Profesa Haroub Othman: Ameondoka akiwa bado anahitajika


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

INNA Lillah Wa Inna Illaih Rajiuun, hakika kwake tumetoka na kwake ndiko tutarejea. Profesa Haroub Miraj Othman, ametutoka na ametangulia kule ambako sote tutakwenda.

Imenichukua muda mwingi kufikiria namna ya kuanza makala hii. Kila ninapotafakari kifo cha Profesa Haroub Othman Miraj, napata simanzi na huzuni nyingi.

Kifo chake kimebadilisha fikra na mwelekeo wa mada nilizopanga kuchambua katika safu hii. Ni kawaida kwa mwandishi mchambuzi kwenda na wakati. Pale anapofikiria kuandika kitu, lazima aangalie ni kitu gani muhimu, kinatokea au kimetokea katika jamii anayoiandikia.

Hivi sasa hapa Zanzibar, hakuna kama kifo cha Profesa Haroub, mtaalamu wa sayansi jamii aliyebobea, mpenzi wa haki za binadamu na demokrasia. Ni profesa wa kila kitu, na kwangu, Profesa Haroub ni mtu wa amani.

Kufikia leo, watu wengi wameandika kumzungumzia. Nami ninafanya hivyo. Ninayajua mengi na kwa kiasi chake, nilikuwa karibu naye kama mwalimu, mpenda haki, mwanaharakati na mzalendo wa kweli kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Namuona Profesa Haroub kama mfano wa wale manabii wasiopendwa au kukubalika wanakotoka. Kwa hulka yake, na mapenzi yake kwa nchi na watu wake, Profesa alikera watawala, hususan wa Zanzibar.

Alizaliwa na kukulia Baraste Kipande, mtaa maarufu mjini Unguja kwa watu wa fani mbalimbali, ikiwemo siasa. Wanaomjua zaidi, wanasema hata yeye alikuwa mwanasiasa, ingawa si katika kiwango cha kuanzisha au kushabikia chama. Baba yake, Miraj Othman, alipenda kucheza na siasa pamoja na watu wa umri wake, waliokuwa wanasiasa.

Namtazama Profesa Haroub kama nguzo kuu iliyokatika ghafla katika ujenzi wa demokrasia, haki, amani na utengamano visiwani Zanzibar, Tanzania, Afrika na duniani kwa jumla, hasa kule ambako wananchi wanaendelea kudhalilishwa na kuonewa.

Baada ya kuhangaika kielimu, akiwa miongoni mwa vijana waliokwenda kusoma nje miaka ya kabla ya uhuru wa Zanzibar wa 10 Desemba 1963, zaidi katika nchi za iliyokuwa Ulaya Mashariki, alijunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alifundisha hadi kuwa mtu maarufu miongoni mwa vijana wasomi wa Tanzania, mashariki na kusini mwa Afrika.

Nilianza kumfahamu kwa karibu mwaka 1992, akiwa mwanzilishi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar – Zanzibar Legal Service Centre (ZLSC). Walikuwa na Profesa Chris Peter Maina, Fatma Alloo na Askofu Douglas Toto wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, ambaye alifariki dunia mwaka juzi.

Nilialikwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kituo hiki nikiwa mwandishi mkuu, mwakilishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Marehemu Francis Nyalali, akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania, alialikwa kama mgeni rasmi.

Profesa Haroub alisema kituo kinakusudiwa kuwa daraja kwa jamii katika kujua haki zao na namna wanavyoweza kusimama kuzidai.

Lakini kama kuna kitu ambacho kazi ya Profesa Haroub ilitafsiriwa kama dhambi kubwa na wakuu wa serikali ya SMZ, basi ni ile ya uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Kupitia Zanzibar Election Monitoring Group (ZEMOG), Profesa Haroub alitoa ripoti iliyoelezea kinagaubaga yaliyotokea wakati wa mchakato wa uchaguzi huo na ikashutumu mashirika yaliyoutambua uchaguzi.

Ripoti hiyo ilizua makubwa dhidi yake. Alisemwa, akashutumiwa, akalaumiwa na kukebehiwa na viongozi waandamizi wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar. Matamshi yao yalichukuliwa na Profesa Haroub kama kitisho kwa usalama wake na dhamira yake ya kujitahidi kujenga jamii inayopenda haki na usawa kwa wote.

Ni ripoti hii iliyosababisha aogope kufika Zanzibar, ikiwemo kufuatilia shughuli za kituo ambacho yeye alikuwa ndiye mwenyekiti wake.

Ilimchukua karibu miaka mitano hadi alipoanza kujisikia salama kupanga safari ya Zanzibar.

Kituo hicho kinajulikana na wengi kwa kusaidia watu kudai haki zo, ikiwamo haki ya kupiga kura. Zaidi ya watu 100,000 wamepitia kituoni hapo kutafuta haki hiyo kila uchaguzi unapowadia. Ni utamaduni wa Zanzibar baadhi ya watu kunyimwa tena kwa makusudi haki ya kupigakura.

Wanasheria wa ZLSC wamesimamia watu hawa katika kufungua kesi za kudai haki hiyo mahakamani. Wangi wamepewa haki na mahakama lakini serikali ikawakwamisha kuandikishwa.

Kwa mwaka wa tatu mfululizo, kituo hicho kimefanikiwa kuchapisha ripoti ya rekodi ya haki za binadamu Zanzibar. Mwanzoni kilisaidiana na Kituo cha Huduma za Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) cha Dar es Salaam.

Msaada wa kituo unatambuliwa pia katika tatizo linalokua kwa kasi Zanzibar, lile la migogoro ya ardhi.

Profesa Haroub mapema mwaka huu alishutumu kitendo cha viongozi wa SMZ kuamuru na kusimamia uvunjaji makazi ya watu eneo la Tomondo, uvunjaji ambao baada ya utafiti waliofanya ZLSC, ilithibitika ulikiuka misingi ya utawala wa sheria.

Ijumaa iliyopita, nilikaa na Profesa Haroub kwa saa nzima kujadili matatizo ya ardhi. Tulikubaliana kushirikiana kutafuta chimbuko la migogoro hii, hasa kwa malalamiko yanayohusisha watu maarufu wanaofahamika kuwa na uhusiano na uongozi wa juu serikalini.

Jumamosi, siku ya mwisho, ambayo Profesa Haroub aliona jua, Wazanzibari, nikiwemo, walimsikiliza Profesa huyu akitoa maneno adhimu kuhusiana na demokrasia na umuhimu wa Wazanzibari kuenzi historia ya nchi yao.

Alihimiza watu wa umri mkubwa, akiwemo Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye alikuwa mgeni rasmi, kuandika mambo wanayoyajua katika historia, wala si katika nyanja ya siasa tu, bali hata katika elimu na utamaduni.

Profesa Haroub, ambaye siku hiyo alikuwa mzungumzaji mahsusi aliyepitia kitabu kilichoandikwa na Profesa Bughees, raia wa Marekani aliyepata umaarufu mkubwa, kwa kujenga mlahaka mzuri na Wazanzibari wengi tangu miaka ya 1990, alisifu kazi iliyofanywa na mwandishi huyo kupitia simulizi za komredi maarufu visiwani Zanzibar, Ali Sultan Issa (waziri wa zamani wa Elimu) na Maalim Seif Shariff Hamad.

Profesa ni mwandishi wa habari, hasa ambaye alianzisha Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Uchina mwaka 1957.

Akiwa na waandishi wa habari, miezi michache mjini Zanzibar, alizungumzia sana demokrasia na akasema, “Nina hamu ya kuona uchaguzi huru na wa haki unafanyika Zanzibar.” Labda alijua siku zake zinakwisha.

Kauli hiyo na maneno yake adhimu katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, ndiyo hasa yaliyoumiza mioyo ya wananchi wengi wa hapa, kiasi cha kumzika kwa maelfu shambani kwao Chuini.

Wazanzibari tunamlilia kaka na mwalimu wetu; wanamlilia mweledi na mwanaharakati mahiri; wanamlilia kipenzi cha jamii. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi Profesa Haroub Othman - Amin.

0
No votes yet