatizo kubwa ni kuwa amezungukwa na watu ambao anatofautiana nao mno kiuwezo na hataki kupingana nao sana akihofu wanaweza kujihisi vibaya.

Mbowe anapozungumzia viongozi vijana ndani ya chama chake anazungumzia watu kama Kabwe Zitto, John Mrema, John Mnyika na Halima Mdee.

Zitto na Mrema waliwahi kuwa viongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mnyika alikuwa kiongozi wa asasi ya kitaifa ya vijana kabla hajaingia rasmi CHADEMA. Mdee alishaanza shughuli za kisheria na harakati kabla hajawa kigogo wa chama hicho.

Ndani ya CUF, ni Mtatiro pekee ambaye ana historia ya kuwa kiongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hivyo ni mwelewa wa masuala ya harakati za makundi.

Wakurugenzi vijana wengine wa chama hicho Tanzania bara, Mbaralah Maharagande, Shaweji Mketo na Ashura Mohamed, ni wanasiasa wazuri lakini hawawezi kuwa kundi moja na vijana wa kaliba ya akina Zitto; kuna tofauti.

Kwa mfano, zaidi ya kuwa kiongozi wa wanafunzi, Zitto alishiriki hadi katika harakati za umajumui wa Afrika (Pan Africanism) na kuhudhuria mikutano ya Bara la Afrika na kidunia katika enzi yake ya uanafunzi.

Uzoefu wa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Joram Bashange, ni kuwa kiongozi wa wafanyakazi katika mashamba ya miwa, Kilombero mkoani Morogoro !

Zanzibar, CUF haina tatizo hili lililopo bara. Katibu Mkuu, Maalim Seif ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar na mtu aliyepikwa ndani ya Afro Shiraz (ASP) na CCM enzi za ujana wake. Hali iko hivyo pia kwa Juma Duni Haji.

Viongozi wengine wa juu wa chama hicho kama vile Ismail Jussa Ladhu na Abobakary Khamis Bakary ni wanaharakati na wasomi wa kiwango cha juu. Ndiyo maana CUF inamea visiwani na taratibu imatokomea Tanzania bara.

Ni kweli kwamba CUF ina matatizo ya kutoandikwa sana kwenye vyombo vya habari kama ilivyo kwa CCM na CHADEMA. CCM ina faida ya kuwa chama tawala ambayo CUF na CHADEMA hawana.

Hata hivyo, CHADEMA inapata faida pia kwa sababu viongozi wake vijana wana ushirikiano mzuri na waandishi wa habari ambao wengi wao ni watu wa umri wa wao.

Suala la kwanini CUF haipati nafasi kwenye vyombo vya habari kama wenzao linahitaji nafasi yake ya peke yake kujadiliwa.

Hata hivyo, uongozi uliopo sasa hauwezi kubadili hali hii kwa sababu unafanya kazi katika mazoea ya kwamba “sisi hatupendwi na vyombo vya habari.” Wanahitajika watu wapya ambao watakuja na mbinu za kuirejesha CUF kileleni.

Na hii ni kazi ambayo Prof. Lipumba anatakiwa kuifanya sasa, maana kama atashindwa kuifufua kutoka hali hii, kuna hatari chama kumfia mkononi katika miaka hii mitano ijayo.

Na kama ataruhusu CUF imfie mkononi mwake, watu watashukuru kwamba Mungu aliwaepusha na balaa la kuongozwa naye iwapo wangemchagua.

Maana, swali ambalo wengi watajiuliza ni kuwa, iwapo CUF imemshinda, angeweza kuifanyia nini Tanzania ambayo changamoto na matakwa yake ni makubwa mno ikilinganishwa na yale aliyonayo sasa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: