Prof. Lipumba: Milango ya majadiliano ni wazi


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Profesa Ibrahim Lipumba

PROFESA Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka huu anaweka rekodi ya pekee. Anakuwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kuwania urais Bara kwa vipindi vinne tofauti tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1992.

Mara zote hizo amewania urais kupitia CUF. Aliwania nafasi hiyo katika chaguzi za mwaka 1995, 2000 na 2005. Mwaka 1995 alishika nafasi ya tatu kwa kura za urais akimfuata Augustine Mrema wa NCCR-Mageuzi; lakini mwaka 2000 na 2005 alishika nafasi ya pili.

Mara zote Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitangazwa kushinda. Mwaka 1995 na 2000 alishinda Benjamin Mkapa wa CCM na mwaka 2005, alishinda Jakaya Mrisho Kikwete.

Anayemfuatia Prof. Lipumba kwa kugombea urais Bara mara nyingi ni Mrema. Mwaka 1995 alikuwa anatokea NCCR-Mageuzi lakini mwaka 2000 na 2005 alipitia TLP. Mwaka huu, Mrema ambaye anaonekana mchovu, ameamua kuwania ubunge katika jimbo la Vunjo.

Katika mahojiano ofisini kwake, Alhamisi iliyopita, nilimuuliza Prof Lipumba: “Nini kipya umepanga kwa ajili ya kampeni mwaka huu kilicho tofauti na vipindi vitatu vilivyopita?”

Profesa Lipumba alisema mwaka huu kuna maeneo mawili ambayo wameamua kuweka nguvu zaidi kuliko katika chaguzi zilizopita. Kwanza, katika kufanya kampeni za uchaguzi na pili, katika kuhesabu kura.

“CUF imejizatiti kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba zitakazokwenda sambamba na zile za majukwaani. Tutawafuata wananchi majumbani mwao na hiki kitakuwa kitu kipya kwetu,” alieleza Prof. Lipumba.

“Lakini pili, tunaimarisha nguvu kwenye mawakala wetu wa uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha kwamba kura wanazopiga zinahesabiwa zote na kihalali. Haya ni maeneo mawili muhimu sana,” alisisitiza.

Anasema hatua hizo zinatokana na uzoefu waliopata katika chaguzi zilizopita ambako anaeleza kuwa kumekuwa na “wizi mkubwa” wa kura.

“Nakumbuka mwaka 2005 nilipiga kura kuchagua rais, mbunge na diwani katika eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam. Lakini ukienda kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi (NEC) utaona mgombea wa udiwani CUF Kunduchi hakupata kura hata moja kwenye uchaguzi huo.

“Na hali hii iko kwenye maeneo mengi hapa nchini. Si kwenye udiwani pekee; iko pia kwenye ubunge na urais. Hii ndiyo maana tumeweka mkakati maalumu kwenye kuhakikisha kura zetu zinalindwa,” anasema na kuongeza kuwa Watanzania wana hamu ya kuona mabadiliko ya uongozi, kwa kuiondoa CCM na kuweka upinzani madarakani.

“CCM imedanganya Watanzania. Mwaka 2005 iliahidi Maisha Bora kwa Kila Mtanzania lakini sasa tunaona Maisha Bomu kwa Kila Mtanzania. Ushahidi wa hili uko wazi.

“Mwaka 2005, kilo moja ya sembe ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 250, hivi sasa inauzwa kwa karibu Sh. 1,000. Mchele wa Kyela ulikuwa ukiuzwa Sh. 450 kwa kilo; hivi sasa unauzwa kwa Sh. 1700. Hali imekuwa ngumu zaidi.

“Wananchi wamechoka na siasa za ghilba, rushwa na zisizo na mwelekeo. Wanataka mabadiliko na sisi CUF tumejiandaa kuweka serikali mbadala na kukata kiu ya Watanzania ya kuwa na serikali makini,” anasema.

Akizungumzia sababu za upinzani kutokuwa na mgombea mmoja katika nafasi ya urais, Lipumba amesema tatizo ni ukosefu wa mawasiliano na kutoaminiana katika kambi hiyo.

“Mimi ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba kama wapinzani tutaungana na kuwa kitu kimoja, itakuwa rahisi zaidi kuing’oa CCM kuliko tukitengana. Na ninafahamu pia kwamba wananchi wanataka sana hilo,” anasema Profesa Lipumba.

Anasema chama chake na vingine vilikuwa vikienda vizuri tangu baada ya uchaguzi wa mwaka 2005. Hata hivyo, anasema kifo cha Chacha Wangwe (Mb) mwaka 2008, kiliacha doa kubwa sana katika mahusiano ya vyama.

“Tangu wakati huo, yakaanza maneno kwamba ndoa ya upinzani imevunjwa na kwa kweli hakukuwapo na mawasiliano mazuri tena tangu kifo cha Wangwe na baada ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime mambo yakaharibika.

Mwanzoni mwa mwaka huu, anaeleza profesa, zilikuwapo dalili mbaya, kwamba kilikuwapo kikundi kidogo ndani ya nchi hii kilichotaka Rais Jakaya Kikwete apite bila kupingwa kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

“Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA) akasema hatagombea. Dk. Willibrod Slaa naye akasema hatagombea. Mrema naye akasema hatagombea na Dk. Sengondo Mvungi wa NCCR-Mageuzi akasema hagombei. Sasa sisi CUF tukasema ni lazima tugombee na tuweke mgombea makini.

Siku chache baada ya CUF kuamua kuweka mgombea makini, vyama vingine navyo vikateua wagombea wao kwa lengo la kupambana na mgombea wa CCM, Rais Kikwete.

DP ilimteua mwenyekiti wake Mchungaji Christopher Mtikila, TPP-Maendeleo ikamteua Peter Kuga Mziray, NCCR-Mageuzi ikamteua…Rungwe…., TLP ikampitisha…Mutamwega Mugayuwa…….. na CHADEMA wakamteua Dk. Slaa.

Kati ya hao wote, Prof Lipumba anastushwa na uteuzi wa Dk. Slaa ambaye amekuja kubadili upepo wa siasa katika kambi ya upinzani.

“Uteuzi wa Dk. Slaa umekuja ghafla. Hatukuwa tumejiandaa kwa hilo na kwa muda uliobaki ni vigumu kufanya lolote lingine. Sheria hairuhusu CUF na CHADEMA kuungana kuwania urais na ugombea mwenza.

Hata hivyo, anasema bado upinzani unaweza kuungana kwa kuachiana nafasi za ubunge na udiwani pale ambako wagombea binafsi wataonekana kuwa bora kuliko wenzao.

“Sote tunajua wapi CUF ina nguvu kuliko CHADEMA na wapi CHADEMA ina nguvu kuliko CUF. Ni suala la kukutana na kujadili tu ili kupata mwafaka,” anaeleza.

Anasema ushirikiano unaweza pia kwenda kwenye eneo la mawakala ambako wanaweza kutumia wakala mmoja kwa vyama viwili.

Profesa Lipumba anasema kuna karibu vituo 55,000 vya kupigia kura nchini. Anasema zinathitajika Sh. 275 milioni kulipa mawakala kwa kiwango cha Sh. 5,000 kwa siku. Hiki ni kiasi kikubwa kwa vyama vya upinzani, anasema.

“Wenzetu CCM wanaweza kumwomba fisadi mmoja awalipie gharama hii na wakampata. Sisi hatuna mjomba, ila tunaweza tukaunganisha nguvu na kukubaliana ili kuona kura zetu zinahesabiwa na matokeo halali yanapatikana,” anasema.

Kuhusu sekta ya habari, Lipumba ameahidi kuwa serikali yake itahakikisha Tanzania inakuwa na sheria ya haki ya kupata habari, jambo ambalo amesema serikali ya Kikwete imeshindwa kushughulikia.

Ameahidi kuweka uwazi kuhusu mali za viongozi na kuhakikisha Watanzania wananufaika na utajiri wa maliasili na rasilimali za nchi kwa kuweka sera, mikakati na mipango endelevu.

0
No votes yet