Prof. Mbwette atishia MwanaHALISI


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
MAKAMU Mkuu wa OUT, Profesa Tolly Mbwette

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwette ametishia kushitaki MwanaHALISI iwapo litaendelea kuanika kashfa za chuo hicho.

Mawakili wake, Esco Law Chambers ya Dar es Salaam, katika hati shinikizi ya tarehe 27 Juni 2012, wanasema gazeti limekuwa likichapisha, katika matoleo ya hivi karibuni (bila kuyataja) “taarifa za kashfa dhidi ya mteja wetu.”

Wamesema wana maelekezo rasmi kutoka kwa mteja wao kufungulia gazeti mashitaka iwapo litaendelea kuandika taarifa za aina hiyo.

Kwa mujibu wa hati, Prof. Mbwette anasema kuwa anaamini bado kuna habari nyingine za “kashfa” zinakusudiwa kuchapishwa na gazeti hili.

Hatua hii ya Prof. Mbwette imetokana na taarifa zilizowahi kuchapishwa na gazeti hili kuhusu ufisadi wa fedha za chuo unaofanywa na baadhi ya watumishi.

Taarifa zilizochapishwa zilianika wizi wa zaidi ya Sh. 800 milioni kwenye chuo hicho cha umma ambapo Sh. 500 milioni ziliibwa katika idara ya malipo ya mishahara; na Angelus Mlekaria kutajwa kama mtuhumiwa mkuu.

Kiasi kingine cha Sh. 300 milioni ziliibwa kutoka fedha za mikopo ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ambapo James Rweikiza, aliyekuwa mhasibu na mkuu wa kitengo, ametajwa kuwa mtuhumiwa.

Taarifa hizo zilieleza zaidi kuwa licha ya uongozi wa chuo kufahamu suala hilo, kulikuwa na ugumu wa kulifuatilia ili wanaotuhumiwa washitakiwe mahakamani.

Gazeti lilinukuu taarifa kwamba, pamoja na wizi huo, Prof. Mbwette aliamua kuagiza watuhumiwa warudishe tu fedha ili wasishitakiwe, hatua aliyosema si ngeni na kwamba alistahili “kupongezwa kwa ubunifu.”

Alisema hata Rais Jakaya Kikwete alifanya hivyo katika sakata la ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika taarifa hizo, Prof. Mbwette alihojiwa na gazeti hili, na maelezo yake yalinukuliwa kama sehemu ya habari hizo zilizochapishwa.

Sasa gazeti hili limepata taarifa nyingine kuhusiana na ufisadi mkubwa unaotajwa kufikia Sh. 2 bilioni.

Fedha hizo zimeibwa kwa nyakati tofauti, kwa mtindo wa wizi kila mwezi, kati ya mwaka 2008 na 2012.

Ufujaji huo wa fedha za umma ulibainika baada ya mmoja wa wafanyakazi kutoa taarifa juu ya ubadhirifu wa fedha za mishahara.

Hata hivyo, taarifa zinasema fedha hizo walilipwa “viongozi” kama posho.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MwanaHALISI limeona, sehemu kubwa ya fedha zilizolipwa kwa viongozi, ni pamoja na mishahara ya watumishi, ama waliofariki dunia au kuacha kazi, lakini majina yao bado yalikuwa kwenye orodha ya malipo Hazina.

Taarifa zinasema mishahara ya wafanyakazi hao inaendelea kulipwa, lakini chuo hakikuwa kinairudisha Hazina kama taratibu za serikali zinavyoelekeza.

Aidha, uongozi wa chuo unadaiwa kuamua kutumia fedha za mishahara ya watumishi waliofariki na, au kuacha kazi, ili kulipa viongozi wa juu wa chuo posho mbalimbali kila mwezi, badala ya posho hizo kutoka kwenye fungu la Matumizi Mengineyo – Other Charges (OC).

Gazeti halikuweza kupata mmiliki wa kampuni iliyofanya ukaguzi wa nje (jina tunalo) kutoa maelezo yake kuhusu taarifa ya ukaguzi aliofanya na ambayo baadhi ya wafanyakazi wanatilia shaka iwapo ilizingatia wanachoita “uoza wa OUT.”

“CAG – mkaguzi na mdhibiti mkuu wa fedha za serikali – anashughulikia huko tu; mbona huku kwetu haji?” amehoji mtoa taarifa.

Mwandishi: Kwani mkaguzi si mkaguzi tu? Huyu tayari amemaliza kazi.

Jibu: Kisheria na kiutaratibu, mashirika na taasisi zote za umma ukaguzi wake hufanywa na CAG. Hakuna taarifa yoyote iliyotoka kwa CAG kuonyesha aliteua kampuni kufanya kazi ya ukaguzi maalum - special audit.

Mwandishi: Si taarifa ni taarifa tu na zimepelekwa kwa CAG?

Jibu: Siamini…sidhani hivyo. Hakuna utaratibu wowote wa manunuzi uliofanywa kama Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 inavyoelekeza. Sidhani kama watadiriki kwenda kwa CAG.

Mtoa taarifa anasema hakuna tenda iliyotangazwa; akifafanua kuwa hakukuwa na “proforma invoice wala quotations zilizoshindanishwa.”

Anasema Sh. 23.3 milioni alizolipwa mkaguzi “…hazikuwa na value for money” – hazikulingana na thamani ya kazi iliyofanywa, kama ipo.”

Taarifa zinasema ukaguzi kifedha ulikuwa haujafanyika OUT tangu mwaka 2007.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo MwanaHALISI limeona, posho zilizolipwa Juni 2008 ni Sh. 7,331,283.48.

Mchanganuo wake katika fedha hizo, ni uwajibikaji (Sh. 5,197,491.36); Umeme (Sh. 790,000); Maji (Sh. 471,552.12); Simu (Sh. 430,000); nyumba (Sh. 70,000) na kukaimu (Sh. 372,240).

Kwa Juni 2009 posho zilizolipwa ni Sh. 27,748,940.16. Chini ya mchanganuo wa uwajibikaji (Sh. 25,596,185.25); Umeme (Sh. 790,000); Maji (Sh. 560,513.91); simu (Sh. 430,000 na kukaimu (Sh. 372,240).

Taarifa zinasema posho ziliongezwa mwezi hadi mwezi. Sh. 37,221,935 zililipwa kwa mwezi Juni 2010 kutoka kwenye fungu la mishahara.

Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: posho za kuwajibika Sh. 28,911,969.25; utaalamu Sh. 3,517,545; Umeme Sh. 790,000; ankara za maji Sh. 791,790.47; gharama za simu Sh. 430,000 na kukaimu 372,240.

Taarifa za kimahesabu zinaonyesha Desemba 2010 posho zilikuwa Sh. 37,011,877.00; Januari 2011 (Sh. 37,118,987.00; Februari 2011 (Sh. 38,439,700.00; Machi 2011 Sh. 38,694,851.50 na Aprili 2011 Sh. 37,221,935.00.

Kwa mwezi huo wa Aprili 2011, mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: posho za uwajibikaji (Sh. 29,302,690); wataalamu (Sh. 1,995,615); Umeme (Sh. 850,000); Maji (Sh. 844,207.26); Simu (Sh. 765,000); na kukaimu (Sh. 372,240).

Prof. Mbwette ameulizwa juu ya madai kuwa amekuwa akichukua posho lakini kwa kutumia meneja au msaidizi wake. Amejibu, “Hizo ni fitina.”

Ameulizwa kuhusu madai ya mtoto wake, Grace Mbwette, kupelekwa kusoma Afrika Kusini, kama ni stahili yake au ni upendeleo.

Prof. Mbwette amesema Grace amepata sifa; na akasisitiza, “Inawezekana vipi kumzuia mtu mwenye vigezo kwenda kusoma?”

Alipoombwa kuelezea kile kilichoitwa “…mpango wote wa ufujaji fedha za umma chuoni,” aling’aka. “Hapa sioni kama kuna habari zaidi, naona ni vita. Tena vita kali ya wivu.”

Mhariri: Tunashikilia msimamo wetu; na taarifa hizi ni kwa maslahi ya umma.
0
No votes yet