PROF. TIBAIJUKA: Natumia sheria kudhibiti mafisadi ardhi


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MIONGONI mwa wizara ngumu kuongoza tangu Tanzania ipate uhuru miaka 50 iliyopita, ni inayosimamia masuala ya ardhi, majengo na maendeleo ya makazi.

Kumejaa migogoro, mingine ikiwa imeleta vifo kufuatia mapigano ya wanaogombania maeneo.

Tangu enzi hizo, matatizo ya ardhi yamekuwa yakipiga hodi ikulu, lakini mkuu wa sasa, Rais Jakaya Kikwete akaona vizuri apate msaidizi makini makini aliyekuja kwa jina la Profesa Anna Tibaijuka.

Ukiacha sifa ya usomi, uzoefu wake katika nyanja hiyo na utashi wa kutenda anachoamini kizuri, zinamsaidia sana kuwajibika.

Prof. Tibaijuka amekuwa mwalimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako bado anahitajika; ametumikia Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habibat) kwa miaka 10 katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu kabla ya kushika wakati huohuo, nafasi ya  Mkurugenzi Mkazi wa Ofisi ya UN mjini Nairobi.

Alistaafu Julai mwaka jana na kuingia moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro cha ubunge, Muleba kaskazini alikoibuka mshindi.

Baada tu ya kuteuliwa kuwa waziri, Prof. Tibaijuka alianza kazi kwa kasi akikagua maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam.

Alipomaliza ukaguzi, alitamka kunyang’anya viwanja Ocean Road, Palm Beach, Jangwani Beach na Mbezi Beach. Baadhi ya wanaodai ni wamiliki, walikimbilia mahakamani.

Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI wiki iliyopita Dar es Salaam, Prof. Tibaijuka alikiri, “Kazi hii ni ngumu. Unapambana na watu wa tabia mbalimbali; nyingine za kutisha. Lakini nasema mimi siogopi. Nitapambana nao kwa sheria siyo mabavu waliyozoea.”

Anazungumzia kasi aliyoanza nayo mara tu alipokabidhiwa wizara Novemba 2010, akisema, “Wakati ule ulikuwa ni moto wa kuingia wizarani; nikitaka kuonyesha kuwa sitakubali kupindisha sheria.”

Prof. anasema, “Jeuri ya sasa tofauti na ile ya mwezi wa pili na tatu. Wakati ule sikuwa na nyenzo za kutosha, lakini sasa nina jeuri ya bajeti ambayo imenipa nguvu nyingi za kutenda kazi niliyopewa na rais wetu. Sasa nayajua mambo mengi. Najua nini tupange na lini; huku tukipima matokeo yanaweza kutupa nini.”

Anajivunia mafanikio ya bajeti yake kupitishwa na bunge mwezi uliopita kwamba “nimeaminiwa kiutendaji. Sasa wametupa fedha, tunafanya kazi waliyoidhinishwa itendwe,” anasema.

Hivi Prof. Tibaijuka hahofii hata wale wenye fursa ya kumfikia rais ambaye ndiye aliyemteua?

Anajibu, “Nina baraka za huyo huko (juu) wanakokimbilia (kwa rais). Hata wabunge wamekubali mipango yetu.”

Anasema anafahamu baadhi yao (mafisadi wa ardhi) wanatumia ushawishi mwingi kumvuruga ili kukidhi maslahi yao. “Najua vizuri; lakini nasema hawatuwezi. Nimeanza kazi rasmi.”

Katika mazungumzo yaliyofanyika mara tu baada ya kukutana na waandishi wa habari alipotamka kufutwa kwa hati 42 za viwanja ndani ya jiji la Dar es Salaam, Prof. Tibaijuka anaahidi kutenda kwa umakini.

Lakini kuna taarifa kwamba baadhi ya maofisa ardhi wa Halmashauri na Manispaa mbalimbali nchini wamekuwa chanzo cha matatizo na migogoro ya ardhi yanayosababishwa na utoaji hati bandia.

Kuhusu hili anasema, “Ndiyo maana nasema nimeanza kazi. Hili la halmashauri nimesema kuna tuhuma za baadhi ya maofisa wetu kuhusika. Tatizo hili tunapambana nalo kwa nguvu na litakwisha.”

“Sasa hivi wizara ikigundua tu chanzo cha mgogoro fulani wa ardhi ni ofisa wetu katika halmashauri au manispaa, tunamnyang’anya madaraka na kumrudisha wizarani. Anayedhani nimelala amekosea sana,” anasema.

Kadhalika, Prof. Tibaijuka anajua namna migogoro ya ardhi ilivyokithiri katika Wilaya ya Kinondoni. Anajua zipo hati feki zinatolewa na maofisa wa serikali kwa wavamizi na waporaji ardhi.

Takwimu walizonazo wizarani zinaonyesha kati ya maeneo 110 katika wilaya hiyo, 88 yameshavamiwa.

Usidhani anatafuta takwimu hizo kwenye makaratasi. Anatoa kichwani; na hiyo inathibitisha namna alivyoshiba taarifa za maeneo yaliyo chini ya usimamizi wa wizara yake.

Manispaa ya Ilala haijasalimika katika tatizo hilo. Anasema wakaguzi wake wamefanyia kazi maeneo 30 ya wazi. Kati yake, 11 yamevamiwa.

Kwa manispaa ya Temeke, anasema maeneo yaliyokaguliwa yanafikia 14. Matano yamebainika kuvamiwa na waporaji waliosaidiwa na mafisadi wa ardhi kutoka serikalini.

Anasema msimamo upo tangu zamani kwamba kisheria, mtu haruhusiwi kujenga mjini bila ya kibali cha maandishi kilichotolewa na mamlaka za mipango miji hata kama alipata eneo hilo kihalali.

“Maisha ya ujanjaujanja jijini Dar es Salaam kupitia ufisadi wa ardhi, sasa basi,” anasema na kuongeza mwenye malalamiko ayafikishe kwa Kamishna wa Ardhi.

Akizungumzia madai ya baadhi ya wakazi wanaopinga ubomoaji wa majengo kando ya Barabara ya Morogoro, Prof. Tibaijuka anasema, “Serikali haikurupuki.”

“Nadhani, mheshimiwa Dk. John Magufuli, anakwenda nalo sawa maana naona utaratibu uko wazi,” anasema akimhusisha waziri huyo wa ujenzi.

“Anayedhani anaonewa aende mahakamani lakini lazima awe na vielelezo, vinginevyo atapoteza tu muda wake,” anasema.

Kuhusu madai ya watu wanaopinga kubomolewa nyumba zao eneo la Kurasini ili panapohitajika kwa kazi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Prof. Tibaijuka anasema:
“Hilo linashughulikiwa… tayari niliagiza wataalamu kupima upya eneo hilo ili kumaliza malalamiko yao.”

Wakazi wa Kurasini wanadai mratibu wa mradi huo, anayetajwa kwa jina la John Mhando, ni chanzo cha migogoro yote inayohusu ulipaji na fidia. Wanashinikiza afukuzwe kazi.

Prof. Tibaijuka ambaye ni mbunge wa Muleba Kusini, mkoani Kagera, ana malengo katika utumishi wake kwa umma akiwa katika nafasi hiyo. Mojawapo ni kutaka kuwapa Watanzania makazi bora.”

Atafanyaje? “Aaah… tunatarajia kupata fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ambazo zitakopeshwa kwa wananchi wa kipato cha chini.

“Tumezungumza pia na Hazina ili kuweka fedha kwa ujenzi wa nyumba bora za wananchi kwa ushirikiano na shirika letu la nyumba. Mambo haya yanawezekana hata tukialika kampuni zinazotoa mikopo ya nyumba," anasema.

Amegusia hilo akikiri kuwa Tanzania ina upungufu wa nyumba 3,000,000 (milioni tatu) na kwa kuwa gharama za ujenzi ni kubwa, wananchi wanastahili kuwezeshwa ili kujenga nyumba za kisasa.

Upungufu huo unakua kwa sababu takwimu zinasema kila mwaka kunaibuka mahitaji ya nyumba 200,000 kutokana na upanukaji miji nchini.

“Ndiyo maana wizara ipo pamoja na Shirika la Nyumba katika kuboresha makazi. Maeneo muhimu hayauzwi ili kuiacha NHC ijenge makazi ya kutosheleza kiu ya wapangaji au familia mbalimbali,” anasema.

Katika malengo hayo, profesa anaonya watu wanaohodhi ardhi kwa muda mrefu bila kuiendeleza, kuwa watanyang’anywa.

Waziri anakumbusha alichokieleza bungeni kwamba wizara itapitia hati za maeneo mbalimbali yasiyoendelezwa kwa zaidi ya miaka mitatu, na kuchukua hatua za kisheria.

Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka alizaliwa mwaka 1950 Muleba, Kagera. Nafasi ya ukuu wa UN-Habitat ilikuwa kubwa kushikwa na mwanamke barani Afrika.

Ni mtaalamu wa kilimo-uchumi, mwenye uwezo wa kuzungumza lugha nne za kimataifa kwa ufasaha – Kiswahili,  Kiingereza, Kiswidi na Kifaransa na mwenye kuongea kwa uhakika wa anachosema na kusimamia.

0
No votes yet