Prof. Safari: Saa ya ukombozi ni sasa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Profesa  Abdallah Jumbe Safari

UAMUZI wa mwanaharakati maarufu wa haki za waislamu,  Profesa Abdallah Jumbe Safari (59) kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), umetikisa siasa za Tanzania.

Hatua yake kujiunga na CHADEMA inalenga siyo tu kuimarisha safu ya juu ya chama hicho, bali pia kuzima propaganda kwamba chama hicho ni cha wakristo na cha kikanda.

Katika mahojiano na gazeti hili mara baada ya kujiunga na CHADEMA Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam, Prof. Safari anasema, uamuzi wake wa kujiunga na CHADEMA umetokana na sababu tatu kubwa. Kwanza, “CHADEMA ni chama makini; na chenye mkakati mahususi wa kuleta mabadiliko.”

Pili, Prof. Safari anasema, “Ni uimara wa safu yake ya uongozi; na tatu ni malengo ambayo chama hicho na viongozi wake wamejiwekea katika kuhakikisha kile wanachokilenga kinafanikiwa.”

Kabla ya kujiunga na chama hicho alifanya uchunguzi juu ya mambo mengi yanayosemwa kuhusu CHADEMA na akagundua kuwa ni propaganda tu. Kazi iliyoko mbele yake ni kusaidia kuondoa dhana chafu ya udini na kuimarisha mikakati ya mabadiliko nchini.

Anasema, “Ninafahamu kuwa kuna propaganda za udini zinazoendeshwa dhidi ya CHADEMA jambo ambalo si la kweli. Wanaoeneza propaganda hizi chafu ni walio madarakani kwa lengo la kuwatia watu ujinga ili wazidi kuwatawala.

“Watanzania wametiwa dozi hii mbaya ya udini kwa muda mrefu na sasa nitazunguka kila mahali nchini ili kutoa dozi mpya itakayoondoa dozi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya udini,” anasema Prof. Safari.

Januari 20, mwaka huu, Prof. Safari alitangaza rasmi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam uamuzi wake wa kukihama Chama cha Wananchi (CUF) alichojiunga nacho mwaka 1995.

“Nimeamua kutoka CUF lakini sijapanga kujiunga na chama chochote kwa sasa. Nilijiunga na CUF kwa sababu niliamini katika itikadi yake ya Haki Sawa kwa Wote ambayo naona sasa wameachana nayo,.

“Nitajiunga na chama ambacho kitafuata haki. Mimi ni mwislamu na siasa ni sehemu ya imani yangu,” alisema katika mazungumzo yake na MwanaHALISI.

Ijuma iliyopita, Prof. Safari alitua CHADEMA akisema, “Taifa hili ni letu wote. Nikiwa msomi na mtu ninayeipenda nchi yangu, dhamira yangu imenikataza kubaki nje ya ulingo wa kisiasa. Ndiyo maana mara baada ya kuombwa na wenzangu katika CHADEMA na kutafakari kwa makini ombi lao, nimekubali kujiunga nao ili kuendeleza harakati za ukombozi wa taifa hili.”

Anasema kabla ya kujiunga nao alifanya mazungumzo ya kina na viongozi wake wakuu na wakafikia makubaliano kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa ambayo anapenda yawe ajenda za msingi za chama hicho.

Kwanza alitaka kujua msimamo wa CHADEMA kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali; pili suala la udini ambao waislamu wamekuwa na madai ya muda mrefu dhidi ya serikali na hayajatekelezwa; na tuhuma kuwa chama hicho ni cha ukanda.

“Nimebaini kuwa kumbe hata CHADEMA nao wanaamini kuwa uuzwaji wa nyumba za serikali ni wizi wa mali ya umma na zinapaswa kurejeshwa serikalini.

“Nikabaini pia kuwa CHADEMA inataka usawa miongoni mwa Watanzania na hakina ubaguzi wa kidini wala ukanda kama inavyodaiwa. Hayo yote nimeyathibitisha mwenyewe,” anasema.

Umaarufu

Msomi huyo wa kiwango cha shahada ya uzamivu (PhD) katika sheria aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Sussex nchini Uingereza, amejipatia umaarufu mkubwa kwa utetezi aliojenga kisheria katika kesi kadhaa kubwa zikiwemo za kidini hapa nchini.

Mwaka 2001, alisimamia kesi maarufu ya Jamhuri dhidi ya Hamisi Rajabu Dibagula aliyehukumiwa kifungo cha miezi 18 kwa kosa la kusema Yesu si Mungu.

Prof. Safari na mwanasheria mwenzake Twaha Taslima, walimtetea Dibagula katika Mahakama Kuu na kushinda kesi hiyo, baada ya kukaa gerezani kwa miezi miwili.

Ni Prof. Safari aliyemtetea aliyekuwa Amiri wa Shura ya Maimamu nchini, Sheikh Juma Mbukuzi, katika kesi yake ya mwaka 1999, aliyoshitakiwa mahakamani na serikali kwa madai ya uchochezi.

Sheikh Mbukuzi akizungumza na waandishi wa habari katika msikiti wa Mkwajuni jijini Dar es Salaam  alieleza namna serikali ilivyokandamiza haki za waislamu tangu wakati wa uhuru na serikali ikamfungulia kesi ya uchochozi. Mbukuzi alishinda kesi hiyo.

Vilevile ni Prof. Safari aliyewatetea wanaharakati maarufu wa kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na mwenzake Sheikh Mussa Kundecha, waliofunguliwa kesi wakidaiwa kumuua muuza nyama wa Manzese jijini Dar es Salaam aliyefahamika kwa jina la Mtunguja.

Kwa hiyo, kujiunga kwake na CHADEMA kunakusudia kufuta dhana iliyoenezwa na inayomshangaza pia wakili huyo wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa waislamu wanatakiwa kuongozwa na mwislamu mwenzao hata kama hana maadili.

Katika hilo Prof. Safari anasema vitabu vitakatifu vya dini yake, ipo hadithi ya wakati mmoja ambapo wafuasi wa Mtume Muhammad (S.A.W) pale Makkah walipata taabu sana kiasi kwamba wakakimbilia Abbysinia (sasa Ethiopia).

“Wakati ule, Mfalme wa Abbysinia alikuwa anaitwa Najash wa madhehebu ya Katoliki, lakini alikaa nao vizuri kuliko kule Makkah ambapo watawala walikuwa waislamu. Hivyo mtume hakuogopa kuwapeleka makureishi wake kwenye utawala wa Mkatoliki. Waislamu wanataka kiongozi mwadilifu na si lazima awe wa dini yao,” anasema.

Miongoni mwa mambo ambayo Prof. Safari anasema yamemfurahisha katika chama chake kipya ni ukweli kuwa viongozi wake wastaafu kama vile Edwin Mtei na Bob Makani, bado wanaheshimika jambo ambalo ni tofauti na vyama vingine.

Prof. Safari ni mtu wa vipaji vingi. Ni mwanasheria aliyebobea, ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na mtunzi wa vitabu vya riwaya na vya taaluma yake ya sheria.

Baadhi ya vitabu tayari ameandika ni Mashitaka ya Jinai na Utetezi; Kabwela; Harusi; Joka la Mdimu; Msomi; Examination of Witness in Trials; Uandishi wa Manufaa, na Ndani ya Treni.

Tofauti na wanasheria wengi ambao hujisikia fahari kwa kuzungumza Kiingereza, Prof. Safari hujisikia fahari zaidi kuzungumza kwa Kiswahili. Katika mazungumzo yake na gazeti hili, alisema baba yake mzazi ndiye mtu aliyemsababishia mahaba makubwa na lugha hiyo.

“Nimeingia kwenye harakati upya lakini nitatenga muda kidogo kwa ajili ya kuandika vitabu. Vitabu ni muhimu lakini ili wananchi wasome vitabu kwa wingi ni lazima wale na kushiba kwanza. Kwa hiyo tutafanya kwanza kazi ya kuhakikisha wananchi wanapata mahitaji yao ya msingi,” anasema profesa huyo.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: